Na Mwandishi Wetu
MTENDAJI Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Profesa Elisante Ole Gabriel amesema mifumo ya mahakama ipo vizuri katika utoaji wa haki kwa kuwa maudhui yake yanazingatia vigezo vilivyowekwa na sheria.

Amesema kuwa wapo watu wanadhani kuwa mahakama haitendi haki, lakini huzingatia utoaji wa taarifa (ushahidi) na kama mashitaka yamethibitishwa bila kuacha shaka yoyote.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, Profesa Gabriel alisema kuwa wapo baadhi ya watu ambalo hawataki kutoa ushahidi mahakamani pale wanapotakiwa kufanya hivyo, jambo ambalo si sahihi.

"Suala la kuthibitisha mashitaka bila kuacha shaka ndio mchakato unaoleta ukinzani kwa baadhi ya watu kuona kuwa mahakama haitendi haki lakini ili haki ipatikane ni lazima kuzingatia eneo hili," alisema.

Aliongeza kuwa wadau wakubwa wa mahakama ni mlalamikaji (mdai) na mlalamikiwa (mdaiwa) ambao baada ya kuwasilisha mashitaka yao na kutoa ushahidi, mahakama inaangalia kama mashitaka hayo yamethibitishwa bila kuacha shaka yoyote na ndipo haki inapopatikana.

Aliwahakikishia watanzania kuwa mhimili huo uko huru na haimaanishi kuwepo kwa mihimili mitatu, washindwe kushirikiana katika majukumu mbalimbali.

Alifafanua kuwa mahakama ina majukumu matano ambayo ni kutoa haki kwa wote bila kujali hali ya mtu kiuchumi, kijamii, kutochelewesha kesi bila sababu za msingi, kutoa fidia kwa mujibu wa sheria na kukuza usuluhishi.

Hivyo, alisema ni wakati wa watanzania kujikita katika usuluhishi wa migogoro yao badala ya kupeleka mashauri mahakamani kwani itasaidia kuwa na mahusiano mazuri badala ya uadui.

Profesa Gabriel alisema kipo kituo cha usuluhishi kwa ajili kazi hiyo na kwamba jamii, wazazi na walezi wafundishe watoto wao kutumia maridhiano katika kutatua migogoro mbalimbali kupunguza gharama za uendeshaji wa kesi na mrundikano wa kesho.

"Niwaombe tusijichukulie sheria mkononi bali tutii sheria bila shuruti na tuzifahamu haki zetu pale tunapokumbana na mkono wa sheria," alisisitiza.

Akizungumzia mafanikio ya mahakama hiyo, Profesa Gabriel alisema kuwa tangu kuanza kwa mahakama mwaka 1920, walikuwa na majaji watatu wa Mahakama Kuu ya Tanganyika na sasa wapo majaji 109.

Alieleza kuwa Mahakama ya Rufani iliyoanza mwaka 1979 ilikuwa na majaji watano na hivi sasa kuwa majaji 35 na mahakimu 1,355.

Mtendaji huyo alisema kuna mahakama za Mwanzo 960, za Wilaya 135, Mahakama Kuu katika kanda 19, Mahakama za divisheni nne (Biashara, Ardhi, Kazi, Rushwa na uhujumu uchumi) na masijala 19.

‘’Mahakama ilianza na watumishi 120 lakini tunavyoongea kuna watumishi 5,850 lakini uhitaji wetu ni watumishi 10,351 kwa kuwa wahalifu hawastaafu tunahitaji mahakimu na majaji wa kutosha,’’ alisema.

Pia alieleza kuwa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) inawasaidia kuongeza ubora wa huduma wanazozitoa na kupunguza mzigo kwa majaji na mahakimu wa kushughulikia mashauri.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akizungumza na wandishi wa habari katika mkutano wake na waandishi hao leo Julai 4,2024. Mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Mikutano wa wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke jijini Dar es Salaam
Baadhi ya Watendaji na Naibu Msajili waliohudhuria mkutano kati ya Mtendaji Mkuu wa Mahakama na Waandishi wa Habari uliofanyika leo tarehe 04 Julai, 2024 kwenye ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke jijini Dar es Salaam. Katikati ni Mtendaji wa Mahakama Kuu-Divisheni, Bi. Mary Shirima, kushoto ni Mtendaji wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia-Temeke, Bw. Samson Mashalla na kulia ni Naibu Msajili wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia-Temeke, Mhe. Evodia Kyaruzi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...