Na Mwandishi Wetu

SERIKALI imekitaka Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), kuweka mikakati ya kujiimarisha kiteknolojia, uvumbuzi na ubunifu ili kuendana na mahitaji ya soko la ajira ambayo yanakwenda kwa kasi.

Wito huo ulitolewa leo jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk. Hashil Abdallah, wakati wa mjadala wa Dira ya Maendeleo ya miaka 50 ya chuo hicho itakayotekelezwa hadi mwaka 2074.

Alisema chuo hicho kinapaswa kutoa elimu ambayo itakidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi kwa kuwa na wahitimu wenye weledi wa kutosha kupokelewa na waajiri popote watakapokwenda.

Alisema sekta ya biashara ni kiungo muhimu katika kukuza biashara nchini na kukuza uchumi hivyo sekta hiyo inapaswa kutoa elimu bora kwani ndio msingi wa maendeleo ya uchumi nay a kijamii.

Alikipongeza chuo hicho kwa kuendelea kufanya mageuzi yanayoendana wakati na teknolojia katika fani ya biashara na juhudi zake za kujenga uwezo wa kitaaluma na kiufundi kwa wanafunzi wa chuo hicho.

“Dira ya miaka 50 ya chuo cha CBE ambayo imeandaliwa kwa umahiri mkubwa na kwa kushirikisha wadau mbalimbali ni hatua muhimu katika kuhakikisha chuo hiki kinabaki kuwa imara katika kutoaelimu bora na kusaidia ukuaji wa biashara,” alisema

Alisema ni matumaini ya serikali kuwa iwapo dira hiyo itatekelezwa kwa ufasaha itasaidia kuleta mabadiliko makubwa kwenye sekta ya biashara na kwenye jamii kwa ujumla.

Alisema chuo hicho kinapaswa kuwa tayari kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza katika taasisiz a elimu ili kiwe na uwezo wa kubailika kwa haraka kukidhi mahitaji ya soko la ajira.

Mkuu wa chuo hicho, Profesa Edda Lwoga, alisema katika kampasi zake zote chuo hicho katika mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza na Dodoma kina jumla ya wanafunzi 19,000 na kwamba wamekuwa wakijitahidikutoan elimu kwa vitendo zaidi.

Aidha, alisema katika kutekelez dira yake ya miaka 50 walishaanza kufanya mageuzi ya kutoa nelimu kwa vitendo ambapo walifanikiwa kuanzisha program za uanagenzi ambapo wanafunzi husoma wakiwa wanafanyakazi kwa vitendo.

“Na napendaa kutoa taarifa kuwa tumeshapata ithibati ya program za uanagenzi na mwaka huu tutaanza na kozi za benki na metrolojia ambapo watakuwa nusu shuleni na nusu watakuwa kazini,” alisema Profesa Lwoga.

Alisema kwenye kozi ya metrolojia watashirikisha n Wakala wa Vipimo (WMA), ambapo wanafunzi watakuwa darasani kwa muda na watakwenda kufanyakazi.

Alisema CBE ilishaanzisha program atamizi kwa wanafunzi wenye ndoto za kuanzisha biashara kupelekwa mawazo yao ambayo huboreshwa na kupewa mafunzo ambayo hatimaye huwawezesha kufanya biashara hizo.

“Tumeshaanza sasa ni miaka miwili na wanafunzi wengi wameshajitokeza kusajili biashara na kampuni zao wakiwa bado chuoni na katika kuendana na mabadiliko ya teknolojia tumeshaanzisha masomo ya mtandao,” alisema

Profesa Lwoga alisema kwa kuanza wameanza kutoa Shahada sita za Uzamili kwa njia ya mtandao na kwamba wataongeza kozi ya biashara ya kimataifa na kozi ya ununuzi na ugavi.

“Tumeona mwitikio ni mkubwa sana kwasababu wanafunzi wetu popote pale walipo watajisajili kwa njia ya mtandao na watalazimika tu kuja hapa chuoni kwa ajili ya mitihani ya majaribio tu na mitihani ya mwisho,” alisema

Alisema dira yao ya miaka 50 inawakilisha maono ya wanafunzi na wadau wote wa chuo hicho kwani chuo kimejitahidi kushirikisha maoni ya watu wengi wakati wa kuandaa dira hiyo.

Alisema miongoni mwa sababu zilizochochea chuo hicho kuandaa dira hiyo ni mabadiliko ya teknolojia kama akili bandia, roboti na utandawazi.

“Tulifikiri namna gani ya kufanya chuo chetu kwenda kimataifa zaidi na kuendana na matarajio ya wanafunzi wetu, mabadiliko katika jamii na mabadiliko ya kiuchumi kwa hiyo tunapaswa kujenga miundombinu imara ya kiteknolojia kuendeleza program za mafunzo zinazotekeleza teknolojia ya kisasa,” alisema



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...