Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki, akimwagilia maji mti alioupanda katika makaburi ya mashujaa wa Afrika Kusini yaliyopo Morogoro, kama kumbukumbu ya mashujaa waliopigania uhuru wa nchi yao wakati wa harakati za ukombozi.

AngloGold Ashanti imesema kuwa inajivunia ushirikiano wake na taasisi binafsi ya Rais wa zamani wa Afrika Kusini , Thabo Mbeki inayojulikana kama ‘Thabo Mbeki Foundation’ katika kuleta muamko wa maendeleo barani Afrika ili kufikia malengo ya 2063 yaliyowekwa na bara hilo ya kimaendeleo kupitia kauli mbiu ya ‘Africa We Want- Afrika tunayoitaka.

Akizunguma wakati wa ziara ya Rais huyo wa zamani wa Afrika Kusini uliojumuisha zaidi ya Waafrika Kusini 50 katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) mkoani Morogoro kwa ajili ya kutembelea makaburi ya mashujaa wa Waafrika Kusini waliopigania uhuru wa nchi hiyo kupitia chama cha African National Congress (ANC), Simon Shayo, Makamu wa Rais wa Masuala ya Uendelevu (Afrika) katika AngloGold Ashanti amesema wanajivunia kuwa sehemu ya safari hii ya mageuzi ya bara la Afrika.

“AngloGold Ashanti inashirikiana na taasisi ya Thabo Mbeki katika mpango huu wa kuleta muamko wa maendeleo kwa bara la Afrika kwa sababu ni mdau wa maendeleo katika nchi mbalimbali katika bara hili kupitia sekta ya madini,”

“Ushiriki wa sekta binafsi katika mpango huu sio tu kibiashara, bali kushiriki katika kuweka daraja kwa watu wa kawaida na viongozi mashuhuri kujadili mambo yanayohusu bara hili na ndio maana AngloGold Ashanti tumeamua kuwa sehemu ya historia hii,”

“Kupitia uwekezaji wetu, tunagusa moja kwa moja maisha ya watu, wakiwemo vijana na maendeleo ya nchi mbalimbali kupitia uwekezaji wetu,” amesema Shayo.

Amesema kuwa ushirikiano wa AngloGold Ashanti, Taasisi ya Thabo Mbeki na Chuo Kikuu cha Afrika Kusini (UNISA) unaonesha nia ya dhati ya kuleta chachu ya maendeleo katika maeneo mbalimbali ikiwemo uongozi ili kufikia malengo yaliyowekwa na bara hili.

“Kupita ubia wetu, tunapenda kuona ustawi wa bara la Afrika kwa watu wake na rasilimali zake ikiwemo madini ili kuharakisha maendeleo ya bara hili na kuondoa utegemezi kutoka mataifa ya kigeni,”

“Ndio maana mjadala wa 15 wa mwaka huu umekuwa na mijadala mbalimbali, ikihusika viongozi mbalimbali akiwemo Rais mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete kwa ajili ya kujadili kwa kina mambo ambayo yatakayosaidia bara hili kupiga hatua kwa haraka na kuangalia namna ya kuondoa vikwazo vilivyopo,” amesema Shayo.

Katika msafara huo uliohusisha viongozi mbalimbali akiwemo Waziri Mkuu mstaafu wa Tanzania Jaji Joseph Sinde Warioba na maofisa kutoka Ubalozi wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki aliongoza msafara wa kutembelea makaburi ya wapigania uhuru hao wa Afrika Kusini walioongozwa na Rais wa zamani Nelson Mandela na kutoa wito wa nchi za Afrika kushikamana katika kujiletea maendeleo na kuwaenzi wapigania uhuru katika bara hili.

Vusi Maqabela kutoka taasisi ya Thabo Mbeki Foundation amesema kuwa amefurahia sana kuona makaburi ya wapigania uhuru wa nchi yake, jambo ambalo hapo awali alikuwa anajifunza historia yao wakati akiwa shuleni.

“Tunawashukuru sana waandaaji wa mjadala huu kwa kusaidia bara la Afrika kuleta muamko kupitia historia yake kwa ajili ya vizazi vya sasa,” amesema Magabela.

Naye Profesa Anthoni Van Nieuwkerk wa UNISA anayejihusisha na mahusiano ya kimataifa amesema kuwa mjadala wa mwaka huu ambao Taasisi ya Thabo Mbeki umeichagua Tanzania kuwa mwenyeji unaamsha tena umuhimu wa viongozi wa Afrika kushiriki kikamilifu katika ajenda hii.

“Nitakachokikumbuka katika ziara hii ni kitendo cha Thabo Mbeki kupanda mti katika katika eneo hili muhimu la kihistoria kwa Afrika Kusini mkoani Morogoro, kitendo ambacho kinazidi kuzidisha udugu uliopo kati ya nchi hizi na umuhimu wa nchi za Afrika kushikamana,” amesema.

Kumekuwa na mfululizo wa matukio mbalimbali ya mijadala kuelekea Hotuba ya Siku ya Afrika, ambayo yatakamilika kwa meza ya majadiliano ya ngazi ya juu itakayoandaliwa na AngloGold Ashanti pamoja na Rais Mbeki siku ya Ijumaa tarehe 23 Mei, ikifuatiwa na Hotuba rasmi siku ya Jumamosi tarehe 24 Mei katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...