Mkurugenzi wa Sheria wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wanawake Katika Usafiri wa Anga Tanzania Maria Makalla Memba akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kuzindua shindano la ubunifu wa nembo ya jukwaa hilo kwa wasichana wenye umri kati ya miaka 14 hadi 20 Tanzania nzima pamoja na mkutano wa wanawake viongozi wanaohudumu katika sekta ya usafiri wa anga nchini unaotarajiwa kufanyika siku hiyo ya Oktoba 31 jijini Dar es Salaam.
JUKWAA la Wanawake katika Usafiri wa Anga Tanzania linatarajia kufanya mkutano wake wa kwanza wa viongozi wanawake katika sekta ya usafiri wa anga utakaofanyika tarehe 31 Oktoba 2024 jijini Dar es Salaam mara baada ya kuzinduliwa rasmi mwaka 2023 na Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa maadhimisho ya miaka 20 ya kuanzishwa kwa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA).
Akizungumza na waandishi wa habari Mkurugenzi wa Sheria wa TCAA ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wanawake katika Usafiri wa Anga Tanzania, Maria Makalla Memba amesema jukwaa hilo limezindua shindano la ubunifu wa nembo ya jukwaa hilo kwa wasichana wa umri wa miaka 14 hadi 20 Tanzania nzima ambalo mshindi wake atatangazwa Oktoba 31 mwaka huu unaenda sambamba na mkutano wa wanawake viongozi wanaohudumu katika sekta ya usafiri wa anga nchini unaotarajiwa kufanyika siku hiyo ya Oktoba 31 jijini Dar es Salaam.
“Mkutano huu utahusisha marubani, wahandisi wa ndege na mitambo ya ndege, waongoza ndege, wahudumu wa ndege, maafisa usalama katika sekta ya anga na kila mmoja ambaye kwa taaluma yake anahudumia sekta ya anga kwa lengo la kuelezana mafanikio, changamoto, fursa pamoja na tija zilizopo kwenye sekta ya usafiri wa anga”. Amesema Memba
Mkutano huo ambao Jukwaa la Wanawake Katika Usafiri wa Anga litaufanya kwa mara ya kwanza utahusisha wanawake viongozi kwenye sekta hiyo na kufuatiwa na mkutano mwingine utakaohusisha wanataaluma wengi zaidi wakiwemo wenye nafasi za chini kwenye usafiri wa anga hivyo jukwaa hilo linalenga kusisimua jamii hususani wanawake na watoto wa kike kusoma masomo ya sayansi ili kujiunga na sekta hiyo ya anga.
Jukwaa hilo tayari limefungua fursa ya kujiandikisha kwa washiriki wa mkutano huo kupitia kiunganishi cha mtandaoni kilichopo kwenye tovuti ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) huku washindani wa shindano la ubunifu wa nembo ya jukwaa hilo wakitakiwa kuwasilisha kazi zao kupitia anuani ya posta ya mamlaka hiyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...