Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MKAZI wa kijiji cha Okutu wilayani Simanjiro mkoani Manyara, Melkzedek Moikani (33) amehukumiwa kwenda jela kifungo cha miezi sita kwa kosa la kufanya fujo kwa kufunga ofisi ya kijiji kwa kutumia kufuli hivyo kuzua hofu na kukwamisha shughuli za maendeleo.
Melkzedek ambaye ni mshtakiwa namba mbili na wenzake watatu walishtakiwa kwenye mahakama hiyo kwa kutenda kosa hilo Januari 28 mwaka 2024 saa 9 alasiri.
Ofisa mtendaji wa kijiji cha Okutu, Neema Gelpeter ndiye alikuwa mlalamikaji kwenye kesi hiyo ya jinai namba 19/2024 ya I'llkufanya fujo na kufunga ofisi ya kijiji kwa washtakiwa hao.
Hakimu wa mahakama ya mwanzo Engasmet, Lucia Evarest Mushi amemuhukumu mshtakiwa namba mbili Melkzedek kifungo cha miezi sita bila faini na kuwaachia washtakiwa wengine watatu baada ya kudhibitisha kuwa hawana hatia.
Washtakiwa wengine kwenye kesi hiyo walikuwa ni mshtakiwa namba moja Said Mdachi (65), mshtakiwa namba tatu, Tumburu Jembe (40) na mshtakiwa namba nne Seuri Moikani (43).
Hakimu Mushi amesema washtakiwa hao walishtaka kwa kosa la kufanya fujo kwa kufunga ofisi ya kijiji kinyume na kifungu cha sheria namba 89/12 ya kanuni ya adhabu sura ya 16.
Amesema washtakiwa hao walifanya fujo kwa kufunga ofisi ya Mwenyekiti wa kijiji hicho kwa kutumia kufuli aina ya Solex yenye rangi ya fedha.
Pia, washtakiwa hao walifunga ofisi ya ofisa mtendaji wa kijiji cha Okutu kwa kufunga mlango kwa kutumia kufuli yenye rangi ya shaba hivyo kusababisha hofu kwa viongozi hao na kukwama kufanya shughuli za kijiji.
"Kulingana na ushahidi uliotolewa mahakamani hapa upande wa mashtaka umedhibitisha bila kutia shaka kuwa mshtakiwa namba mbili Melkzedek amekutwa na hatia hivyo anahukumiwa kwenda jela kifungo cha miezi sita bila faini," amesema.
Hata hivyo, mshtakiwa namba moja, namba tatu na namba nne, upande wa mashtaka umeshindwa kudhibitisha mashtaka yao hivyo mahakama hiyo ikawaachia huru.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...