Dodoma Jumanne 10 September 2024 Ndondo Cup 2024 mjini Dodoma ilianza mwishoni mwa wiki, ikiangazia dhamira thabiti ya Serikali ya Marekani ya kuunganisha michezo na mipango muhimu ya afya inayolenga kupambana na VVU na kukuza chanjo miongoni mwa vijana wa Tanzania. Ikiongozwa na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) na Mfuko wa Dharura wa Raisi wa Marekani wa Kupambana na Ukimwi (PEPFAR) kupitia mradi wa Breakthrough ACTION, mashindano haya ya soka ya ngazi ya chini yanavuka mipaka ya matukio ya jadi ya michezo, yakitumika kama jukwaa lenye nguvu la elimu ya afya na ushirikishwaji wa jamii.

Kutokana na mafanikio makubwa yaliyopatikana kutoka kwa matukio ya awali ya Ndondo Cup yaliyofanyika Dar es Salaam, Iringa, Mbeya, Mwanza, na Ruvuma—ambapo makumi ya maelfu walipata huduma muhimu za afya—mashindano ya mwaka huu yanalenga kuongeza ushawishi wake kupitia kampeni ya vijana ya ‘SITETEREKI’ na mpango wa chanjo wa ‘Kuwa Bingwa’. Mipango hii inaweka kipaumbele kwenye kutoa huduma za afya zinazoweza kufikiwa kwa urahisi katika mazingira yenye uhai na kuvutia ambayo yanaeleweka na vijana.

Mwakilishi wa USAID, Moses Bateganya, alisisitiza ushirikiano kati ya michezo na afya. "Tumejizatiti kuanzisha mbinu za ubunifu zinazotoa matokeo halisi ya afya. Tunaamini kwamba michezo inaweza kuwa nguvu kubwa katika kuleta na kukuza mabadiliko chanya ya tabia na kuboresha upatikanaji wa huduma, na tunafurahi kushirikiana na Ndondo Cup na Serikali ya Tanzania kuleta mpango huu katika uhalisia."

Evangelina Chihoma kutoka mfuko wa PEPFAR alisisitiza umuhimu wa kuwafikia vijana, akiangazia takwimu za utafiti uliofanyika hivi karibuni ukionyesha kuna haja kubwa ya kufikia vijana na elimu huduma za VVU. “Mfuko wa PEPFAR unaendelea kujidhatiti kupambana na VVU Tanzania” alisema. “Lengo letu ni kufikia vijana kwa njia mabli mbali za kibunifu kama kombe la Ndondo”.

Kampeni ya ‘SITETEREKI’ inalenga hasa vijana wenye umri wa miaka 15-24, ikiwawezesha kuchukua jukumu la afya zao. Washiriki wanaweza kupata taarifa muhimu kuhusu VVU, kupima, kupata kinga kabla ya maambukizi (PrEP), tiba ya kufubaza virusi vya ukimwi yaani antiretroviral (ART) iwapo wamepimwa na kupatikana na VVU, na kondomu—yote haya wakifurahia msisimko wa mashindano. Wakati huo huo, mpango wa ‘Kuwa Bingwa’ unahimiza wanaume kuweka kipaumbele kwenye chanjo, huku huduma za chanjo zikifikika kwa urahisi kwenye uwanja wa michezo, zikiimarisha umuhimu wa afya kwao na familia zao.

Baadhi ya mashabiki wameelezea jinsi Ndondo ya mwaka huu ilivyompa mtazamo chanya juu ya afya. Kwa mfano, Amani, kijana wa miaka 19 kutoka Dodoma, alisema, "Mashindano haya yamenifungua macho kuhusu umuhimu wa kujua hali yangu ya VVU. Nimepima VVU, na sasa najua hali yangu. Nilihisi kuungwa mkono na kuwezeshwa kuchukua hatua juu ya afya yangu huku nikifurahia na marafiki zangu."

Katika wiki zijazo, Ndondo Cup itaenea katika mikoa mipya, ikiwa ni pamoja na Pwani na Kagera, ikipanua wigo wa mpango huu na athari zake. Mchanganyiko huu wa kipekee wa michezo na afya unakuza mazungumzo ya maana kuhusu hatari za kiafya, kukubalika, na kukuza tabia chanya, hatimaye kuongeza matumizi ya huduma za afya miongoni mwa vijana.

Ndondo Cup ni ushahidi wa imani ya Serikali ya Marekani katika uwezo wa michezo kuleta mabadiliko ya kijamii. Tukio hili linaonekana kama ishara ya matumaini, likionyesha jinsi mikakati inayotegemea jamii inavyoweza kupambana na VVU na kuboresha afya ya umma nchini Tanzania, na kuwawezesha vijana wa taifa kwa maisha yenye afya bora.

Mwakilishi wa USAID Moses Bateganya wa pili kushoto akimkabidhi zawadi mchezaji Kassim Hussein ambaye alitangazwa mchezaji bora kwenye mechi ya ufunguzi wa mashindano ya Ndondo Cup Dodoma, mechi iliyochezwa baina ya Kikuyu FC na Nkuhungu Terminal FC. Huku ikiongozwa na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) na Mfuko wa Dharura wa Raisi wa Marekani wa Kupambana na Ukimwi (PEPFAR) kupitia mradi wa Breakthrough ACTION, mashindano haya ya soka ya ngazi ya chini yanavuka mipaka ya matukio ya jadi ya michezo, yakitumika kama jukwaa lenye nguvu la elimu ya afya na ushirikishwaji wa jamii.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...