TUME ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) imekabidhi rasmi eneo la mradi kwa mkandarasi TIL Construction Limited kwa ajili ya kuanza ujenzi wa jengo jipya la Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (STI)  jijini Dodoma.

Akizungumza baada ya kukabidhi eneo hilo la mradi Machi 25,2025 jijini Dodoma  Mratibu Msaidizi wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) kutoka COSTECH, Dkt. Aloyce Andrew, amesema hatua hiyo inalenga kurahisisha utoaji wa huduma kwa wadau wa taasisi hiyo.

"COSTECH ina jengo Dar es Salaam lakini tumeamua kujenga Dodoma kwa ajili ya kuwahudumia wadau wetu kwa ukaribu zaidi...,Jengo hili litakuwa na sehemu ya kuhudumia wabunifu, kuatamia kampuni changa, na kuratibu masuala ya utafiti," amesema Dkt. Andrew.

Amesema ujenzi wa jengo hilo, ambalo litajengwa eneo la Azina jijini humo  lenye mita za mraba 4,800, unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 12 kufuatia kusainiwa kwa mkataba Machi 24, 2025.

Kwa upande wake, Mshauri Elekezi wa mradi huo kutoka Kampuni ya MEKON, Benedict Martin, amesema wamekuwa wakihusika katika usanifu wa jengo hilo tangu mwaka jana (2024) baada ya kushinda zabuni kutoka COSTECH.

"Tulishirikiana na COSTECH kuhakikisha jengo hili linakidhi mahitaji yao yote. Pia tuna uhakika kwamba mkandarasi tuliyempata ana uwezo wa kutekeleza mradi huu kwa ubora unaotakiwa," alisema Martin.


Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa TIL Construction Limited, Ding Fubing, ameahidi kwamba kazi itafanyika kwa ufanisi na kumalizika kwa wakati.

"Tunaanza rasmi kesho kwa kulisafisha eneo lote, na baada ya wiki mbili hadi tatu, tutaingia kwenye ujenzi wenyewe. Tunaahidi kufanya kazi nzuri na kukamilisha mradi kwa muda uliopangwa au hata kabla," alisema Fubing.


Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi wa COSTECH, Imanuel Mgonja, amesema taasisi hiyo ina imani na mshauri elekezi pamoja na mkandarasi, akiwashukuru kwa kujitolea kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa ubora unaohitajika..

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...