MATUMIZI ya mbolea hapa nchini,yameongezeka kutoka wastani wa tani
363,599 katika msimu wa kilimo 2021/202 hadi kufikia tani 840,714 kwa
msimu wa kilimo 2023/2024.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa mbolea Tanzania Joel
Lauren amesema hayo jana,wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kuhamasisha
usajili wa wakulima na matumizi sahihi ya mbolea uliofanyika wilayani
Mbinga.
Amesema,mkoa wa Ruvuma ambao ni kati ya Mikoa ya kimkakati ya uzalishaji
wa chakula hapa nchini, kwa miaka ya karibuni umeongoza kwa matumizi ya
mbolea ambapo msimu 2022/2023 Mkoa huo ulitumia zaidi ya tani 83,472.
"katika msimu 2023/2024 mkoa wa Ruvuma umetumia tani 113,000,hivyo
kuendelea kuwa kinara kwa matumizi ya mbolea na kuwa miongoni mwa mikoa
tegemezi katika uzalishaji wa chakula hapa nchini"amesema.
Laurent alitaja mikoa inayofuatia kwa matumizi ya mbolea ni Njombe tani
75,358,Mbeya tani 75,252,Songwe tani 71,230 na mkoa wa Iringa ambao
umetumia tani 44,214.
Amesema,matumizi ya mbolea kwa sasa ni muhimu kutokana na kuongezeka kwa
idadi ya watu kunakohitaji ongezeko la uzalishaji wa chakula ili
kukidhi mahitaji,ukuaji wa miji,miundombinu na huduma za kijamii
zinazochangia kupunguza eneo linalofaa kwa kilimo.
Ameeleza kuwa,matumizi sahihi ya mbolea kunaongeza tija na kuchangia
kukuza kipato cha mkulima mmoja mmoja,ukuaji wa sekta ya kilimo na pato
la Taifa kwa ujumla.
Ameongeza kuwa,hapa nchini kuna mbolea za viwandani na mbolea za asili
ambazo zinatumiwa na wakulima,lakini changamoto ni matumizi kidogo ya
mbolea kwa baadhi ya maeneo kunatokana na dhana potofu kwamba mbolea
inaharibu ardhi na baadhi ya wakulima kukosa elimu ya matumizi sahihi ya
mbolea”alisema Laurent.
Amewakumbusha wakulima umuhimu wa kutumia mbolea katika uzalishaji wa
mazao kwenye mashamba yao kwani unasaidia kurutubisha,kuboresha afya ya
udongo na kuzalisha mazao kwa wingi katika eneo dogo.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga alisema,sekta ya
kilimo ndiyo mhimili wa uchumi wa Tanzania na inaajiri takribani
theluthi mbili ya nguvu kazi ya Taifa na inachangia asilimia 65 ya
malighafi za viwandani,asilimia 100 ya usalama wa chakula na zaidi ya
asilimia 26 ya pato la Taifa.
Kapinga amesema,katika mazingira ambayo kilimo ndiyo sekta ya
uchumi,maendeleo ya mwananchi na Taifa kwa ujumla yanategemea zaidi
ufanisi katika sekta hiyo.
Amesema,Serikali ya awamu ya sita imedhamira kufanya mapinduzi makubwa
katika sekta ya kilimo kwa kuongeza bajeti ya wizara kutoka takrbani
Sh.bilioni 294 mwaka 2021/2022 hadi kufikia Sh.trilioni 1.24 kwa mwaka
2024/2025.
Amewataka wakulima hapa nchini wakiwemo wa wilaya ya Mbinga na mkoa wa
Ruvuma,kuchangamkia fursa zinazotolewa na Serikali kwa kujisajili katika
mfumo wa kidijitali kupitia Ofisi za Watendaji wa vijiji na mitaa.
Naibu Waziri Kapinga alisema,kujisajili kwenye mfumo wa kidijitali
kutawaweza wakulima kununua mbolea kwa gharama nafuu,kuongeza
uzalishaji,kuboresha maisha yao na kuchangia ukuaji wa uchumi.
Ametaja faida nyingne kwa wakulima kujisajili kwenye mfumo wa
kidijitali,ni kuiwezesha serikali kupata takwimu sahihi zitakazotumika
kuweka mipango ya kuwaendeleza wakulima,sekta ya kilimo na kupata huduma
za ugani,taarifa za masoko na huduma za kifedha kupitia kanzidata.
Kaimu Katibu Tawala wa mkoa wa Ruvuma Jumanne Mankhoo,ameipongeza
mamlaka ya udhibiti wa ubora wa mbolea kwa kusimamia vema upatikanaji wa
pembejeo za ruzuku iliyosaidia kupatikana kwa wingi na kwa urahisi
katika meneo mengi ya mkoa huo.
Naye Mkurugenzi wa uzalishaji wa ndani na ununuzi wa mbolea kwa pamoja
wa TFRA Dkt Louis Kasera alisema,kampeni hiyo inalenga kuhamasisha
wakulima kote nchini juu ya matumizi sahihi ya mbolea ili waweze kongeza
uzalishaji.
Amewahakikisha wakulima kuwa,mpango wa mbolea za ruzuku utaendelea
kutolewa hadi katika msimu wa kilimo 2024/2025 na kuwataka wakulima
waongeze juhudi na kutumia mbolea kwenye shughuli zao za kilimo.
Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga kulia,akiangalia mbegu za mazao hususani mahindi kwenye uzinduzi wa kampeni ya Uhamasishaji wa matumizi sahihi ya mbolea kwa wakulima uliofanyika katika Hotel ya One Pasific mjini Mbinga.
Badhi ya watendaji wa sekta ya kilimo kutoka mkoa wa Ruvuma na Mamlaka ya udhibiti wa ubora wa mbolea Tanzania(TFRA)wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga(hayupo pichani)wakati wa usinduzi wa kampeni ya Uhamasishaji wa matumizi sahihi ya mbolea kwa wakulima hapa nchini,uzinduzi uliofanyika katika Hotel ya One Pasific wilayani Mbinga.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...