Na PATRICIA KIMELEMETA

KATIKA kuboresha upatikanaji wa huduma za afya nchini, Serikali ilijenga vituo vya afya kila kata ili kusaidia wananchi kupata huduma za matibabu zikiwamo huduma ya afya ya mama na watoto chini ya miaka mitano.

Hali hiyo ilisaidia kupunguza mlundikano wa wagonjwa waliokua wakipatiwa matibabu katika hospitali za Mkoa na Wilaya na kusababisha baadhi ya wagonjwa wakiwamo wajawazito kudai kulazwa wawili kwenye kitanda kimoja huku wengine wakidai kulazwa chini.

Kutokana na kuwepo kwa ongezeko la wagonjwa kwenye hospitali hizo, Serikali ilijenga vituo vya kutolea huduma za afya kila kata kwa ajili ya kutoa huduma mbalimbaliza matibabu ikiwamo huduma ya dharura ya kujifungua pamoja na huduma ya mama na mtoto.

Hali hiyo ilisaidia kuondoa malalamiko yaliyokua yakijitokeza kipindi cha nyuma ya kuwepo kwa huduma hafifu za matibabu ikiwamo ya mama na mtoto.

Irene Joshua mkazi wa Dar es Salaam amesema kuwa, mwaka 2021 alifungua salama katika kituo cha afya kilichojengwa na serikali kila kata ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya ya mama na mtoto.

Amesema mpaka sasa mtoto wake anaendelea kupatiwa matibabu katika kituo hicho kutokana na serikali kuboresha utoaji wa huduma za afya ngazi ya kata, jambo ambalo limesaidia kupunguza msongamano wa wagonjwa katika hospitali kubwa zilizokua zikitoa huduma ya afya ya mama na mtoto Mkoa wa Dar es Salaam.

" Zamani ukitaka kujifungua lazima uende hospitali za Muhimbili, Amana, Temeke na Mwananyamala, lakini sasa hivi hali ni tofauti ambapo kila kata kuna kituo cha kutoa huduma za afya ya mama na mtoto, jambo ambalo limepunguza msongamano wa wagonjwa kwenye hospitali kubwa za Mwananyamala,Temeke, Ilala na Muhimbili.

" Mwaka 2021 nlijifungua mtoto wa kike mwenye umri wa miaka mitatu na miezi sita katika kituo cha afya cha kata, mwanangu ni mzima ana afya bora na mpaka sasa anaendelea na kliniki katika kituo hicho bila ya matatizo yoyote," amesema Irene.

Ameongeza awali wakati wanaojifungua katika hospitali kubwa, kulikua na changamoto mbalimbali ikiwamo wagonjwa wawili kulala kitanda kimoja, upungufu wa vifaa tiba, na hata kauli za wauguzi zilikua kero kwa wagonjwa.

Amesema lakini sasa hivi hali ni tofauti, mama mjamzito akifika kwenye kituo cha matibabu ananyenyekewa mpaka atakapojifungua, hivyo basi wameiomba serikali kuendelea kuboresha majengo ya matibabu pamoja na vifaa tiba ili viende na wakati uliopo ambao kuna ongezeko kubwa la watu.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda amesema kuwa, huduma za afya mama na mtoto zina changamoto kubwa sio tu Tanzania bali ni Dunia mzima kutokana na baadhi ya wajawazito kufariki wakiwa kwenye uzazi na watoto kufariki mara baada ya kuzaliwa.

Amesema kuwa Serikali imejitahidi kuboresha huduma hizo ili kuhakikisha wanapunguza video vitokanavyo na uzazi ili kuwe na uzazi salama nchi mzima bila ya kuangalia mazingiira yaliyopo.

Amewaomba wadau mbalimbali kujitokeza kuchangia huduma za afya ya mama na mtoto kwenye hospitali na vituo mbalimbali vya afya ili watalaam waweze kutoa huduma bora zaidi.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk. Mohamed Mang'una amesema kuwa zaidi ya watoto 430, wanazaliwa kwa siku katika mkoa huo ambapo kati yao, watoto 100 ambao ni sawa na asilimia 22 hadi 23 wanahitaji matibabu zaidi kutokana na changamoto mbalimbali wanazozaliwa nazo.

Amesema kuwa, kutokana na hali hiyo, serikali imejitahidi kuboresha huduma za afya ikiwa ni pamoja na kujenga vituo vya kutoa huduma ngazi ya kata hadi mkoani humo ili kukabiliana na ongezeko la wagonjwa liende sambamba na uboreshaji wa huduma za matibabu.

" Mkoa wa Dar es Salaam umejenga vituo vya kutolewa huduma za afya kuanzia ngazi za kata hadi Mkoani, lengo ni kurahisisha utoaji wa huduma za afya ikiwamo huduma ya mama na mtoto ili wananchi waweze kupata huduma hizo katika maeneo yao.

" Mkoa wetu kwa siku tunaweza kuzalisha watoto 430 katika hospitali mbalimbali zilizopo mkoani kwetu na kati yao, watoto 100 ambao ni sawa na asilimia 22 hadi 23 wanahitaji huduma ya ziada ya matibabu, jambo ambalo tunalimudu kutokana na kuwepo kwa watalaamu wa afya, vifaa tiba na watumiahi kutimiza wajibu wao," amesema Dk. Mang'una.

Ameongeza kuwa, katika vituo hivyo kuna huduma za dharura za mama na mtoto pale inapotokea changamoto ni mgonjwa aweze kupatiwa matibabu ya haraka, jambo ambalo limesaidia kuboresha huduma za afya.

Ameongeza kuwa, mkakati iliyopo ni kuendelea kutoa huduma bora za afya ikiwamo ya mama na mtoto ili wanawake wanaojifungua katika maeneo hayo waweze kujifungua salama na watoto kuwa salama.

Hivi karibuni, Rais Mstaafu wa awamu ya nne,Jakaya Kikwete amesema kuwa, serikali imejitahidi kupunguza vifo vya kina mama wajawazito kutoka 556 kwa mwaka 2016 mwaka hadi kufikia 104 kwa mwaka 2022.

Amesema kuwa, kupunguza kwa vifo hivyo kunatokana na serikali kujenga vituo vya afya kila kata pamoja na kuongeza watalaam wa afya wakiwamo madaktari, wauguzi na watalaam wengine iii waweze kutoa huduma bora kwa wananachi.

Amesema kuwa, inafedhehesha kuona mama mjamzito ambaye analeta kumbe duniani anafariki kutokana na kukosa huduma bora za afya.

Aliwataka watalaam wa sekta ya afya na watalaam wengine kila mmoja kutimiza wajibu wake ili kuisaidia serikali kupungiza vifo vitokanavyo na uzazi na wajawazito waweze kupata uzazi salama wao na watoto wao.

Hata hivyo, Serikali ilisaini Programu Jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendelo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) kuanzia umri sifuri hadi miaka minane ili kuhakikisha watoto wanaozaliwa wanapata malezi jumuishi katika afua ya afya,,elimu, lishe, ulinzi na usalama na malezi yenyewe mwitikio.

Programu hiyo inashirikiaha wizara mbalimbali pamoja na asasi za kiraia.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...