Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema kuwa Serikali tayari imeshampata Mkandarasi na kusaini mkataba wa ujenzi wa barabara ya Kibada - Mwasonga - Kimbiji yenye urefu wa kilometa 41 kwa kiwango cha lami.


Aidha, Bashungwa ameeleza kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameridhia kuongezwa kwa ujenzi wa kilometa 10 katika barabara hiyo ya Kibada - Mwasonga - Kimbiji kwa kuinganisha na kipande kilichobakia cha Kimbiji hadi Cheka kwa kiwango cha lami.


Bashungwa amezungumza hayo Aprili 29, 2024 Wilayani Kigamboni Mkoani Dar es Salaam katika ziara yake ya kikazi ya kukagua athari za miundombinu ya barabara na madaraja zilizotokana na mvua za El-Nino na kujionea hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Wakala wa Barabara (TANROADS).


“Nilivyokuja Kigamboni kukagua barabara hii ya Kibada - Mwasonga - Kimbiji tulikuwa hatujasaini mkataba, nitumia nafasi hii kuwataarifu kuwa tayari tumesaini mkataba na sasa Mkandarasi anaendelea kuleta mitambo eneo la kazi ili mvua itakapokatika aweze kuanza kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami na haitakuwa kilometa 41 tena bali 51 kwani tunaiunganisha na kipande kilichobakia cha Cheka hadi Kimbiji”, amesema Bashungwa.


Bashungwa amewahakikishia wananchi kuwa Serikali iko kazini na imejipanga kikamilifu kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, TANROADS na TARURA kurekebisha maeneo yote yaliyopata athari ili ziendelee kupitika na kutokwamisha shughuli za wananchi na viwanda katika uzalishaji.


Halikadhalika, Bashungwa amemuelekeza Mkandarasi Estim kuendelea kuleta vifaa na mitambo yote katika eneo la mradi wa barabara ya Kibada - Mwasonga - Kimbiji wakati akisubiria malipo ya awali na kiangazi kianze ili ujenzi uweze kuanza mara moja.


Naye, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ameeleza kuwa Mkoa wa Dar es Salaam hauna mafuriko ila wananchi wameziba njia za maji kwa kujenga nyumba kwenye mikondo ya maji na kusistiza kuwa Mkoa huo unahitaji kufumuliwa upya kwa na kujenga mifereji imara ya maji ya mvua ili kuzuia maji kutoingia kwenye makazi ya wananchi.


Kwa upande wake, Mbunge wa Kigamboni, Dkt. Faustine Ndugulile ameeleza kuwa barabara ya Kibada - Mwasonga hadi Cheka ni barabara muhimu sana kwa wananchi wa Kigamboni kwani inapitisha magari zaidi ya elfu moja ya ujazo mbalimbali makubwa na madogo na pia ni barabara inayoelekea kwenye viwanda vikubwa zaidi ya 10 na kuna eneo kubwa la uwekezaji hivyo ujenzi wa barabara hiyo utaleta tija na chachu ya kimaendeleo kwa wanakigamboni.

Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Eng. John Mkumbo ameeleza kuwa ujenzi wa barabara ya Kibada - Mwasonga - Kimbiji (km 41) utatekelezwa na Mkandarasi wa Kampuni ya Estim na tayari ameshakabidhiwa eneo la ujenzi tangu Aprili 10, 2024.

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa akisisitiza jambo kwa wananchi wa Kibada, Wilayani Kigamboni Mkoani Dar es Salaam akiwa katika ziara yake ya kikazi ya kukagua athari za miundombinu ya barabara na madaraja zilizotokana na mvua za El-Nino katika barabara ya Kibada - Mwasonga - Kimbiji (km 41).

Meneja wa Wakala ya Barabara (TANROADS), Mkoa wa Dar es salaam, Mhandisi John Mkumbo akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, pamoja na viongozi wengine wakati wakikagua miundombinu ya barabara na madaraja katika barabara ya Kibada - Mwasonga - Kimbiji iliyoathiriwa na mvua za El Nino, Mkoani Dar es Salaam.

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa akikagua barabara ya Kibada - Mwasonga - Kimbiji (km 41) ambayo imeathiriwa na mvua zilizonyesha za El Nino Wilayani Kigamboni Mkoani Dar es Salaam.

Meneja wa Wakala ya Barabara (TANROADS), Mkoa wa Dar es salaam, Mhandisi John Mkumbo akizungumza na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, wakati wakikagua miundombinu ya barabara ya Kibada – Mwasonga – Kimbiji (km 41), iliyoathiriwa na mvua Mkoani Dar es Salaam.

Muonekano wa juu wa sehemu ya barabara ya Kibada – Mwasonga – Kimbiji (km 41) ambayo Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameikagua Wilayani Kigamboni katika ziara yake ya kikazi ya kukagua miundombinu ya barabara na madaraja iliyoathiriwa na mvua Mkoani Dar es Salaam. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...