Na Mwandishi Wetu Michuzi TV Dodoma
Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) na Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS), leo tarehe 23 Septemba 2024, wamesaini makubaliano ya kutoa elimu ya ufundi stadi kwa vijana kuanzia miaka 15 mpaka 24, ikiwa ni juhudi za kuwaokoa na vishawishi vinavyoweza kuwasababishia kupata maambukizi ya virusi vya UKIMWI
Makubaliano hayo yamesainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS, Dkt. Jerome Kamwela katika Ukumbi wa Mikutano wa VETA Makao Makuu, jijini Dodoma.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS, Dkt. Jerome Kamwela amesema vijana wengi kati ya miaka 15 mpaka 24 wanakumbwa na kichocheo cha maambukizi ya ukimwi kutokana na kukosa mbinu za kujiajiri na hivyo kuwa katika hatari ya kupata maambukizi ya UKIMWI.
Amesema, kwa kutambua changamoto, TACAIDS imeona ni vyema kushirikiana na VETA ili kuwapatia vijana wa rika hilo ujuzi ambao utawawezesha kujiajiri au kuajiriwa, hivyo kuepukana na vishawishi vinavyosababishwa na kukaa mtaani bila kazi.
Amesema ushirikiano huo, utadumu kwa kipindi cha miaka mitatu (3) kuanzia Septemba 2024 hadi 30 Desemba 2026, ambapo TACAIDS itawatambua vijana kupitia halmashauri za wilaya na kuwasajili kwenye vyuo vya VETA katika maeneo yao ili waweze kupatiwa ujuzi mbalimbali.
“Kwa kuwapa elimu na ujuzi wa ufundi stadi, wataweza kujiajiri na kupata kipato na kuondoa utegemezi na hatimaye maambukizi ya Ukimwi yatapungua kwa kiwango kikubwa. Tutapunguza maambukizi mapya yanayowapata vijana hasa wale ambao wapo nje ya mfumo wa elimu,” Dkt. Kamwela ameseama.
Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, amesema ushirikiano huo, utawezesha vijana wa Kitanzania kupata ujuzi wa shughuli mbalimbali za kiuchumi, hivyo kujipatia kipato na kujiepusha na maambukizi ya UKIMWI.
“Nina imani kupitia makubaliano haya tutaongeza vijana watakaojishughulisha katika shughuli za kiuchumi ambapo pato la mtu binafsi na taifa litaongezeka,” CPA Kasore ameongeza.
Amesema VETA imepokea kwa mikono miwili wazo la ushirikiano kutoka TACAIDS kwa kuwa limegusa majukumu yake ya msingi ya kutoka mafunzo kwa vijana kwa nia ya kuwakwamua kiuchumi na kijamii.
Ameongeza kuwa kundi lengwa la vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24 ndilo lililotawala miongoni mwa wanafunzi walio katika vyuo vya VETA.
Mkurugenzi Mkuu wa VETA CPA Anthony Kasore na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS Dkt. Jerome Kamwela wakisaini makubaliano ya kutoa elimu ya ufundi stadi kwa vijana kuanzia miaka 15 hadi 24 yaliyofanyika Jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mkuu wa VETA CPA Anthony Kasore na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS Dkt. Jerome Kamwela wakishikana mkono mara baada ya kusaini makubaliano ya kutoa elimu ya ufundi stadi kwa vijana kuanzia miaka 15 hadi 24 yaliyofanyika Jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mkuu wa VETA CPA Anthony Kasore na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS Dkt. Jerome Kamwela na baadhi ya watendaji wa VETA na TACAIDS wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kusaini makubaliano ya kutoa elimu ya ufundi stadi kwa vijana kuanzia miaka 15 hadi 24 yaliyofanyika Jijini Dodoma.
Watendaji wa VETA na TACAIDS wakionesha mkataba wa makubaliano ya kutoa elimu ya Ukimwi ,Jijini Dodoma.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...