Na Faki Mjaka-AMMZ
Afisi ya Mwanasheria Mkuu Zanzibar na Chuo Kikuu cha Taifa cha Sheria, Jodhpur cha India (NLUJ) zimesaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) kwa lengo la kujengeana uwezo katika tasnia ya sheria.
Makubaliano hayo yamesaniwa na Naibu Mwanasheria Mkuu Zanzibar, Ndugu Shaaban Ramadhan Abdalla na Makamu Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Sheria, Jodhpur cha India (NLUJ) Profesa Dk. Harpreet Kaur katika Ukumbi wa Chuo hicho kilichopo Jimbo la Jodhpur nchini India.
Akizungumza mara baada ya kusaini Hati hiyo, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar amesema kuwa Makubaliano hayo ni matokeo ya ziara yao ya Mafunzo ya wiki mbili nchini India yaliyofadhiliwa na Serikali ya India (Wizara ya Mambo ya Nje) kupitia Programu yao ya Mpango wa Ushirikiano wa Kiufundi na Kiuchumi wa India (ITEC)
Amesema Makubaliano hayo yatatoa fursa kwa Watendaji wa Afisi yake kuongeza maarifa na utaalamu katika maeneo mbali mbali ya fani zao kwa faida ya Serikali na wananchi kwa ujumla.
Amesema Chuo cha NLUJ ni chuo kilicholeta mapinduzi makubwa katika nyanja ya ufundishaji nchini India, hivyo ni wazi kuwa watendaji wataongeza ujuzi wao kutokana na kuweza kupata uzoefu mkubwa wa wataalam wa sheria wa Chuo hicho.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo cha NLUJ Profesa Dk. Harpreet Kaur, alisema kuwa, Makubaliano hayo sio tu yatakuza juhudi za kitaaluma kati ya Zanzibar na India, bali pia yatakuza urafiki na kubadilishana utamaduni wa nchi hizo.
Amefafanua kuwa, makubaliano hayo pia yatazingatia namna na mbinu bora zaidi za kupeana maarifa pamoja na kuweza kufanya tafiti mbali mbali za kitaaluma kwa maslahi ya sekta ya sheria na maendeleo kwa ujumla wake.
Aidha, Kupitia makubaliano hayo, fursa na utekelezaji wa programu za mafunzo ya kujengeana uwezo zitaendeshwa kwa mashirikiano ya pamoja ambazo zitakuwa zikifanywa kwa nadharia na vitendo yatakayoongozwa zaidi na matumizi ya teknolojia ya kisasa.
Prof. Dk. Harpreet ameongeza kuwa, Makubaliano hayo pia yatatoa fursa mbali mbali kwa Vitivo katika Chuo hicho, Wanafunzi, Mawakili wa Serikali, Maafisa sheria na Watafiti mbali mbali kutoka katika taasisi hizo mbili kuweza kufanya tafiti kuhusiana na mada mbalimbali zitakazoibuliwa kuhusiana na Sheria kama vile Usuluhishi na Njia mbadala za utatuzi wa migogoro, Uandishi wa sheria , Mikataba, Biashara, utumiaji wa Akili bandia( artificial Intelligence) katika uandaaji wa hati za Madai na uendeshaji wa Mashauri, pamoja na kuzingatia masuala mengine yanayohusiana na utawala na uendeshaji wa taasisi.
Mwenyekiti wa Kamati ya mambo ya Nje ya Chuo cha NLUJ Dk. Neeti Mathur, alisema kuwa ana matumaini makubwa kuwa kila upande utanufaika vyema na Makubaliano hayo yanayohusu taaluma na kujengeana uwezo katika mambo mbali mbali yenye mustakabali mzuri unaolenga ustawi wa tasisi zote mbili na maslahi mapana kitaifa.
Aidha Mkurugenzi Rasilimali Watu, Utawala na Mipango, Ndugu Fatma Iddi Ally amemshukuru Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Dkt Mwinyi Talib Haji kwa kufanya jitihada binafsi za kuomba na hatimaye kufanikisha kupatikana kwa mafunzo hayo kwa watendaji wa Afisi yake pamoja na Wanasheria wengine kutoka Wizara na Taasisi mbali mbali za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo yameweza kuleta tija na faida kubwa kwa taifa na pia kukuza upeo na ufahamu wao katika namna bora ya usimamizi wa Mikataba na kuweza kujifunza mbinu bora za kufanya mapatano.
Vile vile amebainisha kuwa ziara hiyo iliyoongozwa na Naibu Mwanasheria Mkuu Zanzibar Ndugu Shaaban Ramadhan Abdalla, ilijumuisha Watendaji 30 kutoka Afisi ya Mwanasheria Mkuu Zanzibar pamoja na Wanasheria 10 kutoka Wizara na Tasisi mbali mbali za Serikali zikiwemo Ofisi ya Rais Katiba Sheria Utumishi na Utawala Bora, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Ofisi ya Rais Kazi Uchumi na Uwekezaji, Shirika la Taifa la Biashara (ZSTC) na Wizara ya Maji Nishati na Madini ambapo mada zisizopungua kumi na saba (17) zinazohusiana na Usimamizi wa Mikataba pamoja na mbinu za kufanya mapatano zilifundishwa
Miongoni mwa mada hizo ni Utayarishaji wa Mkataba pamoja na changamoto zilizopo katika uandaaji na usimamizi wa mikataba ikiwemo umakini wa uandishi wake , haki katika haki miliki, biashara za kimataifa katika uuzaji wa bidhaa, dhima ya kodi katika mikataba ya kibiashara pamoja na mikataba ya bima.
Aidha Mkurugenzi Fatma aliahidi kuwa watayatumia vyema mafunzo waliyopatiwa, na kuhakikisha kuwa dhamira iliyokusudiwa inafikiwa kwa kuyatumia mafunzo hayo kwa ufanisi zaidi katika utendaji wa majukumu yao kwa faida ya Serikali na Taifa kwa ujumla.
Naibu Mwanasheria Mkuu Zanzibar, Ndugu Shaaban Ramadhan Abdalla na Makamu Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Sheria, Jodhpur cha India (NLUJ) Profesa Dk. Harpreet Kaur wakionesha Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) mara baada ya kusaini Hati hizo katika Ukumbi wa Chuo hicho kilichopo Jimbo la Jodhpur nchini India.
Picha ya pamoja baina ya washiriki wa Mafunzo ya wiki mbili nchini India yaliyofadhiliwa na Serikali ya India (Wizara ya Mambo ya Nje) kupitia Programu yao ya Mpango wa Ushirikiano wa Kiufundi na Kiuchumi wa India (ITEC) wakiwa pamoja na uongozi wa Chuo cha Taifa cha Sheria, Jodhpur cha India (NLUJ)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...