--UNYENYEKEVU NA USTAHIMILIVU NDIO MSINGI WA MAFANIKIO YA UONGOZI

Na Derek Murusuri


1 MACHI, 2024: TULIKUWA tunahitimisha ziara ya Rais ya Mkoa wa Shinyanga mwaka 1993.

Tulikuwa kwenye msafara wa Rais Ali Hassan Mwinyi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1985-1995.

Mara, tukaambiwa Mhe Rais anataka kupiga picha na wapiga picha wake. Lol, sisi? Mbio tukaenda. Akatusalimia kwa kutushika mkono, akitushukuru kama baba kwa mwanaye.

Alifurahia jinsi habari zake na hasa picha, zilivyokuwa zikipigwa na kuchapishwa katika magazeti mbalimbali hapa nchini. Alikuwa mtu wa kushukuru.

Nami nilikuwa mmoja wa wapigapicha au photojournalists kutoka Idara ya Habari, MAELEZO. Bosi wangu, Raphael Hokororo alinipanga kwenye ziara hiyo.

Mhe Rais Mwinyi akatuita, "Njooni tupige picha ya ukumbusho."

Hima tukajongea. Akiwa na Mama Sitti Mwinyi, waliketi, sisi wapiga picha tukasimama nyuma yao.

Mpiga picha mmoja akatupiga picha sisi wapiga picha, pamoja na Mhe Rais na mkewe.

Baada ya zoezi hilo, akatuaga. Sio viongozi wote wanaojua kushukuru. Imagine. Rais anakushukuru kwa kutekeleza wajibu wako. Tena Kiongozi Mkuu wa Taifa. Halafu wewe ni mpiga picha tu.

Mwaka huo huo, nilifanya naye kazi Ikulu kwa wiki mbili na ushee hivi, chini ya Balozi Patrick Chokala.

Kipindi hicho, mpiga picha wake, Mzee Henry Isike, alikuwa likizo. Wakubwa wangu pia, walikuwa safari. Nilipomuomba asogee hivi, ili picha itoke vizuri, alikubali kwa unyenyekevu mkubwa sana.

Nikiwa Tume ya Mipango, iliyokuwa ofisi ya Rais, Rais Mwinyi ndiye aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mipango.

Nilihudhuria kikao kimoja cha Tume ya Mipango katika chumba cha Baraza la Mawaziri, Ikulu, nikashuhudia hekima yake kubwa ya kuendesha vikao. Alimsikiliza kila mwenye hoja, tena kwa umakini mkubwa.

Ulihitaji kuwa karibu na Rais Ali Hassan Mwinyi, ili unfahamu.

Alikuwa kiongozi mnyenyekevu sana, mvumilivu, mwana mageuzi, aliyeujenga upya uchumi wa Tanzania, baada ya kuharibiwa sana na vita ya Kagera na hata vita ya harakati za ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika.

Naweza kusema kuwa Mzee Ali Hassan Mwinyi alikuwa Deng Xiaoping wa Tanzania, kwa kipindi kile, kuanzia mwaka 1985. Deng ndiye Baba wa Uchumi wa China.

Aliwahi kupigwa kofi msikitini na kijana mmoja bastard tu hivi, kwa vile alikuwa anajichanganya na raia, lakini akamsamehe. Alishambuliwa sana kwa maneno mengi hadi familia yake ikashutumiwa, lakini, akanyamaza kimya.

Akaendelea kuchapa kazi. Akameza kibri chake. Akajishusha. Hakujitutumua, patachimbika , NO! Sio yule Baba. Alitoa kombe kwa mahasimu wake, yeye aka focus kwenye kazi ya kufanya MAGEUZI ya uchumi wa Tanzania.

Wakati huo, alikuwa Amir Jeshi Mkuu. Majeshi ya ulinzi na usalama vilikuwa chini yake. Hata kama Mahakama ni mhimili tofauti, lakini angeweza kushawishi ili mahasimu wake waadhibiwe, lakini hakuitumia nafasi yake wala maguvu yake kuwashikisha adabu mahasimu wake.

Yeye alikaa kimya. Akasamehe. Tena akafanya kazi na mahasimu wake. Akaondoa foleni za kununua sembe. Sabuni za kufulia na dawa za mswaki zilizokuwa adhim, zikawa zinapatikana kwa magendo zikajaa madukani.

Watu walifulia nguo sabuni za MAGWANJI, wenye bahati ya kuwa na mipapai, wakatumia majani yake kufulia nguo. Mzee Ali Hassan Mwinyi akanyamaza kimya ili aujenge upya uchumi wa Taifa la Tanzania. Akachapa kazi. Akawaamini watu. Hakuchukua maguvu yote peke yake. Nchi ikasimama.

Mzee Ali Hassan Mwinyi ni chuo. Yapo mengi sana ya kujifunza kutoka kwake. Hakika.

Alikuwa kiongozi makini na alijitoa sana kwenye mambo ya kijamii. Power Distance kwake ilikuwa kidogo. Yaani, alikuwa karibu na raia aliowaongoza.

Mbali na kufanya mazoezi ya kutembea kila siku, huenda ndiyo siri ya kuishi miaka 98 na miezi 9, takriban miaka 99, alijaaliwa na Mola wake kwa kuonesha maisha ya msamaha, alifundisha Kiswahi kwa kujitolea nchini Uingereza.

Mhe. Abdullah Ali Hassan Mwinyi, Mbunge wa zamani wa Afrika Mashariki, ambaye ni mmoja wa vijana wa Mzee Mwinyi, alipata kunieleza tukiwa Cardiff University, kuwa wakati Mzee Mwinyi akiwa Uingereza, alijitolea kufundisha Kiswahili kwa bidii sana.

Ndio maana BAKITA na vyombo vya habari vilimtumia vizuri hapa nyumbani. Alijua, tukiwa na lugha yetu, ikakua na kutumika hata kwenye Sayansi, Taifa litapata maendeleo makubwa.

Hili ni somo kubwa sana la unyenyekevu katika uongozi kwa Watanzania na waafrika wote.

Nadhani sio kwa viongozi wa kisiasa pekee, nahisi ni katika maisha ya kila mmoja wetu. Nyumbani, ofisini, katika jamii na Taifa.

Hata Nabii Issa Bin Maryam, Bwana Yesu Kristo, alijishusha na kunyenyekea sana. Kuna nyakati alinyamaza pasipo kusema neno lolote. Hakutumia uwezo wake wa kiungu kuwasaga adui zake.

Nimeamini, Mwenyezi Mungu huwapenda watu wanyenyekevu, wenye huruma na wacha Mungu.

Basi, ngoja Kiongozi wetu, Mzee wetu, Baba yetu, Rafiki yetu, apumzike kwa amani. Mzee wetu Ali Hassan Mwinyi, hakika aliutumia vizuri muda wake hapa duniani.

Kumbe humility ni msingi mkuu wa kiongozi bora na namna njema ya kuishi hapa duniani.

Hata alipolazimika kujiuzulu, ilifika mahali yeye na familia yake wakapatiwa hifadhi na rafiki wa karibu. Hakuwa mbadhirifu. Alikuwa mwadilifu. Lakini hakujisikia vibaya. Muda ulipofika, Mwenyezi Mungu akamkumbuka. Alikuwa mvumilivu sana.

Huyu Kiongozi wetu aliyeondoka hakika alikuwa binadamu wa pekee sana.

Nilifurahi kumuona, yeye na mke wake, Mama Sitti, wakitumia usafiri wa Daladala, Mwendo kasi. Nilifurahi sana. Hii ni ishara ya unyenyekevu. Hakuongelea unyenyekevu, maisha yake yalitangaza unyenyekevu.

Tena siku hiyo haikutangazwa kwenye vyombo vya habari kuwa Mzee Mwinyi atatumia usafiri wa Mwendo kasi, alifurahi kusafiri na Wananchi wa kawaida aliowaongoza. Alipenda maendeleo.

Alijaaliwa kipaji cha hekima kubwa. Kwa kweli ameacha funzo kubwa kwenye kada ya uongozi katika Bara la Afrika.

Mwenyezi Mungu, Muumba wa Mbingu na Ardhi, amjaaliye Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi, pumziko la amani, hadi tutakapoonana ya pili.

INNA LILLAHI WA INNA ILAYHI RAJIUN

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...