Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Bank of Africa Tanzania , Nandi Mwiyombella akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi msaada wa hundi yenye thamani ya shilingi milioni 10 zilizotolewa na benki kusaidia mpango wa "Rafiki wa Amana" unaolenga kuboresha huduma za afya kwenye hospitali ya Rufaa ya Amana iliyopo jijini Dar es Salaam.pichani kushoto kwake ni Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt. Bryceson L. Kiwelu . Wengine pichani ni Maofisa Waandamizi kutoka BOA na hospitali ya Amana.
Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Bank of Africa Tanzania , Nandi Mwiyombella (wa pili kutoka kulia) akimkabidhi mfano wa hundi ya shilingi milioni 10 Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Amana, Dkt. Bryceson Kiwelu (wa pili kushoto), zilizotolewa na benki hiyo kusaidia mpango wa "Rafiki wa Amana" unaolenga kuboresha huduma za afya kwenye hospitali hiyo.
*Yachangia mpango wa “Rafiki wa Amana"unaolenga kuboresha huduma hospitali ya Rufaa ya Amana
BANK of Africa Tanzania imeeleza dhamira yake ya kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika maeneo ya afya, elimu na uhifadhi wa mazingira kama sehemu ya juhudi za benki hiyo katika kukuza maendeleo ya kijamii na kiuchumi hapa nchini.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi hundi ya shilingi 10 milioni kwa Hospitali ya Rufaa ya Amana iliyopo jijini Dar es Salaam kusaidia mpango wa "Rafiki wa Amana" , Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Bank of Africa Tanzania , Nandi Mwiyombella , kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, Esther Maruma alisema kwamba benki hiyo ni sehemu ya jamii.
"Kwetu Bank of Africa Tanzania , tunatambua kwamba jamii yenye ustawi ndiyo msingi wa jamii yenye mafanikio. Hii inaenda sambamba na ajenda yetu endelevu inayolenga katika kukuza jamii bora katika maeneo ambayo tunafanyia biashara zetu”
"Hii ni fursa pekee kwetu kusaidia Hospitali ya Rufaa ya Amana na kuchangia katika kuboresha huduma za afya kwa akina mama na watoto," alisema Mwiyombella.
Alisisitiza dhamira ya benki hiyo ya kusaidia sekta ya afya nchini Tanzania na kuboresha ustawi wa jamii kupitia kuchangia sekta zenye kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii .
Aliongeza kusema kwamba Bank of AfricaTanzania na Hospitali ya Rufaa ya Amana zina uhusiano wa muda mrefu wa ushirikiano katika maeneo mbalimbali ya kimkakati ambayo yanatoa fursa kwa benki hiyo kusaidia mpango wa "Rafiki wa Amana." unalenga kukusanya fedha kwa ajili ya ukarabati, upanuzi, na kuweka vifaa katika wodi ya akina mama na watoto katika hospitali hiyo, ambayo inatoa huduma muhimu za afya mkoani Dar es Salaam.
"Lengo letu ni kuona kila Mtanzania anapata huduma bora za afya na kuwa katika mazingira bora, kuokoa akina mama na watoto ni kuokoa taifa la kesho," alisema, Mwiyombella.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospital hiyo, Dkt. Bryceson L. Kiwelu, alishukuru benki hiyo kwa kuendelea kutoa msaada kwenye hospitali hiyo kwa muda mrefu. "Tunashukuru sana kwa msaada usiotetereka kutoka Bank of Africa Tanzania. Ukarimu wenu unasaidia katika juhudi zetu za kupanua na kuimarisha vifaa vyetu, kuhakikisha huduma bora kwa akina mama na watoto nchini," alisisitiza Dkt. Kiwelu.
Alisema hospitali hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo miundombinu kwa sababu ilijengwa zaid ya miaka 70 iliyopita, ingawa serikali imeendelea kuiwezesha kwa vifaa tiba kama vile CT scan, x-ray za kidijitali na vifaa vingine vya kisasa.
Naye Mkuu wa huduma za kibenki kwa wateja wadogo (Retal Banking) wa benki hiyo, Mwamvua Majeshi, alieleza huduma mbalimbali wanazozitoa hapa hapa nchini ni mikopo ya nyumba, mikopo ya binafsi, huduma za hisa na huduma za akaunti za watoto ambazo zinalenga kuwakwamua watanzania kutoka kwenye umasikini.
Mpango wa "Rafiki wa Amana" ni ushahidi wa jitihada za pamoja zinazohitajika kuboresha miundombinu ya afya, kuifanya iweze kupatikana na kufanikiwa kwa wale wanaohitaji zaidi. Mchango wa Bank of Africa ni sehemu ya juhudi zake kubwa za kijamii zinazolenga kukuza afya, elimu, na ustawi wa kijamii katika jamii inayohudumia.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...