Dar es Salaam.
Baada ya muda mrefu wa kutoa huduma za kisheria bila taaluma, hatimaye kazi ya usaidizi wa kisheria imetambuliwa na kuwa taaluma rasmi.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo (LST) kupewa jukumu la kutoa mafunzo ya taaluma hiyo kwa ngazi ya Cheti (Certificate) na Stashahada (Diploma).
Licha ya Wasaidizi wa Kisheria kuwa nguzo muhimu ya utoaji msaada wa kisheria kwa wananchi mbalimbali hasa vijijini, wengi wao walikumbwa na kejeli kuwa, kazi wanazofanya hazikuwa rasmi.
Hatua ya taaluma hiyo kufundishwa katika taasisi hiyo, imeelezwa na Mratibu wa Mafunzo hayo kutoka LST, Dk. Kevin Mandopi alipokuwa katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba jijini Dar es Salaam ambapo LST inashiriki.
Kwa mujibu wa Dk. Mandopi, uamuzi wa utoaji mafunzo ya Wasaidizi wa Kisheria kwa ngazi ya cheti na diploma umefikiwa ukilenga kuiimarisha taaluma hiyo.
Msingi wa kuimarisha taaluma hiyo ni kutokana na umuhimu wake kwa wananchi wengi hasa walioko vijijini, ambao aghalabu hupoteza haki zao kwa kutojua taratibu za kisheria.
“Imekuwa taaluma rasmi na inayoheshimika na kutambuliwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi ( NACTVET), Serikali imetutaka tufanye hivi kwa kutambua umuhimu wa Wasaidizi wa Kisheria nchini. Kama inavyotambulika kwa sasa Rais Samia Suluhu Hassan ameanzisha usaidizi wa kisheria nchini kote na watu wengi wanasaidiwa,” amesema.
Amesema hadi sasa tayari kuna wahitimu 15 wa ngazi ya Cheti ya taaluma hiyo na sasahivi dirisha limeshafunguliwa kwa ajili ya kutuma maombi ya ngazi ya cheti na diploma.
Sambamba na hilo, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sagini alipofanya ziara katika taasisi hiyo mwezi Juni mwaka huu, pamoja na mambo mengine, alisema Serikali ipo katika hatua za kuwatambua rasmi Wasaidizi wa Kisheria ndio maana LST wamepewa jukumu la kutoa mafunzo hayo.
Mratibu wa Mafunzo ya Wasaidizi wa Kisheria kutoka Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (LST), Dkt. Kevin Mandopi (kushoto) akizungumza na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dk. Yose Mlyambina alipotembelea banda la LST katika Maonesho ya Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...