Na Nasra Ismail Geita
Kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha mkoani Geita radi imeua wanafunzi saba wa darasa moja katika shule ya sekondari Businda iliyopo wilayani Bukombe mkoani Geita.
Mkuu wa wilaya ya Bukombe Paskasi Muragiri amethibitisha kuwepo kwa vifo saba na majeruhi 82 ambao walikutwa na kadhia hiyo wakiwa darasani wakiendelea na masomo.
Aidha Muragiri ameongeza kuwa wanafunzi waliopoteza maisha wa kiume ni 6 na wa kike mmoja ambapo bado hajatambua majina yao huku katika majeruhi 82 wawili bado wana hali mbaya.
"Bado hatujawatambua waliopoteza maisha, lakini baadhi ya majeruhi tayari wameongea na kutuambia majina yao. Kadri hali inavyoendelea, tutapata taarifa rasmi," ameongeza.
Mkuu huyo wa wilaya amesema kwamba, baada ya tukio hilo, madaktari walifika haraka shuleni hapo.
Hilo ni tukio la tatu kutokea mkoani Geita. Oktoba 18, 2019, wanafunzi 39 wa Shule ya Msingi Ihumilo, wilayani Geita, walijeruhiwa kwa kupigwa na radi, na Oktoba 17, 2018, wanafunzi sita wa Shule ya Msingi Emaco Vision walifariki dunia na wengine 23 kujeruhiwa kwa kupigwa na radi wakiwa darasani.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...