▪️ Maabara ya Kisasa ya Madini kujengwa Dodoma

▪️ Helikopta kununuliwa na kufungwa vifaa maalum kwa ajili ya utafiti

▪️ Wachimbaji Wadogo, Wanawake na Vijana ni sehemu ya Kipaumbele


Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kauli moja wamepitisha kwa kishindo Bajeti ya Ofisi ya Wizara kwa Mwaka wa Fedha 2025/26 yenye takribani Shilingi bilioni 224.98 kwa ajili ya wizara na taasisi zilizo chini yake kutekeleza majukumu yake.

Bajeti hiyo iliyopitishwa kwa uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa wabunge, inalenga kuendeleza utekelezaji wa miradi ya kimkakati katika Sekta ya Madini pamoja na kuimarisha utoaji wa huduma na utendaji kazi wa wizara na taasisi zake.

Awali, Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde akiwasilisha Hotuba ya Mpango wa Mapato na Matumizi ya Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha wa Serikali wa 2025/2026 leo Mei 02, 2025 Bungeni Jijini Dodoma, ameeleza Bunge kuwa kiasi hicho ni kwa ajili ya kuwezesha Wizara ya Madini na taasisi zake kutimiza majukumu na wajibu wao.

“Mheshimiwa Spika, ili Wizara iweze kutekeleza majukumu na malengo yaliyopangwa ikiwemo ukusanyaji wa maduhuli ya shilingi 1,405,537,268,755.00 (Trilioni 1.4) naomba Bunge lako Tukufu liridhie na kupitisha makadirio ya shilingi 224,984,150,000.00 kwa ajili ya matumizi ya Wizara na Taasisi zake kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026” ameeleza Mavunde.

Kwa mujibu wa Waziri Mavunde, mchanganuo wa bajeti hiyo, Shilingi 124,604,788,000.00 (Bilioni 124.6) sawa na asilimia 55.38 ya bajeti yote imetengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambayo inalenga kuleta tija na kuchochea ukuaji wa sekta ya madini hapa nchini.

Ameeleza kuwa, Shilingi 100,379,362,000.00 (bilioni 100.3) sawa na asilimia 44.62 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida, ambapo kati ya hizo, Shilingi 24,268,585,000.00 zimetengwa kwa ajili ya mishahara ya watumishi (PE) huku Shilingi 76,110,777,000.00 ikitengwa kwa ajili ya matumizi mengineyo (OC) ya Wizara pamoja na taasisi zilizo chini yake.

Kupitishwa kwa bajeti hiyo kwa kauli moja kunatoa ishara ya dhamira ya Serikali kuendelea kuwekeza kwa nguvu katika sekta ya madini ili kuhakikisha inachangia kikamilifu katika uchumi wa taifa na ustawi wa wananchi.

Katika hotuba yake, Waziri Mavunde ameeleza Wizara kuja na Programu maalum ya “Mining for a Brighter Tomorrow (MBT)” inayolenga kuhamasisha ushiriki wa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye mahitaji maalum kwenye mnyororo mzima wa shughuli za madini.

Aidha, kupitia, maono ya Vision 2030; Madini ni Maisha na Utajiri, Wizara inalenga kuifanya sekta ya madini kuwa kichocheo cha maisha ya Watanzania kwa kufanya utafiti kina wa jiosayansi kwa kutumia teknolojia ya kisasa (airborne geophysical survey) ili kuongeza kanzidata ya jiololia ya nchi sambamba na kuunganisha sekta ya madini na sekta nyingine kama za maji, ardhi, afya, kilimo, kiuchumi n.k.

Katika eneo la Utafiti wa Kina na Teknolojia ya Kisasa, Waziri Mavunde amesema, Serikali kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini (GST) itaongeza utafiti wa jiofizikia kwa njia ya ndege hadi kufikia 34% ya eneo la nchi ifikapo 2026, sambamba na Ujenzi wa maabara mpya ya kisasa (State-of-the-Art Geoscientific Laboratory) Dodoma utaongeza uchunguzi wa madini ya kisasa kama lithium, nickel, cobalt lakini pia ununuzi wa Helicopter itakayofungwa vifaa maalum vya kisasa kwa ajili ya utafiti na vifaa vya kisasa vinanunuliwa kuharakisha ukusanyaji wa taarifa.

Vilevile, Waziri Mavunde ameeleza mpango wa Serikali kuendelea kuboresha mazingira kwa wachimbaji wadogo kwa kuwaunganisha na taasisi za kifedha na mabenki ili waweze kupata mikopo na kukuza mitaji yao, kuwapatia teknolojia za kisasa za uchimbaji na uchakataji madini, elimu na maeneo ya uchimbaji na hivyo kuendesha shughuli zao kwa tija Zaidi.

Pia, Wizara ya Madini itaendelea na mkakati wake wa kujenga mfumo wa kidijitali kwa ajili ya kusimamia Sekta ya Madini kwa ufanisi na tija na kwa manufaa ya kiuchumi na taifa kwa ujumla. 





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...