Na Janeth Raphael - MichuziTv - Dodoma


Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum amezindua rasmi Kamati ya Kitaifa ya ushauri kuhusu ulinzi na usalama wa mtoto mtandaoni sambamba na uzinduzi wa Kampeni ya Ulinzi na Usalama wa mtoto mtandaoni.

Akizungumza na washiriki waliohudhuria hafla hiyo Februari 10, 2024 jijini Dodoma, Waziri Dkt. Gwajima amesisitiza masuala muhimu kwa Wazazi au Walezi kuzingatia hasa kutimiza wajibu wao wa kulea watoto na kufuatilia kwa usahihi matumizi ya vifaa vya kielektroniki hasa wakati wa likizo ili mtoto kuwa salama mtandaoni.

“Wazazi au Walezi wekeni kiwango cha muda wa matumizi ya vifaa vya kieletroniki hasa luninga ili kukwepa janga la urahibu na kutoa muda kwa mtoto kufanya kazi za nyumbani na kujisomea. Hakikisha mtoto anatumia vifaa vya kielektroniki chini ya uangalizi wa karibu ili kutojiingiza katika mitandao ambayo ni hatari kwa usalama wa Mtoto. “

Aidha amewaasa Wazazi au Walezi, kuwaruhusu watoto kushiriki majukwaa yao yaani Mabaraza ya Watoto shuleni na Madawati ya ulinzi wa Watoto ili kujengeana uwezo wa masuala mbalimbali yanayowahusu.

Waziri Dkt. Gwajima amebainisha kuhusu utafiti uliyofanywa na Serikali kwa kushirikiana na Shirika la UNICEF mwaka 2022 kwa watoto wa Tanzania wa umri wa miaka 12 hadi 17 ulioonesha asilimia 67 ya watoto wanatumia mitandao na asilimia 4 ya watoto hao walifanyiwa aina tofauti za ukatili kwenye mitandao ikiwa pamoja na kukutana na wahalifu waliowasiliana nao kupitia mitandao.

Aidha, amesema katika kukabiliana na changamoto ya matumizi mabaya ya mtandao kwa watoto, Wizara kwa kushirikiana na Wadau Kamati hiyo ya Taifa ya Ushauri inayojumuisha Wakurugenzi au Wakurugenzi wasaidizi kutoka Serikalini, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na Sekta Binafsi pamoja na kikundi kazi cha wataalamu wa uratibu wa utekelezaji wa mpango kazi wa kuwalinda watoto dhidi ya ukatili wa mtandaoni.

Ameongeza pia, kampeni hiyo iliyozinduliwa inahusu kuelimisha watoto wenyewe, wazazi, walimu na jamii kwa ujumla kuhusu kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vya ukatili ikijumuisha usalama wa mitandaoni ambapo Kaulimbiu itakayoongoza kampeni hii ni Jukumu Letu; Chukua Hatua.Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...