Na WAF - Dodoma

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel amesema Shilingi Trilioni 6.7 zilizotolewa na Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan zimechangia kuleta mageuzi makubwa ya upatikani wa huduma bora za afya ikiwemo matibabu ya kibingwa nchini.

Dkt. Mollel amesema hayo wakati akichangia hoja kwenye Kamati ya Mipango na Uwekezaji Novemba 07, 2024 bungeni jijini Dodoma.

“Uwekezaji wa kiasi cha Shilingi Trilioni 6.7 umeleta mabadiliko makubwa katika huduma za afya, hali ya ubora wa huduma za afya umeendelea kuimarika nchini na hospitali zote za rufaa sasa zimepata vifaa vya kisasa, ikiwemo CT Scan, huku hospitali za kanda zikifungwa mashine ya MRI, hatua inayomuweka Rais Samia katika rekodi za kihistoria,” amesema Dkt. Mollel.

Dkt. Mollel amesema kiwango cha vifo vya kina mama kimepungua kutoka 556 hadi 104, akieleza kuwa mafanikio hayo yanaonesha upunguzaji wa asilimia 81.2 katika vifo vya uzazi.

Ameongeza kuwa Serikali imepunguza vifo vya wagonjwa wa kansa kwa asilimia 78, kutokana na upatikanaji wa matibabu ya kisasa ndani ya nchi.

Dkt. Mollel ameeleza kuwa kwa sasa Watanzania wengi hawalazimiki kwenda nje ya nchi kutibiwa, tofauti na ilivyokuwa kipindi cha nyuma ambapo mgonjwa aliyetakiwa kwenda India kupata matibabu alihitaji zaidi ya milioni 100, lakini sasa gharama zimepungua hadi milioni 10, huku huduma hizo zikitolewa ndani ya Tanzania. Kutokana na maboresho haya, rufaa za matibabu nje ya nchi zimepungua kwa asilimia 97.

Aidha, Naibu Waziri huyo amesema kuwa vifaa vya kisasa kama PET CT Scan vimewekwa ili kugundua kansa mapema, hata ile inayoweza kuibuka miaka 10 ijayo. Mafanikio haya yamewezesha wagonjwa 10,931 kutoka nje ya Tanzania kufika nchini kwa ajili ya matibabu, jambo linalodhihirisha uwekezaji mzuri uliofanywa na Rais Dkt. Samia katika sekta ya afya.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...