Na Said Mwishehe Michuzi TV
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kupitia Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama CPA Amoss Makala kimepongeza uwekezaji mkubwa uliofanyywa na Serikali katika Bandari ya Dar es Salaam sambamba na uwekezaji wa DP World ambao umewezesha kumalizwa kwa msongamano wa kontena bandarini.
Akizungumza leo Agosti 28,2024 alipofanya ziara ya kutembelea Bandari ya Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya ziara yake inayoendelea katika Mkoa huo CPA Makala amesema Chama kinafurahishwa na maendeleo makubwa katika bandari hiyo.
" Naipongeza Wizara ya Uchukuzi pamoja na Mamlaka ya Bandari Tanzania( TPA) kwa kazi kubwa na nzuri wanaoendelea kuifanya katika kuboresha utendaji kazi wa Bandari zetu na hasa Bandari ya Dar es Salaam.
"Wakati wa kupata muwekezaji (DP World) kulikuwa na mjadala mkubwa sana lakini kwa tunaojua hatukushangaa maana tulishakuwa na TICS lakini zamu yao imeisha na sasa ni DP World. CCM tuko hapa leo kumpongeza Mwenyekiti wa Chama na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia Ilani ya uchaguzi.
"Uwekezaji mkubwa na maboresho haya katika Bandari ya Dar es Salaam ni matokeo ya usimamizi wa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi Mkuu.Ni wajibu Wetu CCM kupanga kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania,"amesema CPA Makala.
Akifafanua zaidi amesema kazi ya vyama vya upinzani ni kupinga lakini kazi ya CCM ni kupanga kunawajibu wa watu Fulani, kazi ya CCM ni kupanga kwa ajili ya kuleta maendeleo.Wengine kazi Yao ni kupinga na tunawatakia kila la kheri katika kazi hiyo ya kupinga.
"Kwa hiyo sisi tunaowajibu na dhamana wa kuleta maendeleo ya Watanzania,hatukushangaa kuona watu wanapinga.Ukiona adui yako anakupongeza kwa jambo ambalo unafanya hilo jambo achana nalo. Walipinga ndege leo tunapanda nao, walipinga ujenzi wa SGR leo tunapanda nao."
Akielezea zaidi kuhusu DP World,CPA Makala amesema tangu waanze kazi bandarini wanamuda wa miezi minne na wameanza kwa kufanya maboresho mbalimbali ambapo tayari wameshatumia Sh.bilioni 214 na mpango wao ni kutumia Sh.Bilioni 675 kwa ajili ya vifaa vya kisasa.
Amesema kabla ya DP World kulikuwa na foleni kubwa ya Meli zenye makontena lakini sasa hakuna foleni na kwa upande meli za kichele kutoka saba mpaka meli moja."Hivyo unaona kwa ushahidi tangu DP World wameanza kazi kuna mabadiliko makubwa.
"Katika biashara unaangalia muda na gharama za mlaji ,hivyo kupitia uwekezaji wa DP World yamepatikana yote mawili.Pia yameongeza na kubwa zaidi Bandari ya Dar es Salaam imeanza kuwa na sifa ya kushindana na bandari nyingine za Afrika na duniani.
"Tumeambiwa Bandari ni Ushindani lakini asilimia 90 ya soko bado linashikiliwa na Bandari ya Dar es Salaam.Tunapongeza Serikali kwa ujenzi wa SGR kuungwanishwa na bandari ya Dar es Salaam.
"Tayari Rais amewekeza katika meli ya kubeba makasha katika Bandari ya Mwanza ,kwa hiyo makasha yakitoka Dar es Salaam yanapakiwa katika ya SGR na kufika kufika Mwanza na kisha yanapakiwa katika meli hiyo kupelekwa Uganda.Kauli ya Rais Samia kufungua nchi inatekelezwa kwa vitendo."
CPA Makala amewaomba viongozi wa bandari ya Dar es Salaam kuchaka kazi,wasirudi nyuma na kusisitiza kwamba TPA wamepata baraka zote za Chama Cha Mapinduzi.
"Mnachokifanya ni utekelezaji wa Ilani lakini mkumbuke biashara ni ushindani na hivyo wengine wanatamani soko hivyo ni vema kuendelea kufanya maboresho na kushika soko."
Akizungumza kuhusu wafanyakazi, CPA Makala amesema kulikuwa na na maneno mengi kwamba uwekezaji huo utawaweka nje wa Watanzania waliokuwa wanaofanyakazi bandarini hapo na kwamba zaidi ya wafanyakazi 350 wako DP World.
"Hakuna aliyepoteza kazi wote wako kazini na hii wamethibitisha kwa vitendo kwamba uwekezaji huu umekuwa na tija kwa Watanzania."
Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania(TPA) Juma Kijavara amesema tangu Rais Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani kumekuwa na maboresho makubwa ya miundombinu ya Bandari huku akifafanua kwa sasa muda wa kushusha kontena umepungua kutoka siku 20 mpaka siku saba.
Amesisitiza kuna mambo mengi yamefanyika ndani ya muda mchache tu baada ya Rais DK. Samia kuingia madarakani na kufanua umefanyika ukarabati mkubwa katika Bandari ya Dar es Salaam pamoja na bandari nyingine nyingine nchini.
"Tunao wawekezaji wawili akiwemo DP World na uwepo wawekezaji umesaidia kumpunguza muda wa kushusha kontena kutoka siku 20 mpaka siku saba.Tena kwa DP World meli zinakuja na kufunga bandarini siku hiyo hiyo ,hivyo kuna mabadiliko makubwa."
Ameongeza kuwa DP World wamewezesha kuongezea kwa mitambo kwa ajili ya kurahisisha upakiaji na upakuaji wa kontena katika Bandari ya Dar es Salaam .Pia DP World wamenunua jenereta kubwa mbili zenye uwezo wa KV zaidi 10000 kwa lengo kusaidia umeme iwapo umeme wa TANESCO utakatika.
Pia amesema DP World imenunua RTG kwa ajili ya kurahisisha shughuli za ubebaji makasha sambamba na ukarabati wa vifaa vilivyokuwa vimeharibika.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...