Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel John Nchimbi amesema mojawapo ya sera muhimu za chama tawala ni pamoja na Serikali zake zote mbili, kusimamia na kuamini katika misingi ya utawala bora.

Akizungumza na viongozi na wanachama wa CCM mjini Mpanda, Dk Nchimbi amesema chama hicho kina wajibu wa msingi wa kusikiliza kero za wananchi kwa kufuata utawala wa sheria bila kuingilia mashauri yaliyoko mahakamani.

Balozi Nchimbi amesema mojawapo ya wajibu wa CCM siku zote ni kuzihamasisha na kuziwezesha mahakama kuendelea kutenda haki muda wote na bila maamuzi yake kuingiliwa .

Balozi Nchimbi amesema hayo leo Jumamosi Aprili 13, 2024, alipokuwa akizungumza na viongozi, wanachama na wananchi mbalimbali waliofika kumlaki katika Ofisi ya CCM Mkoa wa Katavi, alipowasili mkoani humo, ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara katika mikoa ya Katavi, Rukwa, Songwe, Mbeya, Njombe na Ruvuma.

“Katika mambo tutakayoyashughulikia kama kero, hatutagusa yaliyoko mahakamani. Huo ndiyo utaratibu wa utawala bora. Mojawapo ya sera muhimu sana za CCM ni kusimamia utawala bora. Wakati wote wajibu wetu utakuwa kuzihamasisha mahakama zetu zitende haki bila kuziingilia katika uamuzi wake. Nchi inayotaka kufanikiwa lazima isimamie utawala bora,” amesema Balozi Dk. Nchimbi.

Katika ziara hiyo, Balozi Nchimbi ameambatana na Wajumbe wa Sekreterieti ya Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) Taifa, ambao ni Issa Haji Usi Gavu na Amos Gabriel Makala.

Viongozi hao watafanya mikutano ya ndani na hadhara katika maeneo atakayozuru kwa lengo la kukagua na kuhamasisha uhai wa CCM katika ngazi ya mashina na matawi ikiwa pamoja na kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 - 2025.

Aidha, Balozi Nchimbi ametoa wito kwa wana-CCM kuendelea kuwa mstari wa mbele kueleza masuala mbalimbali yanayoyotekelezwa na Serikali kupitia Ilani ya Uchaguzi ya CCM bila haya, huku akisisitiza kuwa chama hicho tawala kitaendelea kuisimamia Serikali.

"Wakati mwingine kinachotuponza sisi ni uvivu wa kutoeleza kazi zilizofanyika, tunatumia msemo wa tenda wema usingoje shukrani, lakini katika siasa shukrani zinatafutwa. Katika siasa lazima useme kama uliahidi katika miaka mitano, utafanya moja, mbili, tatu hadi nne, kadri moja inavyolitekeleza lazima useme umefanya,” amesema Balozi Nchimbi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...