Na Mwandishi Maalum Ruvuma

WAKALA wa barabara Tanzania(TANROADS)Mkoa wa Ruvuma,imekamilisha kazi ya kuimarisha daraja la mto Muhuwesi wilayani Tunduru ambalo liliathirika na mvua za masika na kusababisha taaruki kwa watumiaji wa daraja hilo.

Meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma Saleh Juma alisema,kwa sasa daraja hilo ni salama na haliwezi kusogea tena kama ilivyotokea hapo awali, na amewatoa hofu watumiaji hasa wenye magari kuhusu uimara wa daraja hilo linalounganisha mikoa ya Ruvuma,Lindi na Mtwara.

Aidha alitaja kazi nyingine zilizofanyika,ni kuziba mashimo makubwa kwenye barabara inayoingia katika daraja hilo yaliyosababishwa na maji ya mvua kupita chini ya barabara na kukatika kwa sehemu ya lami.

Alisema, katika eneo hilo barabara imemeza maji na kusababisha ifumuke,lakini tayari TANROADS kwa kumtumia Mkandarasi Kampuni ya Ovans Constructions Ltd imefanikiwa kuziba mashimo yaliyojitokeza.

“katika eneo hili magari yanayopita yalikuwa yanakwama na kusababisha adha kubwa,lakini tayari serikali kupitia wakala wa barabara Tanzania(TANROADS)imefanya matengengezo ya haraka na sasa hali ni shwari”alisema.

Kwa upande wake Mhandisi wa kampuni ya Ovans Constructions Ltd Azimio Mwapongo alisema, katika eneo hilo kulitokea changamoto ya maji kutokea chini kuja juu ya barabara na kusababisha lami kukatika.

Kwa mujibu wa Mwapongo,kazi zilizofanyika ni ulazaji wa mabomba chini ya ardhi kwa ajili ya kunyonya maji kutoka chini na kuyapeleka nje ili yasikae tena pamoja na kurudishia tabaka la lami.

Alisema,kwa sasa daraja na sehemu ya barabara hiyo usalama wake ni mkubwa na kazi iliyoendelea ni ujenzi wa mifereji ya kupitisha maji ambayo nayo iliathiri na mvua.

Mkazi wa kijiji cha Muhuwesi wilayani Tunduru Salum Gambagamba,ameipongeza serikali kupitia TANRAODS kwa kufanya matengenezo ya haraka katika daraja la mto huo na maeneo ya barabara yaliyoanza kuharibika na mvua.
Mhandisi wa kampuni ya Ovans Construtions Ltd Azimio Mwapongo kulia,akitoa taarifa ya ukarabati wa miundombinu ya daraja la mto Muhuwesi linalounganisha mkoa wa Ruvuma na mikoa ya kusini Lindi na Mtwara kwa Meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Saleh Juma aliyetembea daraja hilo ili kujionea kazi ya kurejesha baadhi ya miundombinu yake,kushoto msimamizi wa kitengo cha matengenezo TANROADS Godfery Robbi.
Meneja wa TANROADS Mkoani Ruvuma Mhandisi Saleh Juma kushoto,akitoa maelekezo kwa mhandisi wa Kampuni y Ovans Construtions Ltd Azimio Mwapongo wa pili kulia baada ya kukagua matengenezo ya kipande cha Barabara ya Songea-Mangaka eneo la Muhuwesi wilayani Tunduru kilichoharibiwa na mvua za masika,wa pili kushoto msimamizi wa kitengo cha matengenezo Tanroads Godfre Robbi na kulia mkuu wa kitengo cha mipango Tanroads Rubara Marando.

Meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Saleh Juma,akiangalia sehemu ya mifereji ya kupitisha maji katika barabara ya Songea-Mangaka eneo la daraja la Mto Muhuwesi wilayani Tunduru ambayo imeharibika vibaya kutokana na mvua za masika akiwa katika ziara ya kukagua miundombinu ya barabara hiyo jana.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...