WAKALA wa Nishati Vijijini (REA) umeanza kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha kila Mwananchi anatumia Nishati Safi ya Kupikia.

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy amesema hayo Jijini Dar es Salaam Septemba 08, 2024 wakati wa uzinduzi wa Kipindi maalum cha Pika Kijanja na Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan maarufu kama Azimio la Kizimkazi.

“Mhe. Rais wakati anazindua Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia 2024-2034 Mwezi Mei mwaka huu alitoa maagizo maalum kwa REA; kwakuwa tumefanya vizuri katika kusambaza umeme vijijini huku nako kwa kushirikiana na wadau wengine tuhakikishe asilimia 80 ya Watanzania wanatumia Nishati Safi za Kupikia ifikapo mwaka 2034,” alisema Mhandisi Saidy.

Mhandisi Saidy alibainisha kuwa Wakala umeanza kutekeleza maelekezo ya Mhe. Rais kwa namna mbalimbali ikiwemo kuhamasisha wananchi kutumia Nishati Safi za Kupikia kwa kuondokana na fikra kuwa bidhaa za Nishati Safi ni ghali ama si salama na kwamba chakula kinachopikwa kwa Nishati Safi hakina ladha.

“Tunaendelea kuwakumbusha na kuwaelimisha wananchi kwamba suala la ladha ya chakula linategemea umahiri wa mpishi ama viungo vinavyotumika na sio nishati inayotumika kupikia,” alisema Mhandisi Saidy

Mhandisi Saidy alisema Wakala unaendelea kuwezesha upatikanaji wa Nishati Safi za Kupikia kwa kushirikiana na watoa huduma ambapo REA inawapa fursa watoa huduma kujitangaza ili kuwezesha wananchi wengi kufahamu uwepo wa teknolojia rafiki za nishati safi za kupikia.

Alibainisha kuwa Serikali kupitia REA inatoa ruzuku ili kuwezesha wananchi wamudu kununua bidhaa za Nishati Safi za Kupikia na kujionea ubora wa bidhaa hizo kwa lengo la kuendelea kuhamasisha wananchi wengi wahame kutoka kwenye kutumia nishati zisizokuwa salama.

“Serikali imetoa ruzuku ili kila mwananchi aweze kumudu gharama; Mathalan kwenye mitungi ya gesi (LPG) na vichomeo vyake Serikali kupitia REA imeidhinisha kiasi cha Shilingi Bilioni 10 kitumike kusambaza Mitungi ya Gesi ya kilo 6 itakayonufaisha watanzania wapatao 452,445 kwa bei ya ruzuku,” alifafanua.

Mhandisi Saidy alibainisha kuwa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alielekeza taasisi zote zinazohudumia watu zaidi ya mia moja zianze kutumia Nishati Safi za Kupikia na kwamba katika utekelezaji wake, REA imeandaa miradi ya kufikisha bidhaa na teknolojia za Nishati Safi za Kupikia kwenye taasisi hizo.

“Tunatekeleza agizo la Mhe. Rais na tumeanza na Magereza wao wana maeneo 211 tutakayoyafikishia Nishati Safi za Kupikia pamoja na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwenye Kambi 22 na Shule kongwe zipatazo 52; kwa kifupi kila taasisi yenye watu zaidi ya mia itafikiwa,” alisema Mhandisi Saidy.

Sambamba na hilo, Mhandisi Saidy alisema REA inafanya kazi kwa kushirikiana na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ambalo linazalisha mkaa rafiki na kwamba REA inakwenda kuiwezesha STAMICO kununua mashine tatu za kuzalisha mkaa rafiki ili iweze kufikisha huduma kwenye maeneo mengi zaidi.

Aidha, Mhandisi Saidy alisema REA hadi sasa imefanya vizuri kwenye suala zima la kusambaza umeme vijijini ambapo hadi sasa utekelezaji umefika asilimia 99 na kwamba nguvu iliyotumika kusambaza umeme itatumika pia katika kuhakikisha wananchi wote wanapata Nishati Safi za Kupikia.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...