Na Mwandishi wetu, Mirerani
MWENYEKITI mpya wa wachimbaji wa madini Mkoani Manyara (MAREMA) Elisha Nelson Mnyawi, amesema wachimbaji wanakabiliwa na ukosefu wa mitaji ya kuendesha shughuli zao uchimbaji hali inayosababisha waendelee kuwa masikini licha ya kuzungukwa na utajiri mkubwa wa madini mbalimbali.

Mwenyekiti huyo mpya wa MAREMA Elisha Nelson Mnyawi ameyasema hayo akizungumza mji mdogo wa Mirerani wakati wa makabidhiano rasmi ya ofisi amesema ukosefu wa mitaji ni changamoto kubwa ya wachimbaji.

Mnyawi amesema japokuwa mkoa huo una utajiri mkubwa wa madini mbalimbali ila wachimbaji wake wameendelea kuwa masikini kutokana na ukosefu wa mitaji ya kuchimbia.

“Nikiambiwa nitaje changamoto kubwa ya wachimbaji madini wa mkoa wa Manyara, nitazungumzia kuwa namba moja ni mtaji, namba mbili ni mtaji na namba tatu ni mtaji,” amesema Mnyawi.

Amesema wachimbaji wadogo wanahangaikia mitaji na kutokana na mazingira magumu ya leseni zao imekuwa vigumu kukopesheka kupitia taasisi za fedha ikiwemo benki.

“Chama chetu cha wachimbaji kimekuwa na ukata mkubwa kwa kutokuwa na vyanzo vya mapato, zaidi ya kutegemea michango kutoka kwa wahisani na wadau,” amesema Mnyawi.

Amesema yeye na viongozi wenzake wamelenga kurekebisha rasimu ya katiba ya MAREMA ili waweze kufungua miradi mbalimbali ya maendeleo kwa manufaa ya wachimbaji.

Hata hivyo, mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Gracian Max Makota amewatoa hofu wachimbaji hao kwa kueleza kuwa hivi sasa taasisi za fedha ikiwemo mabenki yanatoa mikopo kwa wachimbaji.

Makota amesema mabenki yameona umuhimu wa kuwapa mikopo wachimbaji wadogo wa madini hivyo mjipange ili muweze kukopa na kufanya shughuli za uchimbaji ipasavyo.

"Tena mna Mwenyekiti mtanashati mwenye muonekano wa kiungwana anayevaa suti bila kutoka jasho nina amini atawavusha na kuwapeleka eneo zuri wachimbaji," amesema Makota.

Mwenyekiti mstaafu wa MAREMA, Justin Nyari amesema ana uhakika chama hicho kitapiga hatua kwani kiongozi wake wa sasa Elisha Mnyawi ni kijana mwenye maono, dira na mtazamo wenye kuona mbali.

“Sisi tumeifikisha Marema hapa ilipo na kupitia uongozi wa Mnyawi nina uhakika mtapiga hatua kubwa na kuendeleza mazuri tuliyoyafanya kwa kuwafikisha wachimbaji mbali zaidi," amesema Nyari.

Makamu Mwenyekiti wa MAREMA, Money Yusuf amesema wachimbaji madini wanapaswa kuendelea kuwa pamoja ili washirikiane na kuanzisha mfuko wao utakaowanyanyua.

“Mkiweka mitaji kwenye mfuko wenu mtaweza kukopesheka kwenye mabenki kupitia fedha zetu na kuweza kufanya shughuli zenu wenyewe ikiwemo kununua mitambo ya uchimbaji,” amesema.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...