TAASISI ya Wanawake na Samia Mkoa wa Dar es Salaam, imesema Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ni miongoni mwa mafanikio makubwa ambayo Tanzania inajivunia inapoadhimisha miaka 63 ya  Uhuru wa Tanganyika.

Hayo yalielezwa na Makamu Mwenyekiti wa Taasisi hiyo,  Hanifa Mrisho, alipoongoza wanachama   wa taasisi hiyo  kufanya usafi na kufariji wagonjwa katika hospitali mbalimbali mkoani Dar es salaam, ikiwa ni kuadhimisha miaka 63 ya Uhuru  wa Tanganyika.

 Hanifa, amesema    Rais Dk. Samia, kushika uongozi wa ngazi ya juu ya Urais wa Tanzania ni mafanikio makubwa katika miaka 63 ya Uhuru  ambayo wanawake  hasa wanatakiwa kujivunia.

“Ni jambo ambalo wengi hawakutegemea katika kipindi hiki. Lakini tumempata Rais Dk. Samia na utendaji wake  umejipambanua uwezo mkubwa wa wanawake katika uongozi,”amesema   Hanifa. 

Ameeleza,  Taasisi ya Wanawake na Samia, itaendelea  kumuunga mkono Rais  Dk. Samia, katika kila hatua.

“Rais Dk. Samia, aliagiza sherehe hizi za uhuru tufanye kwa kupanda miti na usafi. Taasisi ya Wanawake na Samia, tuliona ni vyema tukafanya usafi katika Hospitali zetu  za Mkoa wa Dar es salaam, kuona wagonjwa na kugawa zawadi  mbalimbali kwa wagonjwa,”amesema.

Kuhusu uchaguzi mkuu  unaotarajiwa kufanyika mwakani, Hanifa alihimiza wanawake  kujitokeza  kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kwani Rais Dk. Samia ameonesha njia.

 Akizungumzia kuhusu mikopo ya asilimia 10  inayotolewa na Halmashauri kupitia mapato yake ya ndani kwa vikundi vya wajasiriamali wanawake, vijana na wenye ulemavu, Hanifa aliwataka watanzania kujitokeza.

“Wasikae majumbani. Wajitokeze  kwani zitawasaidia kujenga uchumi na kuchangia mapato ya serikali. Lakini wakikopa warejeshe,”amesema.

Mkurugenzi wa Idara ya Afya Wanawake na Samia Mkoa wa Dar es Salaam,Johari Kafuku,  amesema taasisi hiyo inamshukuru Rais Dk. Samia,  kwa uboreshaji mkubwa  wa huduma za afya.

“Hata vifo vya mama na mtoto vimepungua Tanzania kwa sababu ya Rais Dk. Samia kuboresha huduma, hususan ujenzi wa hospitali, vituo vya afya na  magari ya wagonjwa,”ameeleza Johari. 

 Kaimu Mganga Mfawidhi  wa Hospitali ya Mnazi Mmoja,  Linda Mukasa, amepongeza Taasisi ya Wanawake na Samia kwa  kufanya usafi  katika hospitali hiyo kwani  usafi ni jambo mtambuka.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...