Na Mwandishi wetu,
Songea


WANANCHI wa kijiji cha Lyangweni kata ya Litapaswi Halmashauri ya wilaya Songea mkoani Ruvuma,wameanza kupata huduma ya maji ya bomba kwa mara ya kwanza tangu nchi ipate Uhuru.


Hatua hiyo imekuja baada ya serikali kupitia wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) wilaya ya Songea, kukamilisha ujenzi wa mradi wa maji ya bomba uliogharimu Sh.milioni 618.


Kukamilika kwa mradi huo,ulianza kutoa huduma ya maji kwa wananchi 2,159 wa kijiji hicho kumeleta nafuu kubwa kwa wananchi ambao kwa muda mrefu walitembea zaidi ya kilomita 3 kila siku kwenda kuchota maji kwenye mito na vyanzo vingine vya asili.


Mhandisi wa maji kutoka ofisi ya meneja wa Ruwasa wilaya ya Songea Triphon Mwanangwa alitaja kazi zilizotekelezwa katika mradi huo ni ujenzi wa tenki la kuhifadhi maji la lita 100,000 kwenye mnara wa mita 4 na ujenzi wa vituo 11 vya kuchotea maji.


Mwanangwa alisema,kazi nyingine zilizotekelezwa ni pamoja na uchimbaji wa mitaro na ulazaji wa bomba za kusambaza maji umbali wa kilomita 14 na ujenzi wa chanzo cha maji.


Aidha alisema,chanzo cha mradi huo ni kisima kirefu chenye urefu wa mita 130 chenye uwezo wa kuzalisha lita 168,000 kwa siku huku mahitaji ya maji kwa wananchi wa kijiji hicho ni lita 159,000 kwa siku.


Alitaja faida zinazopatikana baada ya kukamilika kwa mradi huo ni kupunguza magonjwa yanayotokana na matumizi ya maji yasio safi na salama ikiwemo homa za matumbo,kuhara,tyfodi, kipindupindu n ahata kuwapunguzia wananchi muda wa kwenda kutafuta maji mbali na makazi yao.


Kwa mujibu wake,baada ya mradi kukamilika wananchi wa kijiji hicho sasa wanapata muda mwingi kufanya shughuli zao za kujiletea maendeleo kama vile kilimo,biashara ndogo ndogo,ufugaji na shughuli nyingine za maendeleo.


Amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na serikali yake kwa kutoa fedha hizo kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa maji ya bomba ambao umewezesha kutimiza adhima ya kumtua mama ndoo kichwani.


Mwenyekiti wa kijiji cha Lyangweni Menrald Komba alisema,kukamilika kwa mradi huo kumewaondolea mateso makubwa wananchi kwa kutembea umbali mrefu kila siku kwenda kutafuta maji.


Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Kilawalawi Herman Komba alisema,chanzo cha maji kipo umbali wa mita 500 kutoka shuleni,hivyo pindi wanafunzi wanapotaka kwenda kuchota maji kwa matumizi ya kawaida wanatumia muda mwingi kwenda kuchota maji.


Alisema,hali hiyo iliwaathiri sana kitaaluma hasa katika ufundishaji watoto madarasani kwa sababu muda waliotakiwa kuhudhuria vipindi vya masomo waliutumia kwenda kuchota maji.


Mwanafunzi wa shule hiyo Silvesta Haule alisema,kabla ya mradi wa maji ya bomba kila siku tulikwenda mtoni kwa ajili ya kuchota maji,maji ambayo hayakuwa safi na salama kwa matumizi ya binadamu.

Mwanafunzi mwingine Pelgia Nikazi alisema,mradi wa maji ya bomba umewasaidia kutatua changamoto ya uchafu kwenye vyoo a mazingira ya shule uliotokana na ukosefu wa maji ya uhakika.
 

Baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi Kilawalawa kata ya Litapwasi wilayani Songea wakichota maji katika kituo mojawapo kinachotoa huduma ya maji kilichojengwa na wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)wilaya ya Songea baada ya kukamilika kwa ujenzi wa mradi wa maji ya bomba uliogharimu zaidi ya Sh.milioni 618.
 

Afisa mtendaji wa kata ya Litapwasi Halmashauri ya wilaya Songea mkoani Ruvuma George Chiwega kulia,akizungumza na wanafunzi wa shule ya msingi Kilawalawa katika kituo cha kuchotea maji baada ya kukamilika kwa mradi wa maji ya bomba uliotekelezwa na wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa).
 

Kaimu meneja wa Ruwasa wilaya ya Songea Mhandisi Triphon Mwanangwa kulia,akimtwishwa ndoo ya maji mwanafunzi wa shule ya msingi Kilawalawa kata yaLitapwasi Jesca Mligo,baada ya kukamilika kwa mradi wa maji katika kijiji cha Lyangweni wilayani Songea,wa pili kulia kaimu afisa habari wa Ruwasa mkoa wa Ruvuma Geddy Komba.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...