Kilimanjaro. Bw. Nehemiah Mchechu, Msajili wa Hazina na kiongozi anayejulikana kwa mchango wake mkubwa katika sekta ya nyumba, benki, na biashara, ameendesha harambe iliyowezesha kuchangisha Sh117.8 milioni kwaajili ya kuendeleza ujenzi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Naibili, Siha, Kilimanjaro.
Kati ya fedha hizo kwaajili ya jengo hilo mpya la ibada ambalo ujenzi wake ulianza miaka sita iliyopita, Sh50.2 milioni ni taslimu, Sh66.5 ni ahadi na Sh1.1 zilipatikana kwa njia ya mnada.
Katika harambe hiyo iliyofanyika Jumapili (Oktoba 20, 2024), pia ilipatikana mifuko 118 ya saruji.
Pesa hizo na saruji ni kwaajili ya upauzi wa jengo hilo la ibada na kazi ya plasta, kwa mujibu wa Askofu Dr. Fredrick Shoo, mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini ya KKKT.
Kazi hizo mbili za upauzi na plasta, zinatarajiwa kugharimu kiasi cha Sh150 milioni.
Akizungumza na viongozi wa kidini, serikali na kijamii, pamoja na waumini wa Naibili, Bw. Mchechu alieleza haja ya kuendelea kuwa na moyo wa kutoa na kushirikiana mpaka ujenzi wa nyumba hiyo ya ibada utakapokamilika.
Kwa sasa tayari jiwe la pembe limewekwa katika kanisa hilo.
Bw. Mchechu aliwataka wakristo kutoishia kwenye hatua hiyo ya kuweka Jiwe la Pembe tu.
“Tunapoendelea na ujenzi huu, nataka niwaombe ninyi wapendwa msiishie hapa. Tuendelee kufanya kazi kwa pamoja mpaka ujenzi utakapokamilika,” alisema.
Aliongeza: “Kanisa bado linahitaji michango yenu, maombi yenu, na utayari wenu wa kujitoa. Kila mmoja wetu anaweza kutoa kitu, iwe ni fedha, muda, au huduma kwa namna yoyote ile.”
Alisema ikiwa watatoa kwa moyo wa upendo, Mungu atarudisha zaidi na zaidi na vikombe vyao vitafurika.
Bw. Mchechu alisisitiza kwa kunukuu Biblia katika Luka 6:38: "Wapeni watu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa, cha kusukwasukwa, na kushindiliwa, na kufurika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu."
Aliongeza: “Kama vile Nehemia alivyowaongoza watu wa Yerusalemu kujenga tena ukuta wa mji baada ya kuharibiwa, ninyi pia muendelee kujitoa kwa uaminifu na bidii katika ujenzi wa nyumba ya Mungu.”
Kwa upande wa Dr. Shoo, alisema matamanio yao ni kuona wanakamilisha plasta, kuweka madirisha, milango na madhabahu, kupaka rangi na kuanza maandalizi ya kutengeneza samani, ifikapo mwaka 2026.
Mpaka kufikia hatua ya kabla ya upauzi, jumla ya kiasi cha Sh229.8 milioni kimetumika, shukrani kwa watu wenye mapenzi mema na Mungu kwa michango yao.
Askofu Shoo alisema baada ya upauzi na plasta, awamu ya pili ni kujenga madhabahu na madirisha na milango ya mbao.
Baada ya hapo awamu inayofuata itakuwa kuweka tarazo, bodi ya dari, kusuka umeme na rangi, huku awamu ya nne ikiwa ni kuweka viti na kumalizia madhabahu kwa kutumia mbao.
Awamu ya mwisho itakuwa ni kufunga vifaa vya muziki, mifumo ya CCTV Kamera, kiyoyozi na mfumo wa TEHAMA.
“Ni wakati mwafaka wa kushirikiana kufanya kazi hii ya baraka iliyopo mbele yetu. Mungu atutie nguvu” alihitimisha Askofu Shoo.
Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu akizungumza katika harambee kw aajili ya kuendeleza ujenzi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Naibili, Siha, Kilimanjaro.
Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu akijadiliana na Askofu Dkt.Fredrick Shoo wakati akiwa katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Naibili, Siha, Kilimanjaro.
Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu akipata ukarabisho mara baada ya kufika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Naibili, Siha, Kilimanjaro.
Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu akisalimiana na Asofu wa KKKT Dkt Fredrick Shoo wakati alipokwenda katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Naibili, Siha, Kilimanjaro.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...