Dar es Salaam. Tarehe 27 Agosti 2024: VIONGOZI wa dini nchini wameipongeza Benki ya CRDB kwa kuzindua Akaunti ya Sadaka mahsusi kwa ajili ya taasisi za dini kukusanya sadaka, zaka na michango mingine inayolenga kuwarahisishia waumini kumtolea Mwenyezi Mungu wakati wa ibada au hata wanaposhindwa kuhudhuria ibada.
Akizungumza kuhusu Akaunti ya Sadaka Naibu Katibu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padre Chesco Msaga amesema nimapinduzi yatakayosaidia kuwakumbusha Wakristo kumtolea Muumba wao ili kukamilisha kazi kubwa ya uenezi wa Injili nchini na duniani kwa ujumla.
“Maisha ya mwanadamu hayana maana yoyote hapa duniani asipomwabudu Muumba wake na kumtolea zaka na sadaka kama ilivyoagizwa katika Biblia Takatifu. Nawapongeza Benki ya CRDB kwa ubunifu huu na nawaomba Wakristu kote nchini kuiona fursa hii ya kumtolea Bwana kirahisi,” amesema Padre Msaga.
Naibu katibu huyo wa TEC amesema fursa zinazoletwa na maendeleo ya sayansi na teknolojia zinapaswa kutumiwa na Wakristu kuimarisha ukaribu wao na Mwenyezi Mungu na kumtolea sadaka na zaka pamoja na michango mingine ni kati ya njia kuu za kutimiza agano na kuieneza Injili Takatifu.
Akizungumza kwa niaba ya Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Dkt. Abubakary Zubery Bin Ally, Sheikh Hilal Shaweji almaarufu kama Sheikh Kipozeo naye amepongeza ubunifu uliofanywa akisema utawafaa sana Waislamu kushiriki kutoa sadaka ambayo ni kati ya nguzo muhimu za dini ya Kiislamu.
“Waislamu tumeagizwa kutoa sadaka na zaka. Tumeagizwa kutoa sadaka kwa ajili ya kuwasaidia wasiojiweza na kuendeleza Uislamu duniani. Ubunifu uliofanywa na Benki ya CRDB unaturahisishia kutimiza msingi huu muhimu kwa imani yetu. Tusiwe tena na sababu ya kuwa mbali na Mwenyezi Mungu,” amesema Sheikh Kipozeo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema siku zote wamekuwa wakijitahidi kubuni huduma na bidhaa zinazokidhi mahitaji na matarajio ya wateja ukigusa sekta tofauti ukiwamo utamaduni na imani za watu watu wanaowahudumia.
“Maneno Matakatifu yanasema binadamu aliumbwa ili amtukuze Muumba wake. Hili ni jukumu letu wanadamu kwa kipindi chote cha maisha yetu hapa duniani. Katika kumtukuza Mwenyezi Mungu, tunakumbushwa kumtolea sadaka na zaka pia. Azma ya Benki yetu ya CRDB siku zote imekuwa kukidhi matarajio na mahitaji ya wateja wetu na jamii tunayihudumia kwa ujumla. Katika kufanikisha hili tumekuwa tukibuni huduma na akaunti zinazoendana na misingi ya imani pamoja na maeneo mengine mfano biashara, uwekezaji na utunzaji akiba,” amesema Nsekela.
Katika jitihada hizi, Nsekela amesema tayari Benki ya CRDB imebuni Huduma za Al Barakah zinazoendana na imani ya Kiislam lakini bado kuna fursa ya kuwahudumia zaidi waumini wote pamoja na taasisi za dini kwa ujumla ndio maana sasa imeleta Akaunti ya Sadaka.
Hali hii, amesema inatokana na ukweli kwamba ukuaji wa uchumi wa kidijitali umepunguza matumizi ya fedha taslimu kwa kiasi kikubwa hivyo Benki ya CRDB imeona umuhimu wa kuingia kwenye nyumba za ibada na kuwapa waumini mbadala wa kutoa sadaka, zaka na kulipa michango tofauti inayojitokeza mara kwa mara.
“Kwa kuuona umuhimu na kutambua wajibu wetu kwa jamii na Mola aliyetuumba ambaye ndiye anaendelea kuilinda biashara yetu, Benki yetu ya CRDB inayoongoza kwa ubunifu imekuja na huduma mpya ya Akaunti ya Sadaka itakayowafaa waumini wa dini zote nchini. Akaunti hii inawaunganisha waumini na nyumba yao ya ibada wakati wowote,” amesisitiza.
Kwa kanisa au msikiti utakaokuwa na Akaunti ya Sadaka, litamrahisishia muumini kutoa sadaka yake, zaka au kulipa michango mingine kutoka kwenye akaunti yake binafsi na kuiingiza kwenye akaunti ya nyumba yake ya ibada isiyokuwa na makato ya kila mwezi wala gharama za uendeshaji na akathibitisha hilo kwa kutuma risiti kwa kiongozi husika.
Hata atakaye kuwa na dharura kwa mfano ugonjwa, safari, msiba au shughuli nyingine za kijamii ambazo kwa namna moja au nyingine itamzuia kuhudhuria ibada na kumpa wasaa wa kuzungumza na Mwenyezi Mungu ingawa alipanga kufanya hivyo, amesema bado anaweza kutoa sadaka, zaka au michango husika bila wasiwasi wowote.
“Napenda kuwataarifu kwamba Benki ya CRDB leo inazindua Akaunti ya Sadaka ambayo ni maalumu kwa ajili ya kukusanya michango yote ya nyumba ya ibada yaani kanisa au msikiti hivyo kutoa ushiriki wa uhakika kwa kila muumini bila kujali amehudhuria ibada au la. Muumini anaweza kufanya hivyo kwa kwenda tawini, kwa wakala, kutumia huduma zetu za Benki kwa njia ya intaneti au simu ya mkononi kupitia Simbanking,” amesema Nsekela.
Mkurugenzi amewasihi Watanzania kumtolea Mwenyezi Mungu fungu lake bila kukosa kwani Benki ya CRDB imeondoa ugumu uliokuwepo mwanzoni.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...