WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Uchukuzi kusimamia ipasavyo Shirika la Ndege Tanzania ili kuhakikisha uwekezaji mkubwa uliofanywa unaleta matokeo chanya na kuwa kichocheo cha ukuaji wa sekta nyingine mtambuka na uchumi kwa ujumla wake.

Amesema kuwa ongezeko la ndege na huduma za usafiri inasaidia kuongeza fursa za biashara kati ya Tanzania na mataifa mengine kuongeza upatikanaji wa fedha za kigeni na kuongeza idadi ya watalii wanaokuja nchini.

Amesema hayo leo (Jumanne, Machi 26, 2024) alipomuwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye mapokezi ya ndege mpya aina ya Boeing 737-9 Max, kwenye uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam.

Aidha Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa ili kuendelea kuikuza sekta ya anga nchini, Wizara ya Uchukuzi iandae mpango wa kuongeza wataalamu wazalendo katika fani zinazohusu masuala ya ndege hususan katika eneo la matengenezo na urubani.

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amewataka watumishi wa Shirika la Ndege Tanzania kuongeza uzalendo na kuwafichua wale wote wenye nia ya kulihujumu shirika hilo pamoja na kudhibiti upotevu wa mapato kupitia tiketi na mizigo.

Pia, Amewataka viongozi na watendaji wa Shirika hilo wahakikishe ndege zote zinaendeshwa kwa tija kwa kufanya tafiti za kutosha wa masoko kabla ya kupeleka ndege

Amesema kuwa usafiri wa anga umekuwa chachu ya kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo na biashara. “Uwepo wa usafiri wa ndege umeongeza tija kubwa kwa wakulima hususan wa mazao ya mbogamboga na matunda, wafugaji na wafanyabiashara wa Kitanzania”

Katika Hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amesema katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya awamu ya sita imesaini mikataba ya miradi mipya 6 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 674.3 inayohusu ujenzi wa kiwanda cha kujengea meli (shipyard) katika Ziwa Tanganyika, ujenzi wa meli kubwa ya kubeba mizigo tani 3,500 na meli nyingine yenye uwezo wa kubeba tani 3,000 za mizigo ambayo inajengwa katika Ziwa Victoria.

Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amesema kuwa sambamba na ununuaji wa ndege za abiria na moja ya mizigo, Serikali imenunua ndege mbili za mafunzo kwa ajili ya Chuo cha Usafirishaji (NIT) ili kusaidia kuongeza idadi ya marubani kwenye soko la ajira na kupunguza uhaba wa marubani nchini.

“Pia NIT imewezesshwa mitambo na vifaa vya kisasa kwa ajili ya kutoa mafunzo ya shahada na Stashahada ya uhandisi wa ndege ili kuzalisha wahandisi na mafundi mchundo watakaoingia kwenye soko la ajira”

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) Mhandisi Ladislaus Matindi amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuijengea kampuni hiyo uwezo wa kutoa huduma kwa kuinunulia ndege mpya na kuijengea miundombinu wezeshi katika biashara ya anga.

“Hadi sasa Serikali imewekeza shilingi trilioni 2.4 katika ununuzi wa ndege, ujenzi wa mindombinu wezeshi ya kibiashara pamoja na ulipaji wa sehemu ya madeni yaliyolimbikizwa”

Ameongeza kuwa ATCL inaendelea kutekeleza mpango mkakati wake wa pili wa miaka mitano ulioanza mwaka wa fedha 2022/23 na kumalizia 2026/27 ambao pia unahusisha mpango wa maendeleo wa Taifa wa miaka mitano yaani 2021/22-2025/26 ambao unatarajiwa kuiwezesha ATCL kuwa na ndege 20 “Hadi sasa ATCL inandege 14 zilizonunuliwa katika kipindi cha ufufuaji”
Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...