Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefanya mageuzi makubwa katika Sekta ya Afya kwa kuboresha huduma za Afya ikiwemo vifaa tiba na kuendelea kuwasomesha wafanya kazi ili kuweza kuwa na wataalamu bingwa na bingwa ubobezi watakaotoa huduma bora za Afya kwa wananchi wote wa Mijini na Vijijini.

Hayo yamesemwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla katika ufunguzi wa Mkutano wa majadiliano wa wadau wa maendeleo kuhusu ugharamiaji wa huduma za Afya Zanzibar kwa lengo la kufikia adhma ya Afya bora kwa wote uliofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege jijini Zanzibar.

Amesema kuwa katika kuhakikisha Serikali inatoa huduma bora za Afya kwa waanchi wote imeamua kufanya uwekezaji mkubwa wa miundombinu ya Afya ikiwemo kujenga Hospital kumi(10) kila wilaya pamoja na kuweza kuweka wataalamu bingwa na bingwa bobezi ili kuimarisha huduma bora za afya kwa wananchi wote.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema ili kuweza kufikia adhma ya Afya kwa wote Serikali imeimarisha hali ya upatikanaji wa dawa nchini, upatikanaji wa chakula kwa wagonjwa sambamba na kuongeza wigo wa utoaji wa matibabu kwa wananchi kama vile huduma ya usafishaji wa figo(DIALYSIS) ambapo kabla wananchi walilazimika kutumia gharama kubwa za matibabu hayo na wengine kupoteza maisha kutokana na kukosa fedha za kugharamia huduma hio.

Mhe. Hemed amesema kuwa Serikali imeimarisha vifaa vya uchunguzi ikiwemo XRAY, CT-SCAN, MRI, ULTRA SOUND na vifaa mbali mbali vya maabara pamoja na kuboresha vifaa tiba kwa kujengwa mitambo miwili (2) ya Hewa Tiba (OXYGEN PLANTS) katika hospital ya Mkoa wa Mjini Magharibi - Lumumba ambayo itatumika katika hospital mbali mbali za Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira Bora ya Afya kwa kuajiri wafanyakazi wapya 1,566 kwa mwaka wa fedha 2024/2025, kujenga hospitali za Mkoa, hospital ya Rufaa ya Binguni pamoja na kutoa fursa kwa wafanyakazi wa Afya kujiendeleza kielimi na kuwajengea uwezo madaktari bingwa na binga bobezi kuweza kuleta ilufanisi zaidi katika itoaji huduma za Afya kwa wananchi.

Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema katika kutatua chamgamoto mbali mbali, Serikali inaendelea kufanya mageuzi katika mfumo wa kugharamia huduma za Afya ikiwemo kuanzisha Mfumo wa Huduma za Afya Zanzibar chini ya Sheria namba 1 ya mwaka 2023 na kupewa jukumu la kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za Afya kwa wananchi wote wanaoishi Zanzibar.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Afya, Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Hassan Khamis Hafidh amesema lengo la kuwepo kwa Mkutano wa ugharamiaji wa huduma za Afya Zanzibar ni kufanya majadiliano ya pamoja kati ya watendaji wa Wizara ya Afya, washirika wa maendeleo na wadau wa Afya ili kupata njia mbadala za kitaalamu ambazo zitaiwezesha Serikali kupitia Wizara ya Afya kuweza kugharamia huduma za matibabu kwa wananchi wote wa zanzibar.

Mhe. Hafidh amesema gharama za huduma ya matibabu duniani zimekuwa zikipanda siku hadi siku jambo linalopelekea wananchi wengi kutomudu kuchangia huduma hio pale inapobidi hivyo Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar imeona ipo haja ya kukaa pamoja na wadau wa maendeelo ili kutafuta namna bora itakayosaidia kupunguza changamoto hio na kuhakikisha kila Mzanzibari anaweza kupata huduma bora za matibabu bila ya malipo yoyote.

Aidha Mhe. Hafidh amewashukuru washirika wa maendeleo wakiwemo Pharm Access, W.H.O na wengineo ambao wamekuwa mstari wa mbele kwa kushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Afya katika kuhakikisha inatoa huduma bora za Afya kwa wananchi wote wa Zanzibar.

Kwa upande wao Pharm Access na W.H.O ambao wamekuwa washirika wakubwa wa maendeleo katika Sekta ya Afya wamesema kufanyika kwa Mkutano huo utakuwa ni chachu ya upatikanaji wa huduma bora za Afya na zenye usawa kwa wazanzibari wote bila ya malipo.

Wamesema upatikanaji wa huduma bora za Afya unategemea uwepo wa Sera, Mikakati madhubuti, rasilimali watu na rasilimali fedha hasa katika kufikia adhma ya Serikali ya Awamu ya Nane(8) inayolenga kugharamia huduma za matibabu kwa wananchi wake wote.

Imetolewa na Kitengo cha Habari ( OMPR )

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...