Na Albano Midelo

Katika kona ya kusini mwa Tanzania, Kiwanja cha Ndege cha Songea kinasimama kama lango kuu la anga kwa wakazi wa mkoa wa Ruvuma na maeneo jirani.

 Kiwanja cha Ndege cha Songea kilichojengwa eneo la Ruhuwiko Manispaa ya Songea ni mojawapo ya viwanja 58 vinavyosimamiwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), kiwanja hiki kimepitia mabadiliko makubwa katika safari yake ya maendeleo, hasa katika mwaka wa fedha 2023/2024 ambapo serikali ilitoa Zaidi ya shilingi bilioni 37 kuboresha kiwanja hiki.

Historia na Uboreshaji wa Miundombinu

Katika juhudi za kuboresha huduma, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kupitia TAA ilitenga fedha kwa ajili ya kukarabati na kubadilisha jengo lililokuwa likitumiwa na mkandarasi mshauri kuwa jengo la abiria la kisasa.

Mradi huu unajumuisha ukarabati wa ukumbi wa kuondokea abiria wenye uwezo wa kuhudumia abiria 145 kwa wakati mmoja, ukumbi wa kuwasili abiria, pamoja na ujenzi wa maegesho ya magari ya kisasa.

Mbali na hayo, kiwanja hiki pia kimeboresha mifumo ya usalama kwa kusimika kamera za ulinzi, mfumo wa matangazo wa umma (PA system), pamoja na mifumo ya mawasiliano ya mtandao ili kuhakikisha huduma bora kwa wasafiri na wahudumu wa kiwanja.

Huduma za Ndege: Safari za Ratiba na Dharura

Ingawa safari za anga zinaendelea kukua, kwa sasa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) ndilo pekee linalotoa huduma za ratiba katika kiwanja hiki.

Shirika hilo linafanya safari mara tatu kwa wiki, yaani Jumatatu, Jumatano, na Ijumaa. Hii ni hatua kubwa kwa wakazi wa Songea na mkoa mzima wa Ruvuma ambao sasa wanapata huduma za anga kwa uhakika zaidi.

Ukuaji wa Idadi ya Miruko ya Ndege na Abiria

Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, kiwanja hiki kimeshuhudia ongezeko kubwa la miruko ya ndege na idadi ya abiria. Mnamo mwaka 2019, miruko ya ndege ilikuwa 304, lakini hadi mwaka 2023, idadi hiyo iliongezeka hadi miruko 468.

 Vilevile, idadi ya abiria imepanda kwa kasi kubwa kutoka abiria 2,025 mwaka 2019 hadi kufikia abiria 56,884 kufikia Juni 2024. Ongezeko hili linaashiria maendeleo ya uchumi na usafiri wa anga katika eneo hili.

Maendeleo yanayoshuhudiwa katika Kiwanja cha Ndege cha Songea yanatoa matumaini mapya kwa wakazi wa Ruvuma na Tanzania kwa ujumla.

Ukarabati wa miundombinu na ongezeko la safari za ndege ni dalili za ukuaji wa sekta ya anga na umuhimu wake katika kukuza uchumi wa ndani.

Kwa mwelekeo huu, Songea inazidi kujiimarisha kama kitovu cha usafiri wa anga kusini mwa Tanzania.

 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...