Wanafunzi wa TASUBA wakiwakaribisha wageni kwa ngoma kabla ya mdahalo.

Mzee wa Mila wilayani Bwana Mwinyi Hashimu Akida akizungumza

Wadau wakisaini ahadi ya kukuza Urithi wa Utamaduni Usioshikika mjini Bagamoyo


Wadau wakifurahia ngoma



Na Mwandishi wetu, Bagamoyo


Wadau wanaofanya kazi za kudumisha Utamaduni wa Urithi Usioshikika wamesisitiza jamii kuendelea kuenzi michezo ya asili ili kutengeneza jamii ya watu wanaowajibika.


Michezo hiyo ukiwemo ule wa Baba na Mama inaaminika kuwa ilisaidia makuzi ya mtu kujua majukumu yake kama mwanaume na mwanamke.


Ushauri huo ulitolewa mjini Bagamoyo wakati wa mdahalo wa vijana uliolenga kuwajengea uwezo wa namna ya kukuza Urithi wa Utamaduni Usioshikika katika nyakati hizi za kidijitali


Akichangia mjadala huu, bwana Anthony Tiluganilwa mdau kutoka TASUBA alisema michezo ya asili ilikuwa inawafundisha kujitegemea kwani walicheza nje bila wazazi na hivyo kudumisha upendo na watoto wengine tofauti na sasa ambapo watoto wengi wanafungiwa magetini.


“ Tulipocheza kama Baba na Mama, mwanamke aliigiza majukumu ya mama na wa kiume aliigiza majukumu ya Baba. Jambo hili lilisaidia sana kwani hadi tumekua tunajua majukumu yetu. Kwa sasa hili halifanyiki matokeo yake tuna watu wabinafsi na wanaokwepa majukumu yao,” alisema Tiluganilwa.


Akichangia mjadala huo, mzee wa mila na mwenye ushawishi wilayani Bagamoyo bwana Hashimu Ally Kida alisisitiza umuhimu wa kukifundisha kizazi cha vijana ili kujua tulikotoka.


“Ni vema tukaongeza juhudi za kujadiliana ili kizazi chetu kijue mila zetu na desturi ili kujua tulikotoka katika tamaduni zetu,” alisisitiza Mzee Akida.


Kwa upande wake Angela Kidwanga, mwanafunzi wa TASUBA alisisitiza umuhimu wa wazazi kuwafundisha Watoto kujitegemea ili kukwepa vijana kupenda mashangazi ( Wanawake waliowazidi umri) na mabinti kutafuta sponsors ( wanaume watu wazima) badala ya kufanya kazi.


“ Naomba niwashauri wazazi pia wawe wanawapeleka Watoto kijijini walikotoka ili wajue mila na utamaduni wao kuliko kuwaacha mijini. Vilevile tunaomba watufundishe lugha zetu za asili badala ya kutumia Kiingereza tu,” alisema Kidwanga.


Urithi wa Utamaduni Usioshikika unajumuisha ujuzi na maarifa ya kiutamaduni katika jamii ikiwemo ujuzi wa kucheza ngoma za asili, kuandaa vyakula vya asili na namna ya kujieleza ikiwemo lugha ambapo inasemekana lugha nyingi za asili zipo hatarini kupotea kutokana na wazazi kushindwa kurithisha kwa watoto wao.


Majadiliano haya yaliandaliwa na UNESCO kwa kushirikiana na serikali ili kuchagiza urithishwaji wa utamaduni usioshikika na namna ambavyo unaweza kuchagiza ajira na kuongeza kipato hususani katika nyakati hizi za kidijitali.



















Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...