Wananchi wa Bariadi wakifuatilia moja ya burudani ya ngoma za kiasili wakati wa Tamasha la Utamaduni na Utalii Kanda ya Ziwa lililofanyika katika Viwanja vya CCM Bariadi kwa siku tatu kuanzia Julai 5 na kuhitimishwa Julai 7,2024. Tamasha hilo liliandaliwa na Kampuni ya Kilimanjaro One Travel and Tours.

Na Mwandishi wetu, Simiyu.
TAMASHA la Utamaduni na Utalii Kanda ya Ziwa-Lake Zone Cultural and Tourism Festival lililomalizika Mjini Bariadi, Mkoani Simiyu limeacha gumzo kubwa baada ya kuwavutia zaidi ya watu 10,000 katika Uwanja wa CCM Bariadi.

Tamasha hilo la aina yake lililoandaliwa na kampuni ya Kilimanjaro One Travel and Tours, limefanyika kwa siku tatu mfulululizo na kujumuisha kila aina ya burudani ikiwemo ngoma za asili na pambano kati ya makundi mawili ya wagika na wagulu ambazo zilileta msisimko mkubwa.

Akizungumza wakati wa ufungaji wa tamasha hilo, Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Simon Simalenga aliipongeza Kampuni hiyo na kusema Tamasha hilo lilikuwa la aina yake.

“Naipongeza sana kampuni ya Kilimanjaro One kwa hiki walichokifanya na kuweza kuukusanya umati wote huu na kuhakikisha tamasha hili linafanikiwa,” alisema huku akiwapongeza wananchi pia kwa kudumisha amani wakati wote wa tamasha hilo.

Pia Simalenga ametoa wito kwa waandaaji wahakikishe tamasha hilo linafanyika kila mwaka kwani wana Simiyu wameshalielewa na wana matarajio makubwa kwa mwakani.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kilimanjaro one Travel and Tours, Christina Jengo alisema Tamasha hilo lilifanikiwa kwa kiasi kikubwa kwani walitarajia watu 7000 lakini mwisho wa siku tamasha hilo lilivutia zaidi ya watu 10,000 kutoka ndani na nje ya Simiyu.

“Tutaendelea kuboresha mwaka hadi mwaka na tunaamini kuwa Kilimanjaro One Travel and Tours Limited ndio kampuni ya kwanza kabisa kuandaa tamasha kubwa hivi la utamaduni na utalii,” alisema.

Aidha alishukuru wadhamini wa tamasha hilo ambao ni pamoja na NMB Bank, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Z&M General Traders, Widescope Enterprises Limited, na Carehealth and Hospitality Services. “Naamini baada ya tamasha hili la kwanza mwaka huu, mashirika mengine yataona umuhimu wa kuunga mkono tukio la mwakani maana nimearifiwa hili litakuwa tamasha la kila mwaka.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Afisa Utamaduni, Nyambeho Magesa aliipongeza kampuni ya Kilimanjaro One Travel and Tours kwa kuunga mkono mwito wa Rais Mh. Dk Samia Suluhu Hassan ya kuanzisha tamasha katika kila mkoa kwani wao wamefanya kwa vitendo.

Alisema Wizara hiyo itaendelea kufanya kazi pamoja na Kilimanjaro One Travel and Tours na Wizara ya Maliasili na Utalii kukuza utalii wa utamaduni huku akitoa wito kwa makundi mbalimbali ya ngoma ya Mkoa wa Simiyu kujisajili na Baraza la Sanaa Tanzania ili waweze kufaidika na mambo mbalimbali ikiwemo mikopo vya makundi.


Wananchi wa Bariadi wakifuatilia moja ya burudani ya ngoma za kiasili wakati wa Tamasha la Utamaduni na Utalii Kanda ya Ziwa lililofanyika katika Viwanja vya CCM Bariadi kwa siku tatu kuanzia Julai 5 na kuhitimishwa Julai 7,2024. Tamasha hilo liliandaliwa na Kampuni ya Kilimanjaro One Travel and Tours.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...