Absa Bank Tanzania imeendelea kuthibitisha kuwa mstari wa mbele katika uvumbuzi wa bidhaa na huduma kwa kuzindua Huduma ya Mikopo ya Magari (VAF) kwa lengo la kufanya umiliki wa magari kuwa rahisi na nafuu zaidi kwa wateja wake.

Huduma ya Mikopo ya Magari ya Absa (VAF) ni suluhisho la kifedha la muda wa kati lililobuniwa kusaidia wateja wa benki kununua magari mapya na yaliyotumika kutoka kwa wauzaji wa ndani bila hitaji la kuwa na fedha zote za malipo mkononi. Suluhisho hili linaakisi mkakati wa benki wa kutoa suluhisho za kifedha zinazowiana na maisha na matarajio ya wateja wake.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Absa VAF, Mkuu wa Wateja Binafsi wa Benki ya Absa Bank Tanzania, Bi Ndabu Swere, alisema, “Tunafurahia sana kuzindua huduma ya Mikopo ya Magari. Hii ni ishara ya kujitolea kwetu kusikiliza wateja wetu na kutatua changamoto na mahitaji yao. Tunaelewa kwamba kununua gari si rahisi kwa sababu magari si rahisi, na kwa kuwa watu hawana fedha taslimu wakati wote, wanaweza kuhitaji msaada kutoka mahali pengine hasa wakati wauzaji wa magari wanahitaji malipo mapema. Hapa ndipo Mpango wa Mikopo ya Magari wa Absa unapoingia.

Kupitia Absa VAF, wateja wetu watafurahia ufadhili wa hadi 90% kwa magari mapya, na hadi 80% kwa magari yaliyotumika ambapo gari lililonunuliwa kwa mkopo linatumika kama dhamana. Bidhaa hii inatoa faida nyingi kwa wateja wetu, ikiwa ni pamoja na kuwawezesha wateja kupata fedha za kununua gari la chaguo lao wakati ambapo hawana fedha zote mapema. Inawaachia wateja uhuru wa kutumia fedha zao kwa uwekezaji au kwa gharama zisizotarajiwa zinazoweza kujitokeza wakati wa mwaka. Inampa mteja kupata gari lake mara tu benki inapokamilisha mchakato wa mkopo wa VAF. Inapunguza mzigo wa kifedha kwa mteja kwa kumruhusu kulipia gharama kwa awamu ndogo ndogo za kawaida na mteja anahitajika tu kutoa kiasi kidogo cha malipo ya awali.”

Kwa upande wake, Bw. Beda Biswalo, Meneja wa Masoko na Mawasiliano wa benki, alisema, “Suluhisho letu la Mikopo ya Magari sio tu nyongeza ya kimkakati ya kibiashara kwa huduma zetu, lakini pia lina uhusiano wa kina na Ahadi yetu ya Chapa inayosema, ‘Story Yako ina Thamani’. Katika Absa tunajali sana Story za wateja wetu na maendeleo wanayopata katika maisha. Tunavutiwa na safari za wateja wetu na tunataka kuwa sehemu ya maandiko yao, sehemu ya Story za kweli watakazopaswa kuhadithia kwa miaka mingi ijayo wanaposimulia safari zao za mafanikio. Tunaamini kwamba tunapowasaidia wateja wetu kupata vitu wanavyohitaji ili kuboresha ubora wa maisha yao, tunaishi lengo letu la kuiwezesha Afrika ya kesho, pamoja, hatua moja baada ya nyingine.

Katika hitimisho lake, Bi Swere aliwashukuru wateja wote wa benki na kuwataka Watanzania wote kuchukua fursa hii nzuri, akisisitiza kuwa upatikanaji wa huduma hii ni rahisi sana na haina usumbufu. Inaanza na mteja kuchagua gari analopenda kununua kutoka kwa moja ya wauzaji wetu wa magari walioteuliwa kwa makini, kisha kuomba huduma ya VAF kupitia maafisa wetu wa mikopo, tunapopitia ombi la mteja, kama mteja amekidhi vigezo ataombwa kufanya malipo ya awali katika akaunti ya Absa, Absa italipa malipo kamili (malipo ya awali + salio lililobaki) kwa muuzaji wa gari, mteja atapewa gari lake kufurahia safari yake mpya.

“Mchakato wetu wa maombi ni wa haraka, rahisi, na wa gharama nafuu, unampa mteja utulivu wa akili, kwani tunasimamia kila kipengele, kuanzia kutambua wauzaji wa magari wanaoaminika hadi kuhakikisha magari yaliyokusudiwa yanakidhi viwango vya juu kupitia mpango madhubuti wa ukaguzi. Tumeingia makubaliano na wasambazaji na wauzaji wa magari wanaoaminika, ambao watakuwa wasambazaji wakuu wa magari mapya na yaliyotumika yaliyochaguliwa kwa wateja wetu. Pia tunahakikisha usimamizi wa mwanzo hadi mwisho, ikiwa ni pamoja na malipo ya kodi husika za serikali, ada za uhamisho, na bima kwa niaba ya mteja, ikimruhusu mteja kuzingatia mambo muhimu zaidi anapoendelea kuandika kurasa ya safari yake ya mafanikio.” alihitimisha.
Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa Benki ya Absa Tanzania, Bi. Ndabu Swere (katikati), akizungumza wakati wa uzinduzi wa huduma ya mikopo ya magari ya benki hiyo, jijini Dar es Salaam leo. Wengine kutoka kushoto ni, Meneja Masoko na Mawasiliano wa Absa, Bwana Beda Biswalo na Mkuu wa Kitengo cha Mikopo, Bi. Patricia Nguma.
(PICHA NA EMMANUEL MASSAKA,MICHUZI TV)

Meneja Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Absa Tanzania, Bwana Beda Biswalo (kushoto), akizungumza wakati wa uzinduzi wa huduma ya mikopo ya magari ya benki hiyo, jijini Dar es Salaam leo

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...