-Asisitiza umeme wa gridi ya taifa Kigoma ifikapo Machi 2025

-Apokea mamia ya wanachama wapya, wakiongozwa na Mbunge wa Chadema Kigoma na Diwani wa DP

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi amesema ahadi ya kuufungua Mkoa wa Kigoma kuwa lango kuu la biashara inaendelea kutekelezwa kwa vitendo.

Balozi Nchimbi amesema ahadi hiyo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inatekelezwa kwa hatua thabiti, kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo inalenga kuzidi kuufungua mkoa huo, kuendelea kuunganisha na mikoa mingine lakini pia kuiunganisha Tanzania kibiashara na nchi zingine kupitia Kigoma.

Balozi Nchimbi amesema hayo alipokuwa akiwahutubia maelfu ya wananchi wa Kigoma, katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Mwanga Community Centre, mjini Kigoma, Jumapili Agosti 4, 2024.

Katibu Mkuu Balozi Nchimbi amezitaja hatua zinazochukuliwa na Serikali ya CCM inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuwa ni pamoja na ujenzi wa barabara za lami, ujenzi wa meli mbili kubwa kwa ajili ya kuboresha usafiri wa Ziwa Tanganyika, ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Dar Es Salaam hadi Kigoma na kutoka Kigoma kwenda nchi za jirani pia mipango ya kuiboresha Reli ya Kati.

“Nimeambiwa ahadi mbalimbali ambazo Mhe. Rais Dokta Samia Suluhu Hassan alitoa, ikiwemo ya kuufungua Mkoa wa Kigoma. Ninyi ni mashahidi kuwa ahadi hiyo imeendelea kutekelezwa kwa vitendo. Mchakato wa barabara za lami unaendelea Kasulu, Kibondo na Buhigwe.

“Lakini juzi mmesikia wakati Rais anazindua treni ile inayotumia umeme (SGR), kuwa dhamira ni kuifikisha Kigoma. Pia mchakato wa kuiboresha Reli ya Kati unaendelea. Hebu pigeni picha kubwa yote haya yakikamilika, Kigoma itafunguka haijafunguka,” amesema Balozi Nchimbi.

Balozi Nchimbi pia alielekeza utekelezwaji wa ahadi ya kuipatia Mkoa wa Kigoma umeme wa uhakika kwa kuunganisha kwenye gridi ya taifa, ifikapo mwezi Machi, 2025, ambapo ujenzi wa vituo vya kupozea umeme katika maeneo ya Nguruka na Kidahwe uko katika hatua za mwisho kukamilika.

Katika hatua nyingine, ziara hiyo ya Katibu Mkuu Balozi Nchimbi katika Mkoa wa Kigoma iliyoanza jana Agosti 4, 2024, imepokea mamia ya wanachama wapya waliojiunga CCM kutokea vyama vingine, wakiongozwa na aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum wa Chadema Mkoa wa Kigoma, Bi. Sabrina Sungura na Diwani wa Kata ya Mwakizega, Wilaya ya Uvinza, Ndugu Patrick Wilis Bitaliho kutoka Chama cha DP, hivyo kuendeleza wimbi kubwa la wanachama na viongozi wa vyama vya upinzani wanaojiunga CCM katika ziara hizo wakisema wazi kuwa wanavutiwa na uongozi wa Chama na Serikali chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

















Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...