Na Mwandishi Wetu.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa FCC William Erio siku ya Ijumaa Novemba 29, 2024 katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi za taasisi hiyo mkoani Dar es Salaam,
Katika mikakati ya kutoa elimu ni pamoja na FCC kuzindua Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Ushindani Duniani ambayo kilele chake kitakuwa tarehe 8 Desemba, 2024.
Amesema ili biashara ifanyike inahitaji kuwa na mazingira ya haki na usawa na umuhimu kuwa na udhibiti kupitia sera na sheria akiwemo mikataba yote inayokinzana katika kufanya ushindani, na miungano yote ya kampuni ambayo inafifisha ushindani.
Hata hivyo Erio amesema licha ya nchi kuwa na misingi ya biashara huria, kuna utofauti wa rasilimali kutoka kwa wafanyabiashara ambapo wakifanya biashara katika misingi hiyo bila utaratibu wa aina yoyote, watu au kampuni zitaumia kwa kushindwa kupata fursa sawa ya kufanya biashara.
"Mbinu nyingi chafu zinaweza kutumika kwenye utendaji wa biashara, mfano wafanyabiashara kuwaondoa washindani wao sokoni ili wabaki peke yao, kwasababu mfanyabiashara yeyote lengo lake ni kupata faida, sasa mkiwa wengi faida itapungua ingawa ufanisi na upatikanaji wa bidhaa utaongezeka, kwahiyo anaweza kuamua kwa makusudi kabisa kufanya vitu ambavyo vinafifisha ushindani na kwa nguvu yake aliyonayo aidha ya kifedha, rasilimali watu au utaalamu akawasababisha wengine wakashindwa kufanya biashara sokoni na kuondoka", ameeleza.
Amesema changamoto zote hizo zinatokana na kutokuwa na usawa kwa wafanyabiashara hao hivyo amesema kama taasisi jukumu la FCC ni kutengeneza mazingira sawia ya watu wote kufanya biashara kwa usawa kupitia sera na sheria.
Kilele cha maadhimisho hayo kitafanyika tarehe 5 Disemba 2024 katika Hoteli ya Golden Tulip, Oysterbay, Dar es Salaam ambapo Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo anatarajiwa kuwa mgeni rasmi. Kilele hicho kitaambatana na kongamano litakalowakutanisha magwiji wa sheria na biashara ambao watajadili mazingira ya biashara na ushindani Tanzania na watapata fursa ya kuishauri FCC juu ya namna nzuri ya kutekeleza majukumu yake.
Maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Ushindani Duniani, kaulimbiu 'Sera ya Ushindani na Kudhibiti Kukosekana kwa Usawa katika Uchumi'.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...