Wadau wanaojishughulisha na matumizi ya kemikali Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya wamehimizwa kuzingatia Sheria na Kanuni za matumizi ya kemikali ili kuondokana na athari ambazo hujitokeza endapo kemikali hazitotumika kwa kuzingatia usalama.
Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mhe. Mbaraka Batenga alitoa wito huo wakati akifungua Mafunzo ya Usimamizi salama wa Kemikali kwa wadau wanaojihusisha na shughuli za kemikali katika mafunzo yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Ofisi ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini yaliyofanyika leo katika Hoteli ya Omary City iliyopo wilayani Chunya.
“Kemikali hutumika katika uchimbaji na uchakataji wa madini, hivyo kemikali hizi zinahitaji uangalifu katika kutumia, kutunza ili kuepuka kusababisha madhara mbalimbali kwa watumiaji, wauzaji, wanyama na mazingira,” alisema Mhe. Batenga.
Aidha, Mkuu wa Wilaya ameipongeza Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kuandaa mafunzo hayo ya usimamizi salama wa kemikali kwani uchimbaji wa madini huchangia ukuaji wa uchumi wa nchi, hivyo Mamlaka iendelee kutoa elimu ya kemikali kwani wadau wapo wengi.
Kwa upande wake Meneja wa Mamlaka, Ofisi ya Kanda za Nyanda za Juu Kusini, Elias Mulima amewataka wadau walioshiriki mafunzo ya usimamizi salama wa kemikali kuwa mabalozi kwa jamii lakini pia ametoa wito kwa wadau ambao hawakupata nafasi ya kushiriki mafunzo, kuwa mafunzo hayo ni endelevu hivyo wawe tayari kushiriki wakati Mamlaka itakapotangaza tena.
“Hii elimu tutaendelea kutoa mara kwa mara kwa wadau na kuhakikisha kwamba kemikali zinatumika vizuri na hazileti madhara kwa watumiaji wenyewe, lakini pia na jamii inayowazunguka, alisema Mulima.
Naye Omary Hamisi kutoka kampuni ya Small Scale Miners - Chunya, ameishukuru Mamlaka kwa kuwafikia na kuwapa elimu ya matumizi salama ya kemikali kwa sababu wamekutana na mambo mengi ya kigeni kwenye masuala ya matumizi ya kemikali ikiwemo kuzifahamu sheria, alama za kemikali, utunzaji na namna ya utumiaji wa kemikali hatarishi.
Meneja Mulima amesema kuwa mafunzo hayo siku mbili kuanzia Novemba 07-08, 2024 katika Mkoa wa Kimadini Chunya, yamelenga kujenga uelewa wa pamoja kwa wadau mbalimbali wanaoshughulika na matumizi ya kemikali kuhusu matumizi yaliyo salama ya kemikali kwa afya zao na Mazingira kwa ujumla.
Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kimadini Chunya, Eng. Laurent Mayale , akiongea kuwasalimu washiriki wa mafunzo ya Usimamizi wa Kemikali kwa wadau wanaojishughulisha na kemikali katika Mkoa wa Kimadini Chunya.
Mwenyekiti wa Wachimbaji madini Mkoa wa Mbeya, Saddam Kyando akitoa neno la shukrani kwa niaba ya washiriki wengine wa mafunzo wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya Usimamizi wa Kemikali kwa wadau wanaojishughulisha na kemikali katika Mkoa wa Kimadini Chunya
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...