NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA

Zaidi ya washiriki 2000 wanatarajiwa kuchukua sehemu katika mbio za Kimataifa za Utalii Kanda ya Ziwa (Lake Zone International Marathon 2025) zitakazofanyika mkoani Mwanza.,kuhamasisha utalii na kuonesha fursa za uwekezaji zilizopo mkoani humu.

Akizungumza na waandishi wa habari, jijini Mwanza, leo Mkurugenzi wa Kilimanjaro One Sports Promotion Ltd, Mohamed Hatibu, amesema kuwa mbio hizi zitafanyika kuanzia Juni 27 hadi Juni 29, 2025, na zitakuwa na muktadha wa Tamasha la Utamaduni linalotarajiwa kufanyika mkoani Simiyu.
Amesema kuwa lengo la mbio hizo ni kutangaza fursa za uwekezaji na vivutio vya utalii vilivyopo mkoani Mwanza na Kanda ya Ziwa kwa ujumla, ili kuchangia katika kukuza uchumi wa mkoa na taifa zima.

"Vivutio vya utalii na fursa za uwekezaji katika Kanda ya Ziwa ni vingi, na ni muhimu kwa Watanzania kuvitangaza ili kuvutia wageni na kuingiza fedha za kigeni zinazosaidia maendeleo ya sekta mbalimbali," amesema Hatibu.

Mkurugenzi huyo ameongeza kusema kuwa utalii umeimarika kutokana na juhudi za Serikali ya Awamju ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, imefungua fursa na Diplomasia ya uchumi na kutangaza vivutio vya Tanzania kwa dunia.

Hatibu ameipongeza serikali kwa kuhakikisha kuwa nchi inakuwa sehemu salama kwa wawekezaji na kuimarisha amani, hali inayochochea maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa jamii na kueleza kuwa mbio hizo zitahusisha makundi mbalimbali, wakiwemo wajawazito, watoto, walemavu, wazee, na viongozi kutoka mikoa mbalimbali.

Pia, kupitia mbio hizo, wananchi watahamasishwa kujitokeza kwa wingi na kujiandikisha ili kushiriki katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 kwa amani.

Rhoda Kabarua, Msimamizi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Kanda ya Ziwa, amesema kwa kushirikiana na Kilimanjaro One Sports Promotion, mbio hizo zitakuwa ni makakati wa kutangaza vivutio vya utalii vya Mwanza ikiwemo Hifadhi ya Kisiwa cha Saanane na Makumbusho ya Utamaduni wa Wasukuma Bujora.

Amesema michezo hutoa fursa ya kukutanisha watu kutoka sehemu mbalimbali, hivyo mbio hizo zitakuwa na manufaa kiuchumi na zitaongeza mapato ya mkoa kupitia utalii.

Kwa upande wake, Bertha Nikundiwe, Mtaribu wa Huduma ya Afya ya Uzazi, Jiji la Mwanza, amesema mbio hizo pia zitatoa nafasi ya kutoa elimu ya afya ya wajawazito na umuhimu wa mazoezi katika kupunguza vifo vya watoto wachanga na wajawazito. 


Amesema wajawazito watashiriki kwa kutembea kwa dakika 20 hadi 30 na kufanya mazoezi mepesi, ambayo yanafaida kwa afya zao, ikiwemo kuboresha mzunguko wa damu na kupunguza shinikizo la damu, sukari na kupunguza uzito, huku akisisitiza licha ya faida hizo, wanawake wenye matatizo ya kiafya yanayohusiana na mimba hawataruhusiwa kushiriki.



 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...