NA BALTAZAR MASHAKA,MAGU

TAASISI ya The Desk & Chair Foundation,imekamilisha na kukabidhi mradi mkubwa wa kisima cha maji katika Kijiji cha Kitongosima wilayani Magu,utakaohudumia zaidi ya wananchi 2,000 wa kijiji hicho na wanafunzi 840 wa Shule ya Msingi Simakitongo.

Pia mradi huo uliogharimu sh.milioni 20,utawanufaisha watumishi na watoto 75 wenye migongo wazi na vichwa vikubwa wanaolelewa katika Kituo cha Nyumba ya Matumaini cha Child Help Tanzania ikiwemo mifugo (ng’ombe, mbuzi na kondoo).

Akikabidhi mradi huo wa kisima cha maji leo,Mwenyekiti wa The Desk & Chair Foundation,Dk.Alhaji Sibtain Meghjee,amesema kimegharimu sh.milioni 20 na kitaondoa adha ya muda mrefu ya kusaka maji waliyokuwa wakiipata wananchi wa Kijiji cha Kitongosima na kuwanufaisha ikiwemo mifugo.

“Mradi una uwezo wa kuzalisha lita 10,000 za maji na mfumo wa mtandao wa maji tunaokabidhi ni pamoja na mitambo ya Solar (umemejua),manteki mawili ya maji,nguzo mbili za matenki na sehemu ya kunyweshea mifugo, mbali na wananchi zaidi ya 2,000 wa Kitongosima pia,wanafunzi 840 wa Shule ya Msingi Simakitongo na kituo jirani cha cha kulelea watoto wenye mgongo wazi na vichwa vikubwa watanufaika,”amesema.

Dk.Alhaji Meghjee amesema mradi huo umeonesha ufanisi mkubwa kwa wananchi kipekee pia, walifikiria mifugo yao na hivyo wameijengea sehemu safi ya kunywa maji kwa mwaka mzima na kuwataka wananchi hao kutunza miundomboni hiyo iwahudumie kwa muda mrefu.

Amewashukuru wafadhili wa mradi huo wa maji,serikali ya awamu ya sita,uongozi wa kijiji na wananchi kwa ushirikiano uliowezesha kuukamilika kwa ubora kulingana na thamani ya fedha iliyotumika.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwa niaba ya akinamama wa Kitongosima,Nyangeta Magoti na Scolastica Magubu,wamesema mradi uko vizuri sasa wameondokana na adha ya kuzunguka usiku na mchana kutafuta huduma ya maji.

"Eneo hili lilikuwa na shida kubwa ya maji na wananchi waliteseka kusaka huduma hii wakiamka usiku,njiani walikutana na wanyama hasa fisi lakini The Desk & Chair Foundation,kuwekeza fedha zao kutekeleza mradi huu mkubwa,wamewatutua akina mama ndoo kichwani,tunawashukuru sana,”amesema Nyangeta.
Scolastica amesema walikuwa wakitoka saa 9 usiku kutafuta maji na kurudi asubuhi saa 4,walitumia muda mwingi kupata huduma ya maji hali iliyosababisha migogoro na kuhatarisha ndoa zao, hivyo mradi huo utaimarisha familia kwani wamefikishiwa huduma karibu na watapata fursa ya kufanya shughuli za maendeleo na kujikwamua kiuchumi.

"Mradi huu wa maji ni mkombozi mkubwa kwetu wananchi hasa kina mama,tulikuwa tukitembea zaidi ya kilometa tano kutafuta maji,wakati mwingine tulitoka usiku na kurudi asubuhi,jambo hilo lilihatarisha ndoa zetu na hata maisha,"amesema.

Kwa upande wake mwanafunzi wa Shule ya Msingi Simakitongo,Rosemary Avit,amesema ukosefu wa maji shuleni uliwakwamisha baadhi yao kuhudhuria masomo wakipeana zamu ya kuteka maji,tatizo lililowarudisha nyuma kielimu.

Amesema shule hiyo haikuwa na huduma ya majisafi na salama licha ya serikali kuboresha miundombinu ya elimu kwa kuleta vitabu,madawati na kupanda miti ya matunda na vivuli kutunza mazingira,wanashukuru kupata maji ya bomba,changamoto iliyobaki ni uhaba wa vyumba 10 vya madarasa,nyumba nne za walimu,vyoo matundu 14 na madawati 200.

Mtendaji wa Kijiji cha Kitongosima,Majige Masalamali ameishukuru The Desk & Chair Foundation na wadau wa maendeleo kuunga mkono dhamira ya serikali ya kumtua mama ndoo kichwani.

Sheikh wa Bilal Muslim Kanda ya Ziwa,Sheikh Hashim Ramadhan amewashukuru wafadhili wa mradi huo akisema wameingiza furaha kwa jamii kwa zawadi ya maji pia, Mtume Muhammad S.A.W na Mwenyezi Mungu.
Pia watabasamu,wampende Mungu,waishi kwa upendo na jamii,wawasaidie yatima,watoto wenye vichwa vikubwa na migongo wazi,furaha hiyo isiishie hapo wawaombee dua waliotangulia mbele za haki.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...