Na Mwandishi Wetu 

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)  imesema uwepo wa mgandamizo mdogo wa hewa katika Bahari ya Hindi mashariki mwa pwani ya Mtwara kunatarajiwa kusababisha uwepo wa vipindi vikubwa vya mvua katika  baadhi ya maeneo ya mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani, Morogoro, Dar es Salaam na maeneo ya jirani.

Katika taarifa iliyotolewa  na Mamlaka hiyo, leo Mei Mosi, 2024 inasema, mifumo ya hali ya hewa iliyopo kwa sasa inaonesha kuwa mgandamizo huo mdogo wa hewa unatarajiwa kuimarika na kufikia hadhi ya Kimbunga kamili hadi kufikia kesho, Mei 2 2024.

"Wakati mgandamizo huo mdogo wa hewa ukiendelea kuimarika, unatarajiwa pia kusogea kuelekea baadhi ya maeneo ya pwani ya nchi yetu kuanzia usiku wa kuamkia siku ya Ijumaa, Mei 3, 2024 na kwamba Mgandamizo huo mdogo wa hewa unatarajiwa kuendelea kuwepo katika maeneo ya ukanda wa pwani ya nchi  hadi  Mei 6, 2024". Imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Imeendelea kuelezwa kuwa, Hata hivyo, mgandamizo huo mdogo wa hewa unatarajiwa kupungua nguvu baada ya Mei 6 2024.

Taarifa hiyo imesema, uwepo wa mgandamizo huo mdogo wa hewa unatarajiwa kutawala na kuathiri mifumo ya hali ya hewa hapa nchini ikiwa ni pamoja na kusababisha vipindi vya mvua kubwa na upepo mkali katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani, Morogoro, Dar es Salaam na maeneo ya jirani. 

Hata hivyo, Wananchi wanashauriwa kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kujikinga na athari zinazoweza kujitokeza.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kufuatilia mwenendo wa mgandamizo huo mdogo wa hewa na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na itaendelea kutoa taarifa mara kwa mara kila inapobidi.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...