* Uchumi waimarika, mfumuko wa bei wapungua, Akiba fedha za kigeni ipo ya kutosha....

Na Leandra Gabriel, Michuzi Tv


KAMATI Ya Sera na Fedha MPC imepandisha riba ya Benki Kuu (Central Bank Rate -CBR,) kutoka asilimia 5.5 iliyotumika katika robo ya kwanza ya mwaka 2024 hadi asilimia 6 ambayo itatumika katika robo ya pili ya mwaka 2024 kwa kipindi cha mwezi Aprili hadi Juni 2024 na hiyo ni pamoja na MPC kuridhishwa na ukuaji wa uchumi wa Tanzania ambao umeendelea kuimarika licha ya kuwepo kwa changamoto za mtikisiko wa uchumi wa dunia.

Akitoa taarifa ya kamati ya Sera na Fedha (MPC,) kwa waandishi wa habari Pamoja na taasisi mbalimbali za Fedha nchini leo jijini Dar es Salaam; Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT,) Emmanuel Tutuba amesema kuwa, kamati hiyo imepandisha riba ya Benki Kuu (Central Bank Rate -CBR,) kutoka asilimia 5.5 iliyotumika robo ya kwanza mwaka 2024 hadi asilimia 6 ambayo itatumika katika robo ya pili ya mwaka 2024.

Tutuba amesema kufuatia kikao cha kamati kilichofanyika Aprili 3 mwaka huu na kufikia uamuzi huo kulizingatia tathmini ya mwelekeo wa uchumi uliofanyika mwezi Machi hivyo kamati imeona umuhimu wa kuongeza riba ya Benki Kuu hadi kufikia asilimia 6 ambayo itakuwa na wigo wa asilimia 2 juu na chini ili kukabiliana na ongezeko la mfumuko wa bei katika siku za zijazo kutokana na athari za mwenendo wa uchumi wa dunia.

Kuhusiana na mwenendo wa uchumi Tutuba amesema, uchumi unakadiriwa kuongezeka kwa asilimia 5.1 kwa mwaka 2023 kutoka asilimia 4.7 mwaka 2022 huku uchumi ukikadiriwa kufikia 5.1 katika robo ya kwanza ya mwaka 2024.

" Mwenendo huu unatokana na uwekezaji unaofanywa na Serikali hususani katika ujenzi wa miundombinu unaolenga kuongeza uwekezaji kwa sekta binafsi ambazo zimeendelea kuchangia katika kuimarika kwa uchumi kutokana na maboresho yanayoendelea katika kuimarisha mazingira ya biashara uwekezaji nchini na hii inadhihirika kutokana na kuendelea kuongezeka kwa mikopo kwa sekta binafsi na uwekezaji kutoka nje ya Nchi." Ameeleza.

Pia amesema, Akiba ya fedha za kigeni imeendelea kuwa ya kutosha ambapo imefikia dola za Marekani Bilioni 5.3 mwishoni mwa mwezi Machi 2024 ambazo zinatosheleza kuagiza bidhaa na huduma nje ya Nchi kwa miezi 4.4.

Aidha ameeleza, Mwenendo wa uchumi Zanzibar umeendelea kuwa wa kuridhisha ambapo umekua kwa zaidi ya asilimia 6 kwa mwaka 2023 kutokana na kuimarika kwa shughuli za uchumi hususani utalii huku ukuaji huo ukitarajiwa kuongezeka kwa kipindi kijacho cha mwaka 2024 kutokana na maboresho ya mazingira ya uwekezaji na biashara.

Kuhusiana na mfumuko wa bei, Tutuba amesema kwa sasa mfumuko wa bei ni tulivu kwa wastani wa asilimia 3.0 kwa robo ya kwanza mwaka 2024 kiwango ambacho kilikuwa ndani ya lengo la Nchi la mfumuko wa bei usiozidi asilimia 5 na vigezo vya kikanda kwa jumuiya ambazo Tanzania ni mwanachama.

Kwa upande wake Mwenyekiti Umoja wa Mabenki Tanzania Theobald Sabi amesema jumuiya hiyo ina wajibu wa kutekeleza maamuzi hayo na mabenki yote yameendelea kutekeleza agizo hilo kwa wateja kwa wanaowahudumia.

Aidha amesema Umoja huo unafarijika na namna uchumi wa Nchi unavyoendelea kuimarika, mfumuko wa bei kubaki stahimilivu huku mabenki yakiendelea kutoa mikopo kwa wananchi na uchumi kuzidi kukua.


Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT,) Emmanuel Tutuba akitoa taarifa ya kamati ya MPC kwa waandishi wa habari na Taasisi mbalimbali za Fedha nchini na kueleza kuwa riba hiyo itatumika katika robo ya pili ya mwaka 2024 yaani kuanzia Aprili hadi Juni 2024. Leo jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Umoja wa Mabenki Tanzania Theobald Sabi akizungumza wakati wa mkutano huo na kueleza kuwa umoja huo unafarijika na namna uchumi wa Nchi unavyoendelea kuimarika, mfumuko wa bei kubaki stahimilivu huku mabenki yakiendelea kutoa mikopo kwa wananchi. Leo jijini Dar es Salaam.
Matukio mbalimbali wakati wa mkutano huo.

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT,) Emmanuel Tutuba akitoa taarifa ya kamati ya MPC kwa waandishi wa habari na Taasisi mbalimbali za Fedha nchini na kueleza kuwa riba hiyo itatumika katika robo ya pili ya mwaka 2024 yaani kuanzia Aprili hadi Juni 2024. Leo jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Umoja wa Mabenki Tanzania Theobald Sabi akizungumza wakati wa mkutano huo na kueleza kuwa umoja huo unafarijika na namna uchumi wa Nchi unavyoendelea kuimarika, mfumuko wa bei kubaki stahimilivu huku mabenki yakiendelea kutoa mikopo kwa wananchi. Leo jijini Dar es Salaam.

Matukio mbalimbali wakati wa mkutano huo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...