Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Ahmed Abbas Ahmed ,akizungumza na wamiliki wa hoteli kuhusu fursa za Tamasha la Kitaifa la Utamaduni
Baadhi ya wamiliki wa hoteli wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Ahmed Abbas Ahmed (hayupo pichani) wakati ,akizungumza na wamiliki wa hoteli kuhusu fursa za Tamasha la Kitaifa la Utamaduni
*Rais Samia apongezwa
*Wafanyabiashara wafunguka
Na Mwandishi Wetu, RUVUMA
TAMASHA la Tatu la Utamaduni la Kitaifa lenye lengo la kukuza utamaduni nchini linatarajiwa kufanyika Septemba 20-23, mwaka huu mkoani Ruvuma ambapo Rais Samia Suluhu Hassan atakuwa mgeni rasmi.
Kutokana na ujio wa tamasha hilo, wafanyabishara wa Mkoa huo wameeleza shauku yao na namna walivyojipanga kuchangamkia fursa za kibiashara zinazoambatana na tamasha hilo na kumshukuru Rais kwa kuridhia lifanyike kwenye eneo lao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Wafanyabishara hao wamesema mkoa huo unasifika kwa kilimo na upatikanaji wa makaa ya mawe ambayo yameifungua zaidi Ruvuma kiuchumi.
Mfanyabiashara katika Soko Kuu la Songea Mjini Tito Mbilinyi, amesema: “Namshukuru Rais Samia kwa kutuletea hili tamasha sisi kama wafanyabiashara tumefurahi na kila mfanyabiashara atanufaika kwasababu ugeni utakaokuja sio mdogo una takribani watu 5000, tutanufaika.”
Amesema kwa miaka mingi wamekuwa wakiomba kuwa na matukio ya kitaifa kama hilo na kumshukuru Rais kwa kuwapelekea tamasha hilo ambalo kwao ni fursa muhimu.
“Tunamshukuru Rais anatuelewa zile changamoto ambazo tunazilalamikia sisi wa sekta binafsi ameanza kuzitatua tunamshukuru sana, karibu sana Ruvuma Rais Samia, sisi Ruvuma ni wenyeji wa kulima mahindi tunaongoza mkoa sisi tunalisha mikoa mbalimbali yenye shida ya chakula nan je ya nchi,”amesema.
Naye, Meneja wa moja ya hoteli mkoani humo, Upendo Mwakitapwa, amesema mkoa huo kiuchumi unaendelea kupaa zaidi kutokana na kuwapo na mzunguko wa kibiashara ikiwamo makaa ya mawe.
“Tunampokea kwa mikono miwili kwa ajili ya maendeleo ya Ruvuma, tumejipanga kwa ajili ya tamasha la utamaduni linalofanyika kimkoa Ruvuma,”amesema.
Amebainisha ujio wa Rais Samia kwenye mkoa huo ni fursa kwa wafanyabiashara wa mkoa huo na kuwahimiza waongeze ubunifu wa kibiashara ili wajikwamue kiuchumi.
Juzi, Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni,Sanaa na Michezo Gerson Msigwa, ameeleza kuwa tamasha hilo litafanyika Manispaa ya Songea mkoani humo na Kaulimbiu ni ‘Utamaduni wetu ni utu wetu, tuuenzi na kuuendeleza, Kazi iendelee’.
Amesema Tamasha linaratibiwa na Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwamo waratibu wa Tamasha la Majimaji Serebuka, kutoka mkoani, Ruvuma Songea.
“Tamasha hilo litafunguliwa na Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt. Damas Ndumbaro,Septemba 20,mwaka huu na kilele chake itakuwa Septemba 23,mwaka huu na mgeni rasmi atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan”amesema Msigwa
Amesema kuwa Tamasha hilo limekuwa na faida nyingi kwa jamii ambazo ni pamoja na; kuenzi utamaduni wetu, kuimarisha utangamano wa kitaifa, kuitangaza nchi, kutangaza vivutio vya kiutalii na kiutamaduni, fursa za kiuchumi, na kijamii, kutanua wigo na mitandao ya kibiashara kwa bidhaa zinazozalishwa nchini hususani bidhaa za utamaduni, sanaa, na ubunifu.
“Madhumuni ya tamasha hili ni pamoja na; kuenzi na kulinda utamaduni wetu, kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi kupitia ukuzaji wa sekta za ubunifu na utamaduni, kutoa jukwaa la kuonyesha utamaduni kama msukumo madhubuti wa utangamano wa kitaifa kwa kuwaleta/kuwaunganisha pamoja wadau na viongozi wa sekta.”
“Kuendeleza na kuenzi urithi wa utamaduni wetu, kutoa fursa ya majadiliano ya kitaaluma baina ya wananchi wa kila mkoa, kutumia utamaduni na ubunifu kama nyenzo ya kuenzi na kukuza utambulisho wa Taifa na kutangaza fursa na rasilimali za kipekee ilizonazo nchi yetu.”amesema.
Aidha ameongeza kuwa Tamasha la mwaka huu litakuwa na vionjo mahsusi kama vile mirindimo ya kiasili, kuanzia mavazi, maonesho, visasili na visakale.
“Tamasha litakuwa na mdahalo wa kitaifa utakaozungumzia mapambano dhidi ya viashiria vya mmomonyoko wa maadili na nini mchango wa jamii katika kupunguza na hatimaye kuondoa viashirika hivyo,”amesema
Hata hivyo ameeleza kuwa Tamasha litakuwa na onesho maalumu la matumizi ya kanga ikiwa ni vazi la utamaduni wa Mtanzania na zaidi ya vikundi 25 kutoka Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar; vikundi hivyo ni vya sanaa ya asili, ubunifu, utamaduni na mziki wa kizazi kipya.
Pia Tamasha litakuwa na mashindano ya uhifadhi wa ngoma za asili kwa vikundi 25 vya Tanzania Bara na visiwani pamoja na kliniki ya Sekta ya Utamaduni, Sanaa na Michezo
Kutokana na umuhimu na mvuto wa tamasha hilo, ameomba kampuni zote, mashirika, asasi na taasisi zinazotoa huduma mbalimbali, washirika wa maendeleo na wadau kwa ujumla kujitokeza kudhamini tamasha hilo.
Msigwa amesema kuwa Rais Samia ametoa maelekezo mahususi ya kufungamanisha utamaduni na utalii, utamaduni na biashara, utamaduni na uchumi kwa ujumla.
“Kwa ujumla, tamasha hili ni fursa muhimu katika nyanja za kiuchumi, kijamii, kisayansi, kisiasa na kiutamaduni. Aidha, ni njia mahususi ya kukuza viwanda vya ubunifu sanaa na utamaduni nchini.
Tamasha linaandaliwa katika namna ya kuzitangaza tunu zetu, vivutio vyetu vya kiutamaduni, tunaomba sana ushirikiano wa watanzania wote,”ameeleza.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...