Dar es Salaam. Tarehe 23 Mei 2024: Katika kuongeza ujumuishi wa wananchi kiuchumi hasa makundi maalumu, Taasisi ya CRDB Bank Foundation imesaini mkataba wa makubaliano kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) kuwawezesha kiuchumi vijana kuanzia miaka 18 hadi 24, waliopo shule na wale ambao wameacha shule kwasababu moja au nyengine.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye hafla ya kutia saini mkataba huo wenye thamani ya dola 300,000 za Marekani, sawa na shilingi milioni 800, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Mwambapa amesema ushirikiano huo unatokana na kufanana kwa malengo na mipango ya pande zote mbili katika kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za uchumi.
“Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2023, Taasisi yetu ya CRDB Bank Foundation tumeelekeza nguvu kubwa katika kuanzisha programu za kuwawezesha vijana na wanawake kujumuishwa kwenye mfumo rasmi wa huduma za fedha, kuwapa mafunzo na mitaji wezeshi kupitia Programu yetu ya Imbeju.
Ushirikiano huu na UNFPA unakwenda kuimarisha jitihada hizi na kuwezesha kufikia vijana wengi zaidi,” amesema Tully.
Kama ilivyo kwa CRDB Bank Foundation, UNFPA inatekeleza programu tofauti za kuwainua wananchi kiuchumi, kuwajengea uwezo wa kuzitambua haki zao, kupunguza migogoro ya kifamilia na kijinsia, pamoja na kutoa elimu ya uzazi kwa wanawake, mabinti na vijana azma ikiwa ni kujenga vijana wenye uwezo wa kiuchumi kuzikabili changamoto za kila siku.
Tully amesema ushirikiano huu unawalenga vijana walio masomoni na wale walioshindwa kuendelea na masomo kwasababu mbalimbali, walemavu pamoja na mabinti waliopata ujauzito wakiwa masomoni. Katika utekelezaji wake, amesema wanakusudia kupunguza changamoto za upatikanaji wa ajira, kuwapa elimu ya fedha, kuwapa elimu ya afya ili kupunguza mimba za utotoni, kupunguza ukatili wa kijinsia na maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi (VVU), katika mikoa mitatu ya Dar es Salaam, Dodoma na Kigoma.
“Ushirikiano wetu na UNFPA utajikita kwenye maeneo mawili ya msingi. Kwanza ni kutoa elimu na maarifa ya kujitambua kwa vijana walio shule na walioa nje ya shule itakayojumuisha mafunzo juu ya huduma rafiki za afya, unyanyasaji wa kijinsia, na jinsi ya kuepuka na namna ya kuishi na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi. Eneo la pili ni kutoa elimu ya fedha na ujasiriamali kwa vijana na mabinti ili kuwajengea mazingira ya kutekeleza majukumu yao kikamilifu,” amefafanua Tully.
Kwa upande wake, Mark Bryan Schreiner, Mwakilishi Mkazi wa UNFPA nchini amesema shirika hilo limekuwa likitekeleza miradi tofauti inayolenga kuwainua wananchi hasa wa makundi yaliyosahaulika katika jamii ili kuwa na uchumi jumuishi na wanufaika wakubwa wa programu zake ni wanawake, vijana wakiwamo mabinti wenye rika la balehe, na wahamiaji wanaoomba hifadhi kutokana na migogoro ya kisiasa na kijamii inayotokea kwenye mataifa jirani.
“Tukiangalia changamoto zinazowakabili vijana nchini ikiwamo upatikanaji wa mitaji, ukosefu wa ajira na elimu ya ujasiriamali, UNFPA inayo kila sababu ya kushirikiana na wabia wa kimkakati kusaidia kuwawezesha vijana nchini kushiriki kujenga uchumi wa taifa lao,” amesema Schreiner.
Kwa sasa, Schreiner amesema UNFPA inatekeleza programu yake ya tisa nchini inayohamasisha uzazi salama kwa kuitambua na kuikubali kila mimba inayopatikana, pamoja na kumwezesha kila kijana kutimiza ndoto za maisha yake. “Lengo letu ni kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma hivyo tunashirikiana na wadau wenye mtizamo kama wetu kama ilivyo Taasisi ya CRDB Bank Foundation,” amesema Schreiner.
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, zaidi ya nusu ya Watanzania ni vijana wenye umri chini ya miaka 24. Matokeo ya sensa hiyo yanaonyesha asilimia 44 ya watu wote ni watoto wenye chini ya umri wa miaka 15 huku asilimia 19 wakiwa vijana wenye umri kati ya miaka 15 mpaka 24. Hii ni idadi kubwa ya wananchi watakaoguswa na mradi huu wa kwanza wa ushirikiano kati ya CRDB Bank Foundation na UNFPA.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...