Na Nihifadhi Abdulla
KATIKA jamii nyingi, wanawake wenye ulemavu wanakumbwa na
changamoto nyingi zinazowazuia kushiriki katika michezo. Pamoja na uwepo wa
mikataba ya kimataifa kuhusu haki za binadamu, bado kuna uelewa mdogo kuhusu
nafasi ya wanawake wenye ulemavu katika sekta ya michezo.
Miongoni mwa changamoto kubwa zinazotajwa kuathiri ushiriki
wao ni mitazamo potofu ya jamii juu ya Wanawake wenye ulemavu kwani mara nyingi
huonekana kama wasio na uwezo wa kushiriki michezo
Tafiti na ripoti za mashirika kama UNICEF zinaonyesha kuwa
ushiriki wa wanawake na wasichana wenye ulemavu kwenye michezo ni mdogo,
ukifikia kati ya asilimia 10 hadi 20 pekee.
Asha Mfundo kocha wa timu ya wanawake Zanzibar anasema hiyo
inachangiwa na kosefu wa miundombinu rafiki
skuli pamoja na viwanja vingi vya michezo kutozingatia mahitaji ya watu
wenye ulemavu.
"Ukosefu wa elimu Kwa wazazi pia kikwazo kwani wazazi
wengi hawana uelewa wa kutosha kuhusu umuhimu wa michezo kwa watoto wao wenye
ulemavu "Amesema Mfundo
Riziki Sharif Hija,
mwanafunzi mwenye ulemavu wa ngozi
wa darasa la saba katika Skuli ya Kilimahewa, anaeleza kuwa
anapenda mpira wa miguu, lakini skuli
yake haina uwanja wa michezo. "Hili limekuwa kikwazo kikubwa kwangu kwani sina mahali pa kufanya mazoezi
wala kushiriki mashindano ya michezo kama wanafunzi wengine labda kupitia clabu
na Kwa wiki siku moja tu"
Pamoja na changamoto hiyo, Riziki anaamini kuwa michezo ina
faida nyingi, ikiwa ni pamoja na kujenga afya ya mwili na akili pamoja na
kupanua fursa za maisha, "natoa wito kwa jamii na wadau wa elimu
kuhakikisha kuwa watoto wenye ulemavu tunapata
fursa sawa ya kushiriki michezo kwa kuimarisha miundombinu"anasema
Riziki
Asha Mbwana, mzazi wa mtoto Riziki anasema kuwa jamii inapaswa kupata elimu
zaidi kuhusu haki za watoto wenye ulemavu kushiriki michezo, "Mimi
nimepata changamoto kutoka kwa baadhi ya
wanajamii, ambao huwatenga watoto wenye ulemavu au kuwanyima fursa za kushiriki
katika shughuli mbalimbali za kijamii, ikiwemo michezo"
"Kwa kupitia juhudi za taasisi mbalimbali zinazotetea
haki za watu wenye ulemavu, Mimi binafsi nimeanza kupata mwanga kuhusu umuhimu
wa kumtia moyo mtoto wangu kushiriki michezo"
Hivyo anahimiza wazazi wengine kutobagua watoto wao wenye
ulemavu bali wawape nafasi sawa ya kushiriki katika shughuli zinazoweza
kuwajenga kimwili na kiakili.
Taasisi mbalimbali, kwa kushirikiana na Serikali, zimeanza
kutoa elimu kwa jamii ili kuongeza ushiriki wa wanawake wenye ulemavu katika
michezo.
Hija Ramadhan kutoka Shirika la GIZ anasema katika jitihada za kutengeneza usawa wa kijinsia ni
pamoja na kuhakikisha wadau wanashirikiana kuwalinda watoto na wanawake dhidi
ya ukatili.
“ Lengo hili tunaweza kulifikia kwa kutumia mbinu tofauti
Kwa kutoa mafunzo Kwa watu na Wadau
mbalimbali kuhamashisha Michezo
kwa Maendeleo,” amesema Ramadhan
Katika juhudi za kuimarisha usawa wa kijinsia na kuhamasisha
michezo kwa maendeleo, Dkt. Mzuri Issa, Mkurugenzi wa Chama Cha waandishi wa
habari wanawake TAMWA ZNZ, amesisitiza umuhimu wa kuendeleza na kuhamasisha
michezo kwa wote ili kukuza ushiriki wa jinsi na hali zote katika michezo.
"Tuwe mifano mizuri ya kuwa na heshima katika jamii,
kwasababu sisi tuna nafasi ya kupata mawaidha sehemu mbalimbali ya stadi za
maisha. Hivyo tuna kila sababu ya kuendeleza kuimarisha na kuhamasisha michezo
kwa wote,” anasema Dkt Mzuri
Afisa ustawi wa jamii, Salma kombo Abdalla, anasisitiza kuwa
jamii inapaswa kubadili mitazamo hasi na badala yake iweke mazingira
yanayowajenga wasichana na wanawake wenye ulemavu ili washiriki kikamilifu
kwenye michezo.
“Kushiriki kwa wanawake wenye ulemavu kwenye michezo siyo tu suala la burudani bali ni haki yao ya msingi. Jamii inapaswa kubadili mitazamo, kuweka mazingira jumuishi, na kuhakikisha kuwa kila mtu anapata nafasi sawa ya kushiriki kwenye michezo,”Anasisitiza Salma
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...