Raisa Said, Tanga
Katika kipindi cha miaka michache iliyopita, Mkoa wa Tanga umepambana kwa bidii kukabiliana na tatizo la utelekezaji wa watoto wenye umri chini ya miaka saba.
Kwa mujibu wa Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Tanga, Mmassa Malugu, mikakati iliyowekwa na serikali imeanza kuzaa matunda, ambapo idadi ya watoto wanaotelekezwa imeshuka kutoka 387 mwaka 2019 hadi 207 mwaka huu wa 2024.
Utelekezaji
wa watoto, hasa wale wenye umri wa chini ya miaka saba, ulikuwa ukishamiri mkoani Tanga kutokana na sababu mbalimbali za kiuchumi na kijamii.
Takwimu za mwaka 2018 zilionesha kuwa Mkoa wa Tanga ulikuwa unashika nafasi ya juu kwa visa vya utelekezaji, na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Watoto, Mwajuma Magwiza, alithibitisha kuwa mkoa huu uliongoza kwa kuwa na visa 1,039, ukiwafuata Mkoa wa Mbeya kwa visa 1,017.
Mikakati ya Kukabiliana na Utelekezaji
Malugu alieleza kuwa, kwa sasa, juhudi mbalimbali zimechukuliwa ili kupunguza utelekezaji. Miongoni mwa hatua hizo ni uanzishwaji wa Kamati za MTAKUWA katika ngazi za vijiji, kata, na halmashauri. Kamati hizi zina lengo la kusaidia malezi na makuzi ya watoto, huku zikishirikisha wataalamu na jamii kwa ujumla.
"Kamati hizi zimesaidia ufuatiliaji wa karibu wa watoto na kuimarisha utoaji wa taarifa kuhusu ukatili dhidi ya watoto," alisema Malugu.
Hatua nyingine ni kutoa elimu kwa njia ya vyombo vya habari ikiwemo makala na vipindi vya redio vilivyofanywa kupitia Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendelo ya Mtoto (PJT MMMAM).
Pia, uimarishaji wa mfumo wa watu wa kuaminika umekuwa na mchango mkubwa, ambapo watoto wanaopatikana wakiwa wametelekezwa wanahifadhiwa na watu hao, hivyo kutoa fursa ya malezi bora.
Mabadiliko katika Utawala na Ufuatiliaji
Kwa mujibu wa Malugu, uimarishaji wa mchakato wa mashauri ya ukatili wa kijinsia umechangia kupunguza utelekezaji, ambapo sasa kesi hazichukui muda mrefu.
Uanzishwaji wa Polisi Jamii pia umesaidia kupunguza matukio ya ukatili katika jamii.
Katika Wilaya ya Mkinga, tatizo la utelekezaji linashughulikiwa kwa karibu. Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Kenneth Solomon, alieleza kuwa maeneo kama Mwakijembe yanakabiliwa na changamoto kubwa kutokana na mila na desturi za jamii, lakini elimu wanayoitoa inasaidia kupunguza matukio hayo.
Kwa upande wao ,Wakazi wa Tanga.Amina Jumaa, wameeleza kuwa kuwepo kwa Kamati za MTAKUWA kumekuwa na manufaa makubwa.
Amina anasema, "Uwepo wa kamati hizi umesaidia kuongeza uwazi katika ripoti za matukio ya utelekezaji na kumekuwa na ulinzi wa watoto ambao wanaweza kufikiwa kwa urahisi."
Mikakati iliyowekwa na Mkoa wa Tanga katika kukabiliana na utelekezaji wa watoto imeonyesha matokeo chanya. Hata hivyo, bado kuna kazi kubwa ya kufanya ili kuhakikisha kwamba watoto wote wanapata malezi bora na salama.
Kuendelea kutoa elimu na kuimarisha ushirikiano kati ya jamii na serikali ni muhimu katika kufikia lengo hilo. Utekelezaji wa sheria na kanuni zinazopambana na utelekezaji ni muhimu ili kuwalinda watoto wetu na kuwapa fursa ya kuendelea na maisha bora.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...