NA BELINDA JOSEPH, SONGEA
Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Songea SOUWASA, Maswe Nyamhanga, ameitaja hatua ya upandaji miti kama sehemu ya juhudi za mamlaka katika kuhakikisha upatikanaji endelevu wa maji kwa sasa na kwa vizazi vijavyo, ambapo watumishi wa SOUWASA wameshiriki kikamilifu katika zoezi hilo ili kuimarisha uhifadhi wa mazingira.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukamilisha zoezi hilo, Nyamhanga amesema kuwa zoezi la upandaji miti lina lengo la kuhifadhi bonde la Mto Ruhila, ambalo ni chanzo kikuu cha maji katika manispaa ya Songea, Aliongeza kuwa juhudi hizi zinaendana sambamba na kuienzi wiki ya maji, ambapo upandaji miti utasaidia kuhifadhi vyanzo vya maji na kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi.
Amesema Serikali ilitoa fidia ya shilingi bilioni 2.8 kwa ajili ya kulipa fidia kwa wananchi wa eneo hilo ili kuepuka athari zinazoweza kutokea kutokana na shughuli za kibinadamu karibu na chanzo hicho, jambo ambalo linaonyesha dhamira thabiti ya serikali katika kuimarisha uhifadhi wa mazingira na upatikanaji wa maji.
Akizungumzia umuhimu wa miti Nyamhanga amesema uwepo wa miti katika vyanzo vya maji hupunguza maporomoko na huimarisha mzunguko wa maji na kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wa Songea unakuwa endelevu.
Kwa upande wa Mhandisi Jafari Yahaya, Kaimu Mkurugenzi wa uzalishaji na usambazaji kutoka SOUWASA, ameeleza kuwa takriban asilimiazaidi ya 70 ya maji yanayotumika katika Manispaa ya Songea yanatokana na bonde la Mto Ruhila, amewataka wakazi wa Chandarua kuendelea kuitunza miti hiyo iliyopandwa ili kuboresha na kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama unakuwa endelevu.
Wiki ya maji huanza tarehe 16 Machi na kuhitimishwa tarehe 22 Machi ambapo SOUWASA wametoa wito kwa wananchi wa Chandarua na maeneo jirani kuendelea kuitunza miti hiyo ili kuboresha hali ya mazingira na kuhakikisha upatikanaji wa maji kwa sasa na vizazi vijavyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...