Na Janeth Raphael MichuziTv - Morogoro

Imeelezwa Kuwa ili kuweza kufikia utekelezaji mzuri wa bajeti ya Serikali wadau katika sekta ya habari wametakiwa kuendelea kushirikiana pamoja na Serikali kutoa elimu kwa wananchi ili wasikwepe kulipa kodi kwani 70% ya mapato ya nchi yanatokana na kodi za ndani huku 30% yakitokana na misaada na mikopo nafuu na mikopo ya kibiashara ya ndani na nje.

Mchumi Mkuu, kutoka Wizara ya Fedha Salome Kingdom ameyasema hayo Mkoani Morogoro wakati akitoa mada juu ya uwasilishaji wa bajeti ya Serikali kwa lugha rahisi kwenye kongamano la kutoa Elimu kwa wamiliki wa mitandao ya kijamii nchini.

“Ushiriki wa wananchi katika kulipa kodi na michango mingine ya serikali ni muhimu kwa sababu inasaidia kuimarisha mapato ya serikali, ambayo ni msingi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo,”amesema.

Aidha, amebainisha kuwa serikali inategemea mapato yanayokusanywa kutoka kwa wananchi ili kuweza kugharamia miradi muhimu kama vile ujenzi wa miundombinu, huduma za afya, elimu, na maji safi na salama.

"Wananchi wanapaswa kuelewa kuwa kulipa kodi siyo tu wajibu wa kisheria, bali ni mchango wao wa moja kwa moja katika kuleta maendeleo ya taifa. Bila mapato ya kutosha, serikali itashindwa kutekeleza miradi mingi muhimu ambayo inalenga kuboresha maisha ya kila Mtanzania,”ameongeza.

Sambamba na hayo Bi. Salome amesema uwazi na uwajibikaji wa serikali katika matumizi ya mapato ya kodi utasaidia kuimarisha imani ya wananchi na hivyo kuongeza hamasa yao ya kulipa kodi.

Amesema, "Mitandao ya kijamii ina ushawishi mkubwa katika jamii yetu ya sasa hivyo ni muhimu kutumia ushawishi huo kwa njia chanya kwa kuelimisha na kuhamasisha wananchi kuhusu masuala ya msingi kama haya."





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...