Na PATRICIA KIMELEMETA

LICHA ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali za utoaji wa elimu kwa shule za awali nchini, Serikali imeendelea kuweka mikakati ambayo ikitekelezeka inaweza kutatua changamoto hizo kwenye shule za awali nchini.

Uamuzi huo umekuja baada ya kuzinduliwa kwa Programu Jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali (PJT-MMMAM) ambayo inaitaka kutekeleza afua tano za afya, lishe, elimu, malezi yenye mwitikio na ulinzi na usalama kwa watoto.

Programu hiyo inatekelezwa kwa watoto wenye umri kuanzia sifuri hadi miaka minane, inashirikisha asasi za kiraia na kutekelezwa ngazi ya mikoa.

Licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali kwenye utekelezaji wake, tafiti zilizofanyika hivi karibuni zinaonyesha kuwa changamoto hizo zinaweza kutatuliwa endapo serikali itarasimisha elimu ya awali kuwa ya lazima kama ilivyo elimu ya darasa la kwanza hadi la saba.

Tafiti hizo zimeonyesha maeneo yenye changamoto kuanzia shule za serikali hadi za wamiliki binafsi, lakini baadhi ya maeneo tayari serikali imeanza kuonyesha jitihada za kutatua changamoto hizo kwa kuwapa mafunzo walimu wa shule za awali ili waweze kujua wajibu wao wakiwa na watoto shuleni.

Taasisi Isiyo ya Kiserikali ya HakiElimu ni miongoni mwa taasisi zilizofanya utafiti huo ambao umeonyesha kuwa, baadhi ya shule hazina walimu, vitendea kazi, miundombinu hafifu pamoja na wazazi hawana elimu ya kutosha juu elimu ya awali na malezi kwa watoto.


Utafiti huo unaojulikana kwa jina la 'Utafiti wa Elimu ya Awali (ECD)' ulianza Desemba 2023 na kuzinduliwa April 2024 ambao wameweza kuzifikia kaya 1200 za Mkoa wa Dar es Salaam na kuonyesha mambo mbalimbali yakiwamo ukosefu wa walimu wenye sifa pamoja na watoto wenye ulemavu kukosa haki sawa na wale wasio na ulemavu.

Mtafiti Mshauri wa HakiElimu, Dk. Wilberforce Meena amesema kuwa, utafiti huo umeonyesha kuwa, kuna changamoto ya wazazi kutojua umuhimu wa kuwapeleka watoto shule kujifunza.

Amesema kuwa, utafiti huo ulifanyika ili kuangalia mambo mbalimbali yanayohusu elimu ya awali pamoja na ushiriki wa wazazi katika masuala ya malezi ya mtoto kulingana na mazingira wanayoishi.

Amesema kuwa, kwa upande wa serikali, shule hazina miundombinu bora ya kufundisha watoto wa madarasa ya awali, hakuna walimu wa kutosha, hakuna bajeti, takwimu pamoja na vitendea kazi.

" Katika shule za awali walizopelekwa, baadhi ya hizo shule hakuna walimu wenye sifa za kuwafundisha, hakuna madarasa ya awali, hakuna vitendea kazi, hakuna mazingira bora ya kufundisha, hakuna lishe na wala weledi.

" Wazazi wenyewe hawana elimu, hawawajali watoto, baadhi ya watoto wanaoishi na walezi na kwamba hawana muda wa kuwaangalia watoto,

Dk. Meena amesema kuwa, serikali inapaswa kuajiri walimu wenye sifa ili waweze kuwafundisha watoto hao, kuboresha miundombinu iliyopo ili iweze kukidhi mahitaji ya watoto, kuboresha huduma muhimu ikiwamo choo ili kuepusha kujichanganya na watoto wengine, kuweka vitendea kazi ii walimu na watoto wao waweze kujifunza kwa umakini.

" Idadi kubwa ya shule za serikali hazina mazingira bora ya kufundisha watoto wa madarasa ya awali na hata miundombinu iliyopo inashindwa kukidhi mahitaji ya watoto wenye ulemavu," amesema.

Amesema kuwa, serikali inapaswa kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kuona umuhimu wa utoaji wa elimu ya awali ili waweze kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kuonyesha ushiriki wao wa moja kwa moja kwenye ujifunzaji wa mtoto.

Naye Mkurugenzi wa Taasisi Isiyo ya Kiserikali ya Kaya Foundation ambayo inajishughulisha na watoto wenye ulemavu,Anapili Ngome amesema kuwa, miundombinu ya madarasa na choo ni muhimu Kwa watoto wenye ulemavu, Kwa sababu itawasaidia kusoma katika mazingira rafiki kulingana na Hali yao.

" Kuna baadhi ya shule, watoto wenye ulemavu wanaosoma madarasa ya awali wanatumia choo kimoja na wale wanafunzi wa madarasa ya juu, jambo ambalo ni hatari kwa hali zao, hivyo basi serikali inapaswa kuboresha miundombinu Ili iwe rafiki," amesema Ngome

Ameongeza kuwa, lakini pia, Serikali inapaswa kuongea vitendea kazi ya watoto wenye ulemavu wakiwamo wale wenye uoni hafifu ili waweze kupata vifaa vya kujifunza kwa sababu wanahitaji vifaa maalumu ambayo vitawasaidia kusoma na kuandika.

Mkurugenzi wa Elimu Msingi na Awali kutoka Wizara ya elimu nchini, Mwl Abdul Maulid amesema kuwa licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali nchini, lakini tayari serikali imewajengea uwezo wa elimu ya awali kwa walimu na wakufunzi maeneo mbalimbali nchini kote ili waweze kutoa elimu bora ya watoto.

Amesema kuwa, lengo la kuwajengea uwezo walimu hao ni kuhakikisha kuwa, uelewa wa kuwafundisha watoto wadogo unaongezeka na wao waweze kuwajengea uwezo walimu wenzao.

Hata hivyo, Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) ilitangaza kuwafikia walimu 4900 Ili waweze kunufaika na mafunzo ya utekelezaji wa mtaala mpya wa elimu ya awali na msingi nchin.

Naibu Waziri wa Tamisemi, Festo Dugange alizitaka Halmashauri zote nchini kutenga bajeti ya fedha kwa ajili ya kununua vifaa vya kujifunza kwa watoto wenye ulemavu ili waweze kupata elimu sawa kama walivyo wanafunzi wasio na ulemavu.

" Ninaagiza Halmashauri zote kutenga bajeti ya fedha ili kuhakikisha kuwa, shule zinakua na vifaa vya kufundishia, ikiwamo vifaa vya watoto wenye ulemavu, fimbo pamoja na vitendea kazi vingine ili kurahisha watoto kusoma," amesema Dugange.

Katika bajeti pendekezwa ya mwaka 2024/25 ilivyowasilishqa Bungeni hivi karibuni na Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mkoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi ) Mohamed Mchengelwa imeeleza kuwa, Serikali imetenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa vitabu na vifaa vilivyoboreshwa vya kufundishia na kujifunzia kwa elimu ya awali kwenye shule 4,500 pamoja na ununuzi wa vifaa saidizi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika shule 130 za msingi na sekondari.

Kadhalika, Serikali inatarajia kutoa mafunzo endelevu ya walimu kazini (MEWAKA) kwenye shule za awali na msingi kwenye halmashauri 140, kutekeleza mpango wa shule salama kwenye shule za awali na msingi 2,500.Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...