• Benki ya Stanbic Tanzania imefungua tawi lake la 15 mkoani Geita, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza ujumuishaji wa kifedha na kukuza uchumi katika sekta muhimu kama madini na kilimo.
• Upanuzi huu unaendana na miaka 30 ya huduma nchini Tanzania, ukionyesha juhudi za benki kuwawezesha wanawake, jamii na biashara kupitia huduma maalum za kifedha.
• Stanbic inaendelea kuwa mdau mkubwa wa maendeleo ya kikanda kupitia ushiriki wake katika majukwaa ya kiuchumi na ushirikiano barani Afrika Mashariki.
Geita, Mei, 2025 – Benki ya Stanbic Tanzania imezindua rasmi tawi lake la 15 nchini, likiwa katika mkoa wa Geita—eneo muhimu kiuchumi kutokana na shughuli za madini na kilimo. Uzinduzi huu unaendana na dhamira ya benki hiyo ya kuongeza ujumuishaji wa kifedha na kuchochea maendeleo endelevu ya kiuchumi nchini.
Tawi hilo lilizinduliwa mwishoni mwa wiki na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde. Tawi hili linafunguliwa wakati Benki ya Stanbic ikiadhimisha miaka 30 tangu ianze kutoa huduma nchini Tanzania, ikiwa ni ishara ya msimamo thabiti wa benki hiyo katika kutoa suluhisho za kifedha bunifu zinazoboresha maisha ya wananchi na kusaidia ukuaji wa biashara na uchumi kwa ujumla.
Ikiwa ni benki ya tatu kwa ukubwa nchini Tanzania, Benki ya Stanbic inaendelea kuonyesha uthabiti na uongozi katika utoaji wa huduma bora za kifedha.
“Uamuzi wa kufungua tawi Geita umetokana na mchango mkubwa wa mkoa huu katika uchumi wa Taifa, hasa kupitia uzalishaji wa dhahabu, kilimo na biashara. Kupitia tawi hili, Benki ya Stanbic inalenga kuziba pengo la upatikanaji wa huduma bora za kifedha kwa wakulima, wachimbaji, wafanyabiashara na wananchi wa kawaida—na hivyo kuchochea biashara, uwekezaji na maendeleo ya kiuchumi katika mkoa huu na Taifa kwa ujumla,” alisema Fredrick Max, Mkuu wa Idara ya Biashara, Benki ya Stanbic.
“Lakini kwa vile sasa tumekuwa sehemu ya jamii ya wana Geita, kupitia sera yetu ya kurudisha kwa jamii, leo tumekabidhi madawati 200 ambayo yatatumika na wanafunzi wa shule za mkoa huu, tukiwa tunaunga mkono juhudi za Serikali katika kujenga mazingira bora ya elimu kwa watoto wetu. Vilevile, tumetoa miche 200 ya miti kwa ajili ya kupandwa katika shule na maeneo ya jamii kama sehemu ya mchango wetu katika kulinda mazingira na kuendeleza maendeleo endelevu kwa vizazi vijavyo.” Aliongeza.
Akizungumza baada ya kuzindua tawi hilo jijini Geita, Waziri wa Madini, Mhe, Anthony Mavunde alisema amefarijika kusikia kuwa benki hii inalenga kutoa huduma si tu kwa kampuni kubwa bali pia kwa wachimbaji wadogo, wanawake wajasiriamali, na wakulima wanaohitaji huduma za kisasa za kifedha ili kukuza mitaji yao na kuboresha maisha yao.
“Serikali, kupitia Wizara ya Madini, inaendelea kuimarisha mazingira ya uwekezaji na ushirikiano kati ya sekta binafsi na ya umma. Tuko tayari kushirikiana na taasisi kama Stanbic Bank kuhakikisha kuwa kila mdau katika mnyororo wa thamani wa madini anawezeshwa na anaungwa mkono,” alisema.
Katika sekta ya madini, benki imetoa msaada wa kifedha kwa mashirika makubwa na biashara ndogo zinazohudumia sekta hiyo, ikisaidia katika maboresho ya vifaa, uwekezaji wa mitaji na ufanisi wa shughuli. Kwa upande wa kilimo, Stanbic imewawezesha wakulima wadogo na wafanyabiashara walio kwenye mnyororo wa thamani wa sekta ya kilimo kupata vifaa vya kisasa, mifumo ya umwagiliaji na huduma za kifedha shirikishi, hivyo kuongeza uzalishaji na upatikanaji wa masoko.
Mwezi Machi mwaka huu, kuelekea Siku ya Wanawake Duniani, benki ilifanya Kongamano la Maendeleo ya Wanawake mkoani Geita, ikisisitiza umuhimu wa kuwawezesha wanawake kiuchumi. Kupitia vituo vya ubunifu, mafunzo ya ujasiriamali na bidhaa maalum za kifedha kwa wanawake, Stanbic inaendeleza usawa na ujumuishaji.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martin Shigella alisema: “Uwepo wa Benki ya Stanbic hapa si jambo dogo. Ni uthibitisho kwamba mkoa huu unatambulika kama eneo la fursa, uthabiti na uwezo wa kukuza uchumi wa taifa kwa kiwango kikubwa.”
“Kwa miaka kadhaa sasa, tumekuwa tukifanya kazi ya kuhakikisha mazingira ya uwekezaji katika mkoa huu ni rafiki, wazi, na yenye usaidizi wa karibu kutoka kwa uongozi wa serikali ya mkoa. Tunapopokea taasisi kama Stanbic, tunapokea pia wajibu wa kuhakikisha wanafanikiwa na wanatoa mchango wa moja kwa moja kwa wananchi.” Alihitimisha.
Waziri wa madini, Mhe. Anthony Mavunde akikata utupe katika uzinduzi wa tawi jipya la benki ya Stanbic Tanzania, Geita. Kushoto kwa Mhe. Anthony Mavunde ni Martin Shigela, mkuu wa mkoa geita na kulia kwake ni Fredrick Max, Mkuu wa kitengo cha biashara benki ya Stanbic.
Mhe. Anthony Mavunde, Waziri wa Madini, akikabidhiwa rasmi madawati 200 pamoja na miche 200 ya miti kutoka kwa Benki ya Stanbic katika hafla ya uzinduzi wa tawi jipya la Geita. Pembeni ni Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martin Shigella.
Mhe. Anthony Mavunde, Waziri wa Madini, akisaini kitabu cha wageni katika hafla ya uzinduzi wa tawi jipya la benki ya stanbic tanzania mkoani Geita. Wengine kwenye picha ni Omari Mtiga, Mkuu wa Kitengo cha Wateja Maalum na wateja binafsi, Fredrick Max, Mkuu wa Kitengo cha Biashara, pamoja na Geoffrey Kondo, Meneja wa Tawi la Geita.
Meza kuu ya hafla ya uzinduzi wa tawi la Stanbic Bank Geita ikiongozwa na Mhe. Anthony Mavunde (Waziri wa Madini), Mhe. Martin Shigella (Mkuu wa Mkoa wa Geita), pamoja na Fredrick Max (Mkuu wa Kitengo cha Biashara – benki ya Stanbic Tanzania).
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...