*Achangisha zaidi y ash. Milioni 600 katika harambee ya ujenzi wa maktaba, madarasa ya amali na ukumbi kwa ajili ya Seminari ya Agape

 

*Asema lengo ni kujenga jamii madhubuti na yenye kujitambua

*Asisitiza sekta ya elimu ni wakala wa mabadiliko

 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imeweka kipaumbele kikubwa cha uwekezaji katika sekta ya elimu nchini ili kujenga jamii madhubuti, yenye kujitambua, kujitegemea, kujiheshimu na kufuata misingi ya uwajibikaji na ubunifu.

Ameyasema hayo jana (Alhamisi, Machi 20, 2025) alipomuwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika harambee ya ujenzi wa maktaba ya kisasa, ukumbi wa mikutano na madarasa ya amali ya shule ya Seminari ya Agape inayomilikiwa na Kanisa la KKKT Dayosisi ya Kaskazini.

Katika harambee hiyo iliyofanyika kwenye Hotel ya Serena jijini Dar es Salaam ambapo zaidi ya shilingi milioni 600 zilikusanywa ikiwa ni ahadi na fedha taslimu, Waziri Mkuu alisema sekta ya elimu ni wakala wa mabadiliko katika jamii kiuchumi, kiteknolojia na kiutamaduni katika kuleta maendeleo ya nchi.

“Harambee hii ni hatua muhimu katika kuhakikisha kwamba tunafanya uwekezaji mkubwa katika elimu ya watoto wetu. Maktaba na madarasa ya amali katika Sekondari ya Agape yataleta manufaa mengi yenye tija kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla.”

Alisema ni muhimu kutambua kwamba bila ya uwekezaji mzuri katika elimu, hatuwezi kufika mbali. “Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejizatiti kuunga mkono juhudi za taasisi mbalimbali zinazochangia katika ujenzi wa Taifa letu.”

Mheshimiwa Majaliwa amesema ili kuwa na vijana wenye maarifa na ujuzi wa kukabiliana na changamoto za kijamii, kitaifa na kimataifa inahitaji kuwa na sekta ya elimu iliyo bora, imara na inayokidhi mahitaji ya jamii.

Waziri Mkuu amesema ili kuongeza fursa za elimu kwa Watanzania wote, Serikali imeongeza idadi ya shule za msingi kutoka 16,656 mwaka 2020 hadi 19,783 mwaka 2024 na shule za sekondari kutoka 5,001 mwaka 2020 hadi 5,926 mwaka 2024.

Naye, Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amelipongeza KKKT kwa kushirikiana na Serikali katika kuendeleza sekta ya elimu nchini.

Awali, Mhashamu Baba Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini, Dkt. Fredrick Shoo alitumia fursa hiyo kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri ya maboresho ya sekta ya elimu nchini. “Ninampongeza Mheshimiwa Rais Dkt Samia kwa maboresho ya sera ya elumu pamoja na ujenzi wa shule na ufadhili wa masomo ya sayansi.”

Akizungumzia kuhusu harambee hiyo alisema inalenga kukusanya shilingi bilioni 1.1 kwa ajili ya ujenzi maktaba ya kisasa, madarasa ya amali pamoja na ukumbi anuwai katika shule ya Seminari ya Agape ili kuunga mkono maboresho yaliyofanyika katika sera ya elimu.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...